Malezi ya mtoto wa kambo ni moja ya changamoto kubwa zinazowakumba wazazi wa kisasa, hasa katika familia zilizoanzishwa baada ya ndoa ya kwanza au baada ya wazazi wa awali kuachana.
Mtoto wa kambo si wako kidamu, lakini kwa mazingira ya ndoa au uhusiano, unahusika moja kwa moja katika malezi yake.
Haha hivyo, kumlea mtoto wa kambo si kazi rahisi, lakini pia si jambo lisilowezekana. Kinachohitajika zaidi ni hekima, upendo wa kweli, subira, na mawasiliano ya wazi.
Tunaangazia nanna unavyoweza kuishi na mtoto wa aina hii, akahisi thamani sawa na mtoto uliyemzaa.
Kubali nafasi yako mpya
Hatua ya kwanza ni kujikubali wewe mwenyewe kuwa sasa ni sehemu ya maisha ya mtoto huyo.
Usijaribu kuchukua nafasi ya mzazi wa damu, bali jenga nafasi yako mwenyewe ya kipekee katika maisha ya mtoto.
Watoto mara nyingi huwa waangalifu na wanahitaji muda wa kukuamini, hivyo kuwa mvumilivu. Usijilazimishe kumpenda au kupendwa papo kwa hapo, lakini jenga msingi wa uhusiano wenu kidogo kidogo.
Watoto wa kambo mara nyingi hupitia hisia za mchanganyiko kama huzuni, hasira, kukosa imani na hata hofu ya kupoteza nafasi ya mzazi wao wa awali. Wakati mwingine wanaweza kukuona kama tishio kwa uhusiano wao na mzazi wao wa damu. Hali hii ni ya kawaida.
Ni muhimu kuelewa kuwa mtoto anaweza kuwa katika hali ya mpito kihisia, na anahitaji mtu atakayemsikiliza, si wa kumhukumu au kumlazimisha kubadilika haraka.
Kama mzazi wa kambo, usianze kwa kujenga hofu kwa mtoto kwa kujaribu kuwa mkali au kuleta nidhamu kali. Badala yake, anza kwa kujenga urafiki. Jifunze anachopenda, zungumza naye, cheka naye, na mshirikishe katika shughuli za kifamilia. Mtoto akikuzoea na kujenga uaminifu kwako, atakuwa tayari kukusikiliza hata pale utakapomwelekeza au kumkosoa.
Ushirikiano na mzazi wa damu ni muhimu
Ikiwa mzazi wa damu wa mtoto yupo na anahusika katika maisha ya mtoto, basi ni muhimu kuwa na uhusiano mzuri na yeye kwa ajili ya ustawi wa mtoto.
Epuka migogoro au mivutano ya mara kwa mara ambayo inaweza kumchanganya mtoto au kumweka katika hali ya kuchagua upande.
Mtoto anahitaji kuona mshikamano wa watu wote wanaomlea ili ajisikie salama na kupendwa.
Katika kujenga uhusiano mzuri na mtoto wa kambo, usisahau kuweka mipaka ya heshima. Mtoto ajue kuwa unamheshimu kama mtoto, lakini pia anapaswa kukuheshimu kama mzazi au mlezi. Usikubali dharau au lugha zisizofaa kwa kisingizio cha kumzoea. Hii itasaidia kuweka mazingira ya nidhamu bila kuonekana mkali kupita kiasi.
Shirikiana na mwenza wako
Mzazi wa damu anapaswa kuwa kiunganishi muhimu kati yako na mtoto.
Ni muhimu kuwa na mazungumzo ya wazi na mwenza wako kuhusu majukumu yako katika malezi ya mtoto. Elewaneni kuhusu mambo ya msingi kama nidhamu, ratiba, maadili, na mambo mengine yanayohusu maisha ya kila siku ya mtoto. Usijaribu kumpinga mwenza wako mbele ya mtoto au kumpinga mtoto mbele ya mzazi wake, kwani hili linaweza kuharibu uhusiano wenu kwa ujumla.
Ikiwa una watoto wa damu katika familia hiyo, ni muhimu kuwa makini kutotoa upendeleo. Watoto wa kambo mara nyingi huwa na hisia kuwa hawapendwi kama wengine.
Hakikisha kila mtoto anahisi kuwa na nafasi sawa, kupendwa, kusikilizwa na kupewa haki sawa. Hili linaweza kuwa gumu, lakini ni la msingi katika kujenga familia yenye mshikamano.
Uhusiano na mtoto wa kambo haujengwi kwa siku moja. Inahitaji muda, kujitoa, na moyo wa upendo. Tafuta muda wa kuwa naye peke yako kama kutembea pamoja, kufanya kazi zake za shule pamoja au hata kutazama runinga.
Muda huu maalum hujenga uhusiano na kusaidia mtoto kujisikia kuwa ni sehemu ya familia.
Sikiliza zaidi kuliko kusema
Wazazi wa kambo wakati mwingine hukimbilia kutoa maelekezo, hukumu au ushauri, kabla ya kuelewa hali halisi ya mtoto.
Jifunze kusikiliza hata kimya chake kwani kinaweza kukuambia mengi. Mtoto anapojisikia kuwa unasikiliza bila kumhukumu, anaweza kufunguka na kuanza kukuona kama mtu wa kuamini.
Kumlea mtoto wa kambo kunaweza kuwa changamoto ya kihisia kwa mzazi wa kambo. Usione aibu kuomba ushauri kutoka kwa wataalamu wa malezi, wanasaikolojia au hata kutoka kwa marafiki na familia waliowahi kupitia hali kama yako.
Msaada wa kiushauri unaweza kusaidia kujenga uhusiano bora na mtoto na kupunguza msongo wa mawazo.
Kifupi, kumlea mtoto wa kambo ni safari inayohitaji moyo wa kipekee, lakini ni safari inayowezekana na yenye thawabu kubwa hata upande wa dini.
Inahitaji kujitoa, kuvumilia, kuelewa, na zaidi ya yote kumpenda bila masharti. Watoto hawachagui mazingira waliyozaliwa, lakini sisi watu wazima tuna nafasi ya kuyabadilisha maisha yao kwa kuwapa mazingira salama, yenye upendo na matumaini. Ukiamua kwa dhati kuwa mzazi bora kwa mtoto wa kambo, unaweza kuwa miongoni mwa watu wachache wanaofanya mabadiliko makubwa katika maisha ya mtoto ambaye sio damu yako.