“Uwanja huu ni fursa kwa vijana wa Kyerwa, na siku moja timu kubwa za Tanzania zitakuja kucheza hapa,” alisema Nsekela kwa shauku.
Aliongeza kuwa, “Hata hivyo, naomba kuwaasa wazazi kuwa michezo ni nyongeza kwa elimu na si badala yake, hivyo ni vyema kwa wazazi kuwasaidia mtoto wako kuwa bora darasani, ndipo talanta yake kiwanjani itakapokuwa na msingi imara.”
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa, aliyekuwa mgeni rasmi, alimtaja Nsekela kwa kukumbuka asili yake na kuwekeza kwenye mradi mkubwa na wenye tija kwa wananchi wa Kyerwa.
“Ninamshukuru sana Ndugu Nsekela kwa kuwekeza kwenye maeneo haya. Hii ni kumbukumbu ya kudumu na itaweza kuchangia katika kuleta maendeleo nyumbani kwao,” alisema Mwassa.
Aidha, alionya wasimamizi na jamii kwa ujumla kuutunza uwanja huo kwa dhati na kuuhifadhi kwa manufaa ya vizazi vijavyo, akikataza vitendo vya uharibifu.
Kwa upande wake Msemaji wa Taasisi ya Abdulmajid Nsekela (Abdulmajid Nsekela Foundation), Tully Esther Mwambapa, alisema kuwa uwanja huo sio wa mpira wa miguu pekee, bali utajumuisha viwanja kamili vya mpira wa kikapu na pete, pamoja na eneo maalum la michezo ya riadha.
Aliongeza kuwa uwanja huo umewekwa majukwaa ya kisasa na salama kwa ajili ya watazamaji, na utakuwa ni wa kiwango cha kimataa.
Wadau wa michezo na viongozi wa jamii wamepongeza juhudi hizo za kuwezesha kupata uwanja mpya, kwani utawavutia vijana kuonyesha na kulea talanta zao kitaalamu. Zaidi ya hayo, wamebainisha kuwa uwanja huo utajenga uchumi wa ndani kwa kuwapa fursa wadau mbalimbal wakiwemo wakulima wadogo, wafanyibishara wa vyakula na vinywaji, na wauzaji wa vifaa vya michezo kuingia kwenye mnyororo wa uchumi unaozaliwa na shughuli za kimichezo.
Hatua hiyo ya uwekezaji inaonekana kuwa chanzo kipya cha furaha, umoja na matumaini kwa wananchi wa Kyerwa na mkoa mzima ya Kagera.
Sambamba na uzinduzi wa uwaja huo Taasisi ya Abdulmajid Nsekela ilitoa vifaa vya michezo kwa timu 16 wilayani humo ambazo zitakwenda kutumika katika mashindano ya Nsekela Cup ambayo pia yalizinduliwa rasmi siku ya uzinduzi wa uwanja huo. Pia taasisi hiyo imefanikisha uchibwaji wa kisima cha maji kwaajili ya kusaidia kuutunza uwanja huo kwa kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa maji. kisima hicho pia kimekua mkombozi kwa uunganishwaji wa mabomba ya maji katika shule zilizopo maeneo ya jirani na uwanja huo, hivyo kuwezesha wanafunzi wa shule hizo kupata maji safi na salama na kupunguza adha ya upatikanaji wa maji.

