Watoa Sh4.6 bilioni kujenga shule ya wasichana Kijiji cha Terati

Simanjiro. Wadau wa elimu ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na Serikali, wametoa zaidi ya Sh4.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana ya Tukuta katika Kijiji cha Terati, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Mradi huo ambao ni ujenzi wa madarasa 12, maabara za sayansi nne, mabweni sita,  vyumba vya walimu 16 na vyumba vya utawala, unalenga kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wa kike hususan wanaoacha  shule kutokana na umbali mrefu pamoja na kuboresha kiwango cha ufaulu.

Mradi wa shule hiyo ambayo itakuwa ni ya kidato cha kwanza hadi cha sita, unatekelezwa na Shirika la ECLAT Development Foundation Tanzania chini ya ufadhili wa Shirika la Upendo Foundation kutoka Ujerumani, lengo ikiwa ni kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa kike katika kijiji hicho.

Ofisa mradi, Bakiri Angalia amesema kwa kipindi  cha miaka tisa, shirika hilo limejenga miradi 55 yenye thamani ya Sh26 bilioni katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ufundi nchini.

“Uanzishwaji  wa sekondari hii ni fikra na mawazo ya pamoja kati ya uongozi wa Wilaya ya Simanjiro, washirika wa maendeleo na jamii, na lengo  kuhudumia wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita kwa idadi inayokadiriwa kuwa na wanafunzi kati ya 760 hadi 800,” amesema Angalia.

Amesema lengo la mradi huu ni kuhakikisha kunakuwa na miundombinu bora ya kufundishia na kujifunzia kwa wasichana.

“Tunataka kupunguza kiwango cha wanafunzi kuacha shule na kuboresha ufaulu wa wasichana katika wilaya hii,” amesema Angalia.

Aidha, amesema ujenzi wa mradi huo utafanyika kwa awamu tano kuanzia mwaka huu na utakamilika mwaka 2029 huku akisema baada ya awamu zote za ujenzi kukamilika, majengo na vifaa vyote vitakabidhiwa kwa Serikali kwa ajili ya umiliki na uendeshaji.

“Mradi huu utagharimu Sh4.6 bilioni na Sh216 milioni thamani ya ardhi iliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Terati lakini miundo mbinu itakayojengwa ni madarasa 12, maabara za sayansi nne, mabweni sita na kila bweni litakuwa na wanafunzi 120, vyumba vya walimu 16 na vyumba vya utawala,” amesema.

Ameishukuru Serikali kwa kuboresha uhusiano wa kidiplomasia unaowezesha asasi zisizo za kiserikali kutekeleza majukumu yake kwa maendeleo ya wananchi na kushiriki katika ujenzi wa Taifa.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara ambaye pia ni Mwenyekiti wa ECLAT Foundation, Peter Toima amesema mradi huo utawasaidia kupunguza changamoto za wananchi hususan wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali kuendelea kuboresha maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini.

“Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa sana katika sekta ya elimu hapa nchini. Kazi inayofanyika hapa Terati inatupa fursa ya kutekeleza sera ambazo amesimamia na kuzindua Rais wetu,” amesema Profesa Mkenda.

Amewapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kutoa eneo lao la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.