Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga, imewahukumu adhabu ya kifungo cha miaka 20 Anderson Luhozya na Habona Antony baada ya kukiri kuua bila kukusudia.
Wakati Mahakama hiyo ikiwahukumu adhabu hiyo, imemuachia huru Maliki Nestory, kwa masharti ya kuwa chini ya usimamizi wa baba yake mzazi Nestory Telemka kwa kipindi cha miaka miwili bila kutenda kosa lolote, kutokana na kutenda kosa hilo akiwa chini ya umri wa miaka 18.
Hukumu hiyo ilitolewa Agosti 22, 2025 na Jaji Thadeo Mwenempazi aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ambapo baada ya washtakiwa hao wote kukiri shitaka la kuua bila kukusudia lililokuwa likiwakabili.
Hata hivyo, Jaji Mwenempaze amesema kuwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 20 jela inajumuisha na miaka mitano ambayo washtakiwa walikaa mahabusu wakati kesi yao ikiendelea kusikilizwa, hivyo kuanzia ilipotolewa hukumu hiyo watatumikia kifungo cha miaka 15.
Katika kesi hiyo, watatu hao walishtakiwa kwa kosa la kumuua Janeth Romano (aliyekuwa mama wa watoto sita), Septemba 16,2020 katika Kijiji cha Lwega wilayani Tanganyika.
Ilielezwa kuwa Maliki alimtaka Janeth (marehemu) kimapenzi ila hawakuwa wameafikiana ambapo alimfuata nyumbani kwake kwa lengo la kufanya naye mapenzi lakini alikataa, hali iliyosababisha ugomvi baina yao.
Ilielezwa kuwa Anderson na Habona walipotokea walimsaidia Maliki kutekeleza azma hiyo ambapo alichana suruali ya mwanamke huyo, kisha Maliki akambaka na Anderson akachukua kanga na kumnyonga Janeth hadi kufa.
Awali wote watatu walipandishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka la mauaji bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu.
Ilielezwa mahakamani hapo tukio hilo lilitokea Septemba 16, 2020 katika Kijiji cha Lwega wilayani Tanganyika Mkoa wa Katavi, baada ya mwathirika wa tukio hilo na washtakiwa hao kunywa katika baa ya Theresia Romano (dada wa marehemu).
Kesi hiyo kwa mara ya kwanza ilipangwa kusikilizwa Aprili 24, 2024 ambapo awali walikuwa wameshtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.
Siku hiyo washtakiwa hao walikana kutenda kosa hilo na kupitia mawakili wao waliwasilisha ombi la kutenda kosa dogo la kuua bila kukusudia na upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi.
Baada ya kukiri kutenda kosa hilo la mauaji bila kukusudia walikutwa na hatia na kutiwa hatiani kwa kosa hilo.
Wakati wa kutenda kosa hilo Anderson alikuwa na umri wa miaka 37, Habona miaka 46 na Maliki miaka 17.
Katika kesi hiyo Jamhuri iliwakilishwa na Wakili, Octavian Mzee huku washtakiwa hao kila mmoja akiwakilishwa na wakili wake.
Wakili Mzee aliomba Mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa hao ili kuzuia vitendo vya kikatili katika jamii na kuwa kukatisha maisha ya binadamu ni kosa, ingawa alikiri washtakiwa walikuwa wamekunywa pombe.
Wakili huyo aliieleza Mahakama kuwa mwathirika wa tukio hilo (marehemu kwa sasa), baada ya kulewa aliamua kurudi nyumbani ila Maliki ambaye alikuwa amemtongoza na hawakuwa wameafikiana alimfuata na kumuomba wafanye mapenzi, ambapo alikataa.
Alieleza kuwa mwathirika alikuwa mama anayelea watoto sita ambao kwa sasa wameachwa yatima, watatu kati yao walikuwa wakisoma ila kwa sasa wameachwa bila uangalizi mzuri hivyo kuomba adhabu kali itolewe ili iwe fundisho kwa jamii.
Washtakiwa hao waliomba wapewe adhabu nafuu ambayo italingana na mazingira yaliyokuwepo wakati kosa lilipofanyika, wakosaji wa kwanza, wamekubali kutenda kosa ikiwa ni ishara ya kujutia walichokifanya na wamekaa rumande kwa muda wa miaka mitano.
Iliwasilishwa kuwa mshtakiwa wa kwanza na pili ni wanaume wenye familia, ambapo mshtakiwa wa kwanza alikuwa na mke na watoto wanne huku wa pili akiwa na mke na watoto wawili, hivyo kuomba kupunguziwa adhabu kwani wanategemewa na familia zao.
Kwa upande wake mshtakiwa wa tatu, ilielezwa kuwa alikuwa na umri wa miaka 17 wakati akitenda kosa hilo hivyo kuomba hilo lizingatiwe wakati wa kutoa uamuzi.
Jaji Mwenempazi amesema kwa kuzingatia kifungu cha 198 cha Kanuni ya Adhabu kinaelekeza kuwa mtu aliyetenda kosa la kuua bila kukusudia atawajibika kwa kifungo cha maisha jela.
Jaji amesema kwa kuzingatia mawasilisho ya pande zote ikiwemo upande wa utetezi, pia ni kanuni katika kutoa hukumu kwamba kukiri hatia katika hatua ya awali kabisa kunastahili sifa zaidi kuliko yule anayekiri hatia katika hatua za baadaye, na kunapaswa kupunguzwa kwa adhabu.
“Kwa hivyo, kiwango cha kupunguzwa kwa adhabu inategemea hatua ambayo mshtakiwa anakiri hatia, katika hatua ya kwanza inapendekezwa theluthi moja ya hukumu na katika hatua inayofuata robo ya kiwango cha juu,”amesema.
Jaji amesema katika shauri hilo anaona washtakiwa wanastahili kupunguzwa kwa kuzingatia ukweli ambao umetolewa, na pia hatua ya maombi yao na njia yakutenda kosa.
“Mshtakiwa wa kwanza na wa pili walipaswa kumwongoza mshtakiwa wa tatu ambaye alikuwa mtoto na kumzuia kutenda kosa hilo, badala ya kufanya hivyo walimsaidia kufanya kitendo kibaya zaidi na cha kinyama na kusababisha kifo cha mwathirika wa tukio hilo,”amesema.
Jaji Mwenempazi amehitimisha kwa kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela badala ya kifungo cha maisha, mshtakiwa wa kwanza na wa pili na kwa vile wamekaa mahabusu miaka mitano, wanapunguziwa na kubaki na kifungo cha miaka 15 jela.
Kuhusu mshtakiwa wa tatu (Maliki), Jaji huyo amesema chini ya masharti ya kifungu cha 4(a) cha sheria ya Sheria ya Mtoto namba 21/2009 inaelekeza kuwa mtu chini ya umri wa miaka 18 atajulikana kama mtoto.
Jaji amesema kifungu cha 4(b) cha sheria ya mtoto, kinaeleza kuwa, masilahi bora ya mtoto yatazingatiwa katika hatua zinazofanywa na taasisi za umma au za kibinafsi za ustawi wa jamii, mahakama au vyombo vya utawala.
“Kwa kuzingatia vifungu vya sheria vilivyotajwa hapa juu, ninatumia kifungu cha 119(1) cha Sheria kama Sheria ya Mtoto, kinaeleza kuwa mtoto hatahukumiwa kifungo kwa wazi, adhabu ya kifungo cha chini sio chaguo,”
Jaji ameongeza kuwa kwa kuongozwa na sheria hiyo, anaamuru kuachiliwa huru kwa mshtakiwa huyo wa tatu kwa masharti kuwa chini ya usimamizi wa baba yake mzazi kwa kipindi cha miaka miwili bila kutenda kosa lolote la jinai.
Masharti mengine ni itakuwa ni wajibu wa Ofisa ustawi wa jamii wa Wilaya ya Tanganyika kupata ripoti angalau robo mwaka katika mwaka ili kuhakikisha kuwa Maliki hajihusishi na kitendo chochote kilichokatazwa na sheria na akitenda kosa lolote ripoti itolewe mahakamani.