Wazazi chungeni watoto wasiwaharibie ndoa

Canada. Japo watoto ni neema katika ndoa, wana changamoto tena nyingi tu. Si watoto tu. Hata mafanikio yawe ya elimu na mali, vyote vina changamoto zake.

Katika kuzingatia na kulijua hili, leo, tutadurusu visa viwili vilivyowaletea changamoto na mtihani wanandoa karibia wakosane kutokana na kuharibika au kuharibikiwa kwa watoto wao.

Katika kisa cha kwanza binti alipachikwa mimba mtaani. Baada ya taarifa za kuwa na mimba kujulikana kwa wazazi, baba alianza kumtuhumu na kumlaumu mke.

Alishangaa ni kwanini binti alipata mimba bila mama kujua kana kwamba ndiye aliyempa hiyo mimba. Mume hakutaka kujipa muda wa kudurusu changamoto, mazingira, na wakati tuliomo.

Alichoona cha maana ni kukimbilia kumlaumu mama kana kwamba kuna mzazi anataka mwanawe aharibikiwe. Bila kufanya utafiti wa kina na kujiridhisha, japo kwa kumbana mtoto aeleze chanzo cha yote haya, baba alikimbilia kumlaumu mkewe kana kwamba alikuwa akiandamana na binti yao kila alipokwenda.

 Katika kadhia hii, baba alishindwa kujua kuwa binti yao alikuwa binadamu mwenye utashi, malengo, hata, wakati mwingine, ujanja kuliko wazazi wake.

Pia, baba alishindwa kujua kuwa kulaumu kusingeleta suluhisho la tatizo bali kuzalisha matatizo mengine na kupoteza fursa ya kumsaidia binti yao pia ndoa yao ukiachia kuzidi kumuumiza mkewe.

Wakiwa wamekwama kwenye kulaumu, mama aliamua kwenda kwa wazazi wake na kuwahusisha. Walimwita mkwe wao na mjukuu wao kutafuta namna ya kuwasaidia.

Kuna usemi kuwa aliyeko nje ya uwanja, anaona vizuri mpira unavyochezwa kwa sababu hayuko chini ya shinikizo la mechi.

Kwa kutumia busara na uzoefu wao, waligundua kuwa hapakuwa na kosa la mzazi yeyote bali tamaa na ujinga wa mjukuu wao.

Kwani, katika kumbana, mjukuu wao aliwaambia namna alivyoweza kuwaficha wazazi wake kwa kujionyesha alikuwa mtoto mwema, mwenye malengo makubwa, na aliyewasikiliza hadi wakamuamini kiasi cha kutomshuku kuwa alikuwa anajihusisha na mapenzi kabla ya ndoa.

Kufupisha kisa kirefu, baada ya wazazi kuhusisha busara na jicho la tatu, walipata suluhu wakaacha kulaumiana na kujikita katika kumsaidia binti yao. Kimsingi, waliridhika na kukubaliana kuwa hakukuwa na mwenye makosa wala mwenye kuharibu maisha yake zaidi ya binti yao.

Hivyo, walisimama pamoja kutafuta namna ya kumsaidia, kwani, maji yalikuwa yameishamwagika.

 Katika kisa cha pili, mtoto wa kiume aliyekuwa akisoma chuo, alirudi nyumbani na kukatisha masomo ghafla. Wazazi walishangaa sana na kujiuliza nini kilikuwa kimemsibu mtoto wao.

Badala ya kulaumiana, wazazi hawa walishirikiana kutafuta chanzo. Katika kudurusu na kutafuta jibu, waligundua kuwa kumbe mtoto wao alikuwa na uraibu wa kucheza kamari.

Hivyo, kila senti waliyomtumia, aliitumia kucheza kamari au kubet kama inavyojulikana akitegemea angetengeneza mamilioni ya fedha aachane na kuwaumiza wazazi wake kumgharimia.

Kimsingi, licha ya tamaa na ujinga, kijana alikuwa na lengo zuri ila alitaka kulitimiza kwa njia mbaya ya kubabaisha.

Hapa unabainishwa usemi kuwa unaweza kufanya jambo zuri kwa njia mbaya japo hatujui kama unaweza kufanya jambo baya kwa njia nzuri. Inawezekana.

Kwa wanaokumbuka kisa kilichotoka Kigamboni miaka ya nyuma, kuna jamaa alivunja nyumba na kuiba chakula akaacha fedha na runinga. Alipokamatwa, alikiri kutenda kosa na akaeleza kuwa sababu ilikuwa ni njaa.

Kwa kuangalia mazingira ya tukio na namna ‘mwizi’ yule alivyokuwa mwaminifu kwa kutoiba fedha na runinga, wenye nyumba walimhurumia na kumpa debe la unga, maharagwe, na sukari na kuachana naye.

 Je,  kama mzazi, yangekukuta ungechukua hatua gani katika visa vyote viwili hapo juu? Katika kuamua nini la kufanya, ungekimbilia kutafuta wa kulaumu au ungetuliza akili na kutafuta jawabu na suluhu ukiwa umetulia?

Hapa licha ya wahusika wawili, wazazi wana makosa au upungufu wowote? Tukiri. Yanaweza kuwapo makosa hata upungufu kama vile kumuamini mtoto kupita kiasi bila kuja uwezo wake wa kuyaangalia maisha ambalo ni jambo la kawaida.

Tunapaswa kufahamu kuwa watoto ni binadamu. Wana upungufu na ubora wao. La muhimu kuzingatia ni kwamba hawana uzoefu sawa na wazazi.

Mnaweza kuwapangia watoto mazuri wakaishia kuchukua mabaya na kugoma kusikiliza au kufanyia kazi mipango na ushauri wenu kwao.

Hili ni kawaida. Linatokea, wazazi mjipange kulitafutia suluhu badala ya kutafuta mchawi au kulaumiana bila sababu za msingi.