Kagera. Ahadi ya Serikali ya kufikisha umeme wa gridi ya Taifa katika wilaya zote za Mkoa wa Kagera imetekelezwa baada ya kusaini mikataba ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako, Ngara hadi Kyaka wilayani Misenyi.
Utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Benako cha msongo wa kilovoti 220/33, hatua inayotoa uhakika kwa mkoa huo sasa kupata umeme wa gridi badala ya kutegemea wa kutoka Uganda.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini kwa mikataba hiyo jijini Dodoma leo Jumatatu Agosti 25, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ni moja ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa na kiu ya kuona mradi huo unatekelezwa kama Serikali ilivyoahidi kwa wananchi wa Kagera.
” Kupitia mradi huu, Mkoa wa Kagera kwa mara ya kwanza unaingia kwenye gridi ya Taifa na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme hususan katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Misenyi, Karagwe, Kyerwa na maeneo mengine ya jirani, nawahakikishia watu wa Kagera kuwa Serikali imeshaamua mradi huu ufanyike kwa wakati na ndani ya miezi 24 tu,” amesema Dk Biteko
Amesema Kagera ambayo mahitaji yake ya umeme hayazidi megawati 47, baada ya muda itakuwa na uhakika mkubwa wa upatikanaji umeme kwa sababu kutakuwa na njia mbalimbali za kuufikisha mkoani humo ikiwamo Benako- Karagwe hadi Kayaka, Nyakanazi- Biharamulo hadi Muleba.
Naibu waziri mkuu huyo amesema tayari kuna mradi mwingine mkubwa unaotarajiwa kujengwa kutoka Ibadakuli hadi Mbarara Uganda wa kilovoti 400 na ule wa uzalishaji umeme wa Kakono wa megawati 87 ambao upo katika hatua za mwisho za kutafuta mkandarasi.
Amesema Serikali unaendelea pia na utekelezaji wa miradi mingine ya umeme katika maeneo mengine.
Amaitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na wa usafirishaji umeme wa kilovoti 400 wa Tanzania- Zambia, Chalinze Dodoma wa kilovoti 400 na wa Mkuranga – Pwani ambao utapeleka umeme kwa wananchi wa Kusini.
Mwingine ni ule utakaosafirisha umeme wa gridi imara wa Tunduru – Masasi – Mahumbika ambao pia unaenda kutoa uhakika wa umeme katika mikoa ya kusini.
“Utekelezaji wa miradi hii yote ya umeme ni kielelezo kuwa, Rais Samia ameshaonesha njia ya kuwafikishia wananchi umeme wa uhakika, sasa kinachohitajika kwa watendaji ni kukimbia badala ya kutembea kwani yanahitajika matokeo na siyo kusema sana,” amesisitiza Dk Biteko.

Amewashukuru wafadhili wa mradi waliotoa takriban Dola105.6 za Marekani alizowaagiza watendaji kuwa zitumike kwa usahihi ili kuwapa sababu wafadhili wengine kuendelea kusaidia miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa nchini.
Katika hatua nyingine, Dk Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuhakikisha wananchi 1,014 wanaopisha mradi wanalipwa fidia kuanzia Septemba, mwaka huu.
Amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na watendaji wa Tanesco kwa kuendelea kusimamia kwa umakini Sekta ya nishati.
Na ameomba wananchi mkoani Kagera kuchangamkia fursa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika baada ya miradi itakayofikisha umeme mkoani humo kukamilika.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa ameipongeza Serikali kwa kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuunganisha mkoa huo na gridi ya Taifa, akisema hatua hiyo ni uthibitisho wa namna inavyowajali wananchi kwa vitendo.
Mwassa amesema kwa sasa ni wilaya tatu pekee mkoani humo ndizo zimeunganishwa na gridi, hivyo kuanza utekelezaji wa mradi huo utawezesha wilaya zote kufikiwa na huduma ya umeme.
Amesema wananchi wa Kagera wataendelea kuwa watumiaji wazuri wa nishati hiyo na walipaji waaminifu wa bili ili shirika liendelee kupata mapato kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi
Felchesmi Mramba amesema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa minne ambayo haijaunganishwa na gridi ya Taifa, huku akiitaja mingine ni Rukwa, Lindi na Mtwara.
Mramba amesema tukio la kusainiwa kwa mikataba ya utekelezaji wa mradi huo ni la kihistoria, kwa sababu sasa mikoa yote ambayo haikuwa imeunganishwa na gridi, tayari ipo kwenye mpango wa kupelekewa umeme.
“Kwa sasa hakuna mkoa nchini ulio nje ya mpango wa kuunganishwa na gridi,” amesema Mhandisi Mramba.
Kwa mujibu wa Mramba, Kagera kwa sasa inapokea megawati 40 za umeme kutoka Uganda kupitia kituo cha Kyaka na megawati 7 kutoka kwa mwekezaji binafsi anayesimamia mradi wa Mirongo/Kikagati.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange alisema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba zimekuwa zikitegemea umeme unaotoka Uganda kwa muda mrefu kupitia kituo cha kupoza umeme cha Kyaka.
Amesema kituo hicho ncho hupokea umeme kutoka Masaka, Uganda, kwa njia ya msongo wa kilovoti 132 chini ya makubaliano baina ya Tanzania na Uganda.
Mramba amesema mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili ambazo ni M/s. TBEA Co. Ltd kutoka China, ambayo itajenga kituo cha kupoza umeme cha Benako na M/s. Transrail Lighting Limited kutoka India, ambayo itajenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Benako hadi Kyaka.