Moshi. Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao amefariki dunia leo Jumatatu, Agosti 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini (KCMC), Mjini Moshi.
Dk Shao amehudumu kama Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini kuanzia mwaka 2004 hadi 2014 alipostaafu na nafasi hiyo kuchukuliwa na Dk Fredrick Shoo ambaye anaishikilia mpaka sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Agosti 25, 2025 na Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Zebadiah Moshi imeeleza kuwa Askofu huyo mstaafu amefariki dunia asubuhi ya leo Jumatatu hospitalini hapo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uongozi wa Dayosisi kwa kushirikiana na familia ya marehemu wanaendelea na maandalizi ya mazishi ambapo taratibu zitatangazwa baada ya kukamilika.
Akizungumzia msiba huo, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Fredrick Shoo amesema watamkumbuka marehemu Shao kwa hekima na busara zake katika kipindi chake cha utumishi na hata alipostaafu.
“Ni kweli baba yetu amefariki leo, alikuwa baba mwenye hekima nyingi, busara na moyo wa utumishi, amefanya mengi, tutamkumbuka kwa mengi katika Dayosisi yetu,” amesema Dk Shoo.
Uongozi wa Dayosisi umetuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, waumini wa KKKT na wote walioguswa na msiba huo mkubwa.