Shinyanga. Mkazi wa kata ya Masekelo, Pendo Samson Methusela (37) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumkata kata na kiwembe sehemu mbalimbali za mwili wake, Timithoy Magesa (35) na kusababisha kifo chake.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital leo Agosti 25, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 23, 2025 saa 3 usiku katika nyumba ya wageni ya Bwashee iliyopo kata ya Ndala Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
“Kabla ya mauaji hayo, Pendo alipigiwa simu na mwanamke mwingine kwa kutumia simu ya marehemu, akimuonya aachane naye kwa madai kwamba ndiye anayempenda baada ya muda Timothy (marehemu), alimtafuta Pendo na kumtaka wakutane katika nyumba hiyo ya kulala wageni ili wazungumze,” amesema Magomi.
Ameongeza kuwa, “Hata hivyo, walipokutana walianza kugombana kuhusu mwanamke aliyempigia simu, hali iliyosababisha Pendo kutumia kiwembe alichokuwa nacho kumkata Timothy katika mkono wake wa kushoto pamoja na tumboni hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi.”
Magomi ameeleza kuwa, marehemu alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, huku akiainisha kuwa tukio hilo limetokea kutokana na wivu wa mapenzi.
Amesema taratibu za kisheria zitakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Mmoja wa majirani wa eneo hilo, Maria John ameeleza kuwa alipokuwa akitoka kanisani aliona watu wengi alipouliza akaambiwa kuwa kuna mtu amejeruhiwa lakini hakujua ni nani.
“Nilipokuwa natoka kanisani niliona watu wengi wamekusanyika, baada ya kuuliza nikaambiwa kuna mtu amekatwakatwa lakini huyo mtu mwenyewe simjui ni nani,” amesema Maria.
Aidha, Kamanda Magomi ametoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi na badala yake kutumia njia za amani kutafuta suluhu pindi wanapokumbwa na migogoro ya kimahusiano.