UTANGULIZI
Hebu fikiria kuwa wewe ni mpelelezi, unafika katika tukio la mauaji. Kuna mtu amenyongwa na mtu asiyefahamika. Unamkuta mtu ananing’inia kwenye kitanzi akiwa tayari ameshakufa lakini unakuta mtu mwenyewe aliyenyongwa siku hiyo, ndiye yule ambaye alishanyongwa hadi akafa miaka miwili iliyopita kwa hukumu ya mahakama kutokana na kosa la kuua!
Uchunguzi wa polisi unaonyesha kuwa mtu aliyegunduliwa amemnyonga mwenzake naye alishauawa kwa kunyongwa miaka miwili ilipita!
Bado kumbukumbu za polisi zinaonyesha kuwa aliyemnyonga mwenzake mara ya pili ndiye aliyenyongwa na mwenzake huyo huyo mara ya kwanza!
Watu wote hao walikuwa makaburini na walishasahauliwa lakini ghafla linatokea tukio hilo!
Nataka nikiri kuwa tangu nianze kazi ya upelelezi takribani miaka kumi iliyopita sikuwahi kukumbana na tukio la kustaajabisha kama hilo. Hapo hujui unapeleleza nini wakati watu hao wote wawili walishakuwa wafu!
Mimi ni mpelelezi Fadhil Bwanga na tukio linatokea katika jiji la Tanga.
Sasa hebu anza kufuatilia mkasa huu wa kusisimua. Naamini mpaka utakapoumaliza kijasho chembamba kitakutoka!
SASA ENDELEA…
KILIKUWA ni kipindi ambacho nilipata furaha lakini pia nilipata majonzi. Nilipata furaha kwa sababu nilipata cheo changu kipya cha uinspekta wa polisi nikiwa katika idara ya upelelezi wa makosa ya jinai. Kabla ya hapo nilikuwa Staff Sajin Meja.
Na nilipata majonzi kwa sababu siku hiyo hiyo niliyopata cheo ndio niliyomwagana na mchumba wangu Hamisa baada ya kunituhumu kuwa nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na polisi mmoja mwanamke aliyeitwa Helena ambaye alikuwa katika idara ya usalama barabarani.
Kabla ya siku ile niliyopata cheo changu msichana aliyenituhumu naye alinialika katika sherehe za harusi ya dada yake, nikaenda usiku bila kumuarifu mchumba wangu.
Baada ya sherehe kumaliza usiku wa manane ndipo Hamisa aliponipigia simu na kuanza kunishutumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Helena.
Alinitumia picha ya video kwa njia ya WhatsApp iliyoonesha nipo na Helena nikicheza naye kihasara hasara huku nikiwa nimelewa wakati tupo katika sherehe ya harusi ya dada yake.
Ilikuwa kweli kuwa nilicheza naye na kulikuwa na wakati Helena alinikumbatia. Vile ambavyo nilikuwa nimelewa na nilikuwa na uhakika kwamba Hamisa hakuwepo, sikujali kukumbatiana na msichana huyo.
Si hasha kwamba niliutomasa mwili wake kimahaba takriban muda wote niliokuwa naye. Lakini bila mimi kujua video ilikuwa inatuchukua!
Sasa kitu ambacho kilinishangaza ni kuwa Hamisa hakuwepo, je alikipataje kile kipande cha video alichonirushia?
Nilishuku kwamba pengine Hamisa alifika kwa siri mahali hapo kwa ajili ya kunichunguza au alirushiwa kipande hicho na mtu ambaye alikusudia kuuvunja uchumba wetu.
Sikuwa na kingine zaidi ya kumuomba msamaha Hamisa kwani picha aliyonirushia ilionyesha nilikuwa nikimtomasa tomasa kimahaba Helena bila kujielewa.
Mtu yeyote ambaye angeiona ile video angeshuku kuwa Helena alikuwa mpenzi wangu.
Niliamini kuwa ile video ilimuumiza Hamisa.
Kwa vile Hamisa alishanishutumu mara nyingi kuwa nina uhusiano wa kimapenzi na Helena, alilikataa ombi langu la msamaha na akaamua kuachia ngazi na kumpisha Helena.