USIKU ule nilirudi nyumbani nikiwa na fadhaa. Asubuhi yake ndio siku ambayo mkuu wangu wa kazi alinikabidhi cheo changu kipya kilichotoka makao ya polisi jijini Dar na kunivalisha tepe za uinspekta.
Akili yangu ilikuwa haipo pale, ilikuwa kwa Hamisa. Hata baada ya kupata cheo hicho sikuonekana kuwa mwenye furaha kamili.
Nilikabidhiwa ofisi mpya na majukumu mapya huku nikiwa na dukudu. Nilikuwa nimebakisha miezi mitatu tu nioane na Hamisa. Uchumba wetu ulikuwa umedumu kwa miezi sita.
Mara tu baada ya kukabidhiwa ofisi simu yangu ikaita.
Skrini ya simu ilinionyesha namba ya mkuu wangu wa kazi, yaani ofisa upelelezi wa mkoa.
Nikaipokea simu haraka.
“Ndiyo afande!”
“Umeshakabidhiwa ofisi?”Sauti ya ofisa upelelezi wa mkoa ikasikika kwenye simu.
“Ndiyo afande”
“Hebu njoo ofisini kwangu”
“Sawa, afande ninakuja”
Sikujua nilikuwa ninaitiwa nini. Nikatoka ofisini na kupanda ngazi kwenda ghorofa ya tatu ilikokuwa ofisi ya bosi wangu.
Nilipofika niliingia ofisini humo. Ofisa huyo akanikaribisha kwenye kiti.
“Keti tafadhali,” akaniambia kiungwana. Pengine ni baada ya kuona sasa nina cheo cha ukaguzi.
Nikakaa kwenye kiti.
“Kuna kiporo chochote cha kazi ulichokikuta katika ofisi uliyokabidhiwa?”
“Ndiyo nilikuwa napekua pekua mafaili afande”
“Sawa. Kama kuna viporo vyovyote utashughulika navyo baada ya kumaliza kazi hii nitakayokupa sasa.”
Ofisa upelelezi alipekua faili lililokuwa juu ya meza yake kisha akanitazama.
“Leo unakabidhiwa ofisi na leo unakutana na tukio ambalo litahusika na ofisi yako. Sijui utalichukuliaje, kwamba ni mwanzo mzuri au mbaya! Lakini vyovyote utakavyoona, fikia tamati kwamba kupanda cheo ni kuongezeka kwa majukumu. Unapofurahia cheo, furahia na majukumu yatakayokuwa mbele yako. Sawa Inspekta?”
“Sawa afande”
“Nimepokea taarifa sasa hivi kutoka kituo kikuu cha polisi kwamba kuna mtu aliyenyongwa katika mtaa wa shukuruni nyumba namba 222 eneo la Kisosora. Polisi wameshakwenda katika eneo la tukio. Kwa vile upelelezi huo utaangukia katika idara yetu, nataka ufike mapema katika eneo hilo kuanza upelelezi.”
“Umesema huyo mtu amenyongwa, hakuna maelezo zaidi?” nikamuuliza ofisa upelelezi huyo.
“Maelezo zaidi tunayategemea kutoka kwako ukifika huko”
“Sawa afande”
Dakika chache badaaye nililisimamisha gari la idara ya upelelezi nyuma ya gari la polisi, mbele ya nyumba namba 222 iliyokuwa mtaa wa Shukuruni eneo la Kisossora.
Nilikuta kundi kubwa la watu waliokuwa wamesimama ili kujionea kilichotokea.
Hapo nje hapakuwa na polisi hata mmoja. Baada ya kulizima moto gari hilo nilishuka na kuingia ndani ya nyumba hiyo, Ukumbini nilikuta watu wachache wakiwemo polisi wanne.
Watu hao walikuwa wakijadiliana huku wameuelekea mlango wa chumba cha pili cha mkono wa kushoto.
Wakati naingia nilimsikia mtu mmoja akiwaeleza wale polisi.
“Jana usiku walizungumza sana. Nafikiri walizungumza hadi saa sita usiku. Baada ya hapo nilipitiwa na usingizi. Sasa sikujua kilichotokea baada ya hapo. Leo asubuhi nilipombishia mlango kumjulisha kuwa leo ni zamu yake kununua Luku na umeme unakaribia kwisha, ndio tukakuta amenyongwa.”
“Na mlijuaje kuwa amenyongwa?” Mmoja wa polisi waliokuwa hapo ukumbini akamuuliza.
“Tulijua baada ya kuchungulia kwenye hiki kitundu cha kitasa cha mlango. Hata wewe ukichungulia utaona miguu yake inaning’inia.”
Polisi aliyekuwa akiuliza maswali akapeleka jicho lake moja kwenye kitundu hicho cha kitasa na kuchungulia.
“Ni kweli, miguu inaonekana inaning’inia,” akasema.
“Habari za kazi?” nikawasalimia ghafla.
Polisi na watu wengine waliokuwa wameshughulika na mazungumzo wakageza vichwa na kunitazama.
“Oh afande,” Polisi aliyekuwa akichungulia kwenye kitundu cha kitasa aliniambia kisha akasita na kunipigia saluti pamoja na polisi wenzake, kunipa heshima kama mkuu wao kabla ya polisi huyo kuendelea kunieleza.
“Ni vizuri umefika. Tulikuwa tunajadiliana jinsi ya kuingia humu chumbani. Kuna tatizo kidogo limejitokeza.”
“Tatizo gani?” nikamuuliza.
“Huu mlango umefungwa kwa ndani,” Polisi huyo aliendelea kuniambia huku akijaribu kuusukuma sukuma mlango huo kunionyesha kwamba haufunguki.
“Kama amejifungia una maana alijinyonga mwenyewe?”
“Hatujajua hadi sasa lakini kwa mujibu wa wakazi wenzake wa humu ndani ni kwamba alikuwa na mwenzake ambaye alikaa naye humu chumbani hadi saa sita usiku”
Na mimi nilisogea karibu na kuujaribu mlango huo.
“Ina maana huyo mwenzake aliyekuwa naye, pia yumo ndani au alishatoka?’ Nikawauliza.
“Hatujajua bado,”
“Huu mlango unavunjwa tu, hakuna njia nyingine,” nikawambia na kuupiga kikumbo kimoja tu, mlango ukafunguka.
Nikausukuma na kuruhusu macho ya watu wote waliokuwa hapo ukumbini kukimbilia kutazama ndani.
Tulimuona mtu aliyekuwa akining’inia kwenye kitanzi kilichofungwa kwenye mti mmoja wa dari lakini chumba chenyewe hakikuwa na gypsum board juu wala ceiling board. Juu kulikuwa wazi.
Ilikuwa kamba za nailoni iliyokuwa imechimba kwenye shingo ya mtu huyo aliyekuwa akining’inia bila uhai.
Sura yake ilikuwa inatisha. Akiwa na uso wenye ndevu ndefu pamoja na sharubu, macho yalikuwa yamemtoka na ulimi pia ulikuwa nje.
Alikuwa amevaa suti ya rangi nyeusi, shati jeupe na viatu vyeusi pamoja na soksi nyeupe.
Jinsi mwili huo ulivyokuwa ukining’inia unaweza kuhisi kuwa ulikuwa mwepesi usio na uzito wowote.
Baadhi ya watu waliouna mwili huo walishituka na kutaharuki lakini mimi sikushituka. Nilishazoea kuona maiti zinazotisha kuliko hiyo.
“Naona yuko peke yake,” nikasema na kuongeza.
“Hatuoni mwenzake yeyote humu chumbani”
“Labda alitoka usiku,” Yule mtu aliyekuwa akitoa maelezo alisema.
Chini ya ule mwili kulikuwa na meza iliyokuwa na chupa tupu kadhaa za bia, moja ikiwa imeachwa nusu. Pia kulikuwa na bilauri mbili.
Zile chupa tupu za bia pamoja na bilauri mbili vilionyesha kuwa kulikuwa na watu wawili waliokuwa wakinywa bia kabla ya tukio lile kutokea.
“Ndugu wewe ni mkazi wa humu ndani?” Nikamuuliza yule mtu aliyekuwa akitoa maelezo.
“Mimi ni mmoja wapangaji wa nyumba hii,” akaniambia.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Alphonce Kabendera.”
“Huyu marehemu naye ni mkazi nyumba hii?”
“Yeye ni mpangaji mwenzetu.”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa John Lazaro.”
“Ana mke na watoto?”
“Tangu aishi katika nyumba hii hatujamuona mke wake isipokuwa aliwahi kutuambia mke wake anafanya kazi Dar. Hapa alikuwa anakuja na wasichana tu mara moja moja.”
“Kwa hiyo alikuwa akiishi pake yake?”
“Ndiyo.”
“Huyo mtu ambaye umesema alikuwa naye jana usiku ni nani?”
“Hatumjui.”
Wakati nikizungumza na Alphonce, polisi mmoja alikuwa akishughulika kupiga picha. Aliupiga picha mwili wa marehemu kwa mielekeo tofauti.
Baada ya hapo mwili wa marehemu ulichomolewa kwenye kitanzi na kulazwa chini.
Midomo ya marehemu ilikuwa inanuka pombe hali iliyoashiria kuwa alikuwa amelewa wakati ananyongwa.
“Bila shaka alinyongwa akiwa amelewa,” nikawaambia polisi wenzangu.
“Inaonekana kuwa ni hivyo. Mwenyewe ananuka pombe,” Polisi mmoja akasema.
Tukalifungua fundo la kitanzi lililokuwa limekaba kwenye shingo ya marehemu. Tukaona karibu na fundo hilo paliambatanishwa na kipande cha karatasi nyeupe. Nilikichomoa kile kikaratasi na kukitazama. Nikaona kilikuwa na maandishi yaliyoandikwa kwa wino mwekundu ambayo yalisomeka. “BADO WATATU”. Chini ya maneno hayo palikuwa na saini pamoja na alama ya dole gumba.
Karatasi ile ilinishitua. Nilipata wazo kwamba maana ya maneno yale “Bado Watatu” ni kwamba kulikuwa na watu wengine watatu ambao wamepangiwa kuuawa kama alivyouawa mtu yule.
Pia nilihisi kwamba sahihi ile niliyoiona na alama ya dole gumba vilikuwa vya muuaji. Alikuwa ameamua kuweka sahihi yake pamoja na alama yake ya dole gumba.
Niliwaonyesha kile kipande cha karatasi polisi wengine ambao walisoma yale maneno na kushangaa.
Polisi wote walikubaliana na mimi kwamba maana ya yale maneno yaliyokuwa kwenye karatasi ni kwamba kuna watu wengine watatu ambao watauawa kama alivyouawa mtu yule.
Kadhalika ile sahihi na alama ya dole gumba, hapakuwa na shaka yoyote kwamba ni ya mtu aliyemuua Lazaro.
“Mimi nina shaka kwamba huyo mtu aliyekuwa naye usiku ndiye aliyemnyonga mwenzake,” Polisi mmoja akasema.
Mwingine akaongeza: “Na inaonekana haya mauaji ni ya kisasi kwa sababu muuaji ameorodhesha watu wengine watatu ambao hawajulikani”
Nilikubaliana naye. “Ni kweli koplo Hamisi. Ni lazima tumtafute huyu muuaji tuhakikishe tunamtia mikononi kabla ya kuua hawa watu wengine,” nikasema.
“Na pia ni vizuri tuwatambue mapema watu hao,” Polisi mwingine akachangia.
“Unaweza kuona ni jambo dogo tu lakini linaweza kutushughulisha sana,” Polisi mwingine akasema.
“Hili sio jambo dogo. Tukio lolote linalohusu mauaji ni kubwa hata kama mtu amejiua mwenyewe. Hapa panahitajika uchunguzi wa kina.”
Nikachutama na kuipekua mifuko ya marehemu. Nilikuta vitu kadhaa ikiwemo pochi iliyokuwa na pesa, simu, leseni ya udereva, kitambaa cha mkononi, funguo na vitu vingine. Niliwaonyesha wana usalama wenzangu kabla ya kuvihifadhi.
Nikavua saa aliyokuwa amevaa marehemu kisha nikawaambia wale polisi waubebe mwili wa marehemu wautoe nje na kuupakia kwenye gari la polisi.
Wakati polisi wanaubeba mwili huo na kuutoa nilimwambia yule mwenyeji wetu.