“SI nimekwambia nina mazungumzo na wewe!”
“Kumbe Fadhil hunijui. Nilikuheshimu pale ulipokuwa unaniheshimu. Kama unathubutu kuvunja heshima yangu mbele ya kirukanjia wako yule, nitakuvunjia heshima halafu utaniona mbaya. Mimi sitaki kufuatwa na wewe tena na sihitaji mazungumzo yako.”
Bahati njema hapakuwa na watu karibu. Kama wangekuwepo ningekuwa nimeumbuka kutokana na maneno makali niliyokuwa nikiambiwa.
Ilikuwa ni idhilali kwa inspekta mzima kudhalilika kiasi kile!
Niliifahamu nguvu ya mapenzi, ilikuwa kubwa kuliko uwezo wa yeyote. Ingemtikisa hata rais wa nchi, achilia mbali inspekta wa polisi kama mimi!
Hamisa baada ya kufunga mlango alichapuka kuelekea barabarani huku akilikwepa gari langu.
“Naweza kukupakia nikupeleke mara moja?” nikamwambia Hamisa.
“Kampakie Helena umpeleke mara moja, sio mimi?”
“Una maana suala la uchumba wetu unalichukuliaje?”
Hamisa alikuwa akitembea huku akisema lakini kwa vile alikuwa amenipa mgongo sikuweza kusikia alichokuwa anakizungumza.
Alifika katika kituo cha daladala kilichokuwa karibu na nyumba aliyokuwa anaishi, akasimama kusubiri daladala. Daladala nayo ilikuwa inakuja, ikasimama ubavuni mwake. Mlango ulikuwa umeshafunguliwa. Hamisa akaingia.
Nilikuwa nimeshafika kwenye gari nililokuwa nikilitumia nikafungua mlango na kujipakia. Kabla ya kufunga mlango wa gari nilitoa simu yangu na kumuandikia meseji Hamisa.
“KUMBUKA KUVUNJA UCHUMBA NI GHARAMA KUBWA!”
Baada ya kuituma ile meseji nilifunga mlango wa gari na kuliwasha.
Sikutarajia kuwa Hamisa angejibu meseji ile lakini aliijibu. Wakati naendesha gari hilo nilisikia mlio wa meseji iliyoingia kwenye simu yangu. Nikauondoa mkono wangu mmoja kwenye sukani na kuishika simu.
Niliifungua ile meseji na kuisoma.
Hamisa alikuwa amenijibu. Jibu lake lilikuwa; “KUMBUKA KUKOSA UAMINIFU KATIKA UCHUMBA NI GHARAMA KUBWA!”
Alikuwa amenizunguka kutokana na ujumbe niliokuwa nimemtumia. Vile nilivyomwambia kwamba akumbuke ni gharama kubwa kuvunja uchumba wetu. Yeye aliniigizia maneno akaniambia na mimi nikumbuke kukosa uaminifu katika uchumba ni gharama kubwa akiwa na maana kwamba kuvunjika kwa uchumba wetu kulitokana na kukosa kwangu uaminifu.
Nikaguna na kuirudisha simu yangu mahali nilipokuwa nimeiweka.
Maneno yake yakayarudisha mawazo yangu katika kile kilichotuletea tafrani katika uchumba wetu.
Ilikuwa ni kweli kwamba nilikuwa na uhusiano na Helena lakini uhusiano wetu haukudumu kwa muda mrefu ukavunjika baada ya mimi kuanzisha uhusiano na yeye Hamisa na hatimaye kuwa wachumba.
Lakini hata baada ya kuachana na Helena, ukaribu wetu mimi na Helena bado ulikuwqpo. Ulikuwqpo kwa sababu ya uhusiano wetu wa kikazi na pia kwa sababu tulikuwa tunafahamiana.
Mimi nilipokuwa na Hamisa, Helena akawa na bosi wetu mmoja ambaye alipata uhamisho kwenda Tabora.
Hamisa allikuwa hafahamu chochote kuhusu uhusiano wangu na Hellena, lakini Helena alikuwa anafahamu kuhusu uchumba wangu na Hamisa.
Siku ile ambayo Helena alinialika katika harusi ya dada yake tulialikwa maofisa wengi wa polisi, sikuwa peke yangu. Kwa sababu nilikunywa sana na Helena alikunywa sana tulionekana kama vile tumerudisha uhusiano. Nilicheza naye mara kadhaa, nilicheka naye mara nyingi na pia niliteta naye kwa muda mrefu.
Lakini baada ya sherehe hizo kumalizika Hamisa alinitumia video iliyoonesha nikicheza na Helena. Na akaniambia “kama umerudiana na mpenzi wako, mimi sikutaki tena!”
Nilishangaa. Nilishangaa kwa sababu nilivyokuwa nikijua mimi Hamisa hakuwa akijua kama nilikuwa na uhusiano na Helena na hakuwahi kuniuliza kuhusu hilo hata siku moja. Hivyo swali lake kwamba nimerudiana na mpenzi wangu wa zamani lilinishangaza sana.
Nikahisii kwamba kulikuwa na kidudu mtu aliyemwambia na ndiye aliyemrushia video ile ili kumuonyesha nilivyokuwa nikivinjari na Helena.
Ukitazama ile video na kuona jinsi nilivyokuwa nikimtomasa Helena na jinsi Helena alivyokuwa amelegea kama mnyoo begani kwangu, ilikuwa vigumu kujitetea mbele ya Hamisa kuwa Helena hakuwa mpenzi wangu.
Kutahamaki nikajikuta nimeshafika kituo kikuu cha polisi. Nililisimamisha gari nikashuka na kuingia ndani ya kituo hicho.
Nilikwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya kitengo cha uchukuaji wa alama za vidole.
Nikamkuta Sajin Meja Ibrahim amesimama kando ya meza yake akipiga picha kisu kilichokuwa juu ya meza yake.
“Oh Inspekta karibu!” akaniambia na kuongeza.
“Kazi yako nimeikamilisha.
Aliacha kazi aliyokuwa akiifanya akaenda kuketi kweye kiti. Na mimi nikakaa kwenye kiti cha wageni.
Alichakura nyaraka kutoka kwenye chano cha nyaraka kilichokuwa upande wa kushoto wa meza yake akatoa karatasi moja ambayo alikuwa ameiandika kwa mkono akaiweka juu ya meza.
“Katika zile bilauri na chupa, nimepata alama za vidole za watu wawili tofauti. Nimeziwekea alama A na B. Na katika ile karatasi yenye ujumbe ambayo ilikuwa na alama ya dole gumba nimepata alama tofauti, nimeiwekea alama C,” Sajin Meja Ibrahim alikuwa akinieleza huku akisoma kwenye ile karatasi aliyoiweka juu ya meza.
“Kwa maelezo yako ni kwamba alama ya dole gumba iliyoko kwenye karatasi ni tofauti na alama ulizozipata kwenye zile chupa na bilauri?” nikamuuliza.
“Ndiyo ni tofauti. Hapa nimepata alama za watu watatu tofauti na mojawapo nimegundua kuwa ni ya marehemu.”
“Alama ya marehemu umeigundua kutoka kwenye nini?”
“Kwenye baadhi ya zile chupa na bilauri moja”
“Uchunguzi huo umekuja tofauti na uchunguzi wangu wa awali.”
“Uchunguzi wako wa awali umeonyesha nini?”
“Uchunguzi wangu wa awali umeonyesha kwamba aliyekuwa akinywa bia na marehemu ndiye aliyeweka alama ya dole lake kwenye ile karatasi.”
Sajin Meja Ibrahim akatikisa kichwa.
“Uchunguzi wa hizi alama za vidole umetoa matokeo tofauti. Mwenye alama ya dole gumba ni mtu mwingine. Alama yake ni tofauti na zile nilizozikuta kwenye bilauri na chupa.”
“Kwa hiyo wahusika hapo ni watu watatu?”
“Ndiyo, hapa pana wahusika watatu.”
“Sasa huyo watatu atakuwa nani wakati maelezo tuliyopata yameonyesha kuwa kulikuwa na watu wawili!”
“Unatakiwa umtafute huyu mtu wa tatu.”
“Ukichunguza kwa akili tu utaona kwamba huyu aliyeweka dole lake ndiye muuaji. Vinginevyo hakuwa na sababu ya kweka dole lake na saini.”
“Huenda walikuwa watu watatu.”
Baada ya kuwa kimya kwa sekunde kadhaa huku nikiwaza, nilipata wazo jingine.
“Sasa sikiliza meja. Zifanyie utafiti hizi alama zote uone kama zinafanana na alama zilizoko kwenye kumbukumbu zetu za wahalifu halafu utanifahamisha.”
“Kazi hiyo itachukua muda kidogo kwa sababu alama zilizoko kwenye kumbukumbu zetu ni nyingi sana. Kuzipitia moja moja itachukua muda.”
“Si kitu hata kama itachukua muda.”
“Lengo langu ni kuwa kama tutagundua mmojawapo ni miongoni mwa wahalifu ambao waliwahi kukamatwa na polisi tutampata kirahisi.”
“Nimekuelewa. Nitajitahidi kuifanya hiyo kazi, nikifanikiwa kumgundua mmojawapo nitakujulisha.”
“Hivi vifaa viendelee kubaki huku?” Sajin Meja huyo akaniuliza.
“Hizi chupa na bilauri zake”
“Acha zikae huku huku mpaka nitakapokamilisha uchunguzi wangu.”
Nikamuaga Sajin Meja Ibrahim na kutoka ofisini mwake. Nilikuwa ninafanya kazi lakini akili yangu ilikuwa kwa Hamisa. Yale majibu aliyokuwa anayatoa kinywani mwake hasa ndio yaliyonikwaza.
Nilipoingia ofisini mwangu nikaanza kuyatafakari yale matokeo ya uchunguzi wa alama za vidole.
Kulikuwa na mambo yaliyonipa utata. Kwanza ni alama ya dole gumba kuwa tofauti na alama zilizokuwa kwenye chupa na bilauri. Na pili ni lile swali tulilokuwa tunajiuliza, huyu mtu wa tatu ni yupi wakati nilifahamishwa kuwa kulikuwa na watu wawili chumbani mwa marehemu?
Maswali mengine yaliyonijia akilini mwangu ni kama, je aliyeua siye aliyekuwa anakunywa na marehemu?
Na kama ni yeye, aliyesaini na kuweka alama ya dole gumba kwenye kile kikaratasi tulichokikuta kwenye kitanzi ni nani?
Maswali hayo hayakuwa na majibu kichwani mwangu. Nikahisi uchunguzi wa kina ulikuwa unahitajika.
Nikaitoa simu ya marehemu na kuanza kuipekua.
Kwanza niliangalia upande wa namba zilizosajiliwa pamoja na majina yake. Nikakuta orodha ndefu iliyonitia kichefu chefu.
Nilipoiacha ile orodha yenye majina ya wanawake na wanaume, nikaingia upande wa meseji.
Upande wa meseji zilizoingia nilikuta meseji tatu tu ambazo zilikuwa hazijafutwa na ambazo zilitumwa kwenye tarehe ya jana yake.
Meseji ya kwanza ilisema.
“Inabidi tuzungumzie nyumbani, tupate na bia mbili tatu.”
Na meseji ya tatu ilisema.
“Nitafika kwenye saa tatu hivi.”
Hizo meseji zilinigutusha. Nikaona akili yangu imepata msisimko.
Nikahisi kwamba aliyetuma meseji hizo atakuwa ndiye mtu ambaye alikunywa kilevi na marehemu na ambaye ndiye niliyekuwa nikimtuhumu kuwa alimnyonga marehemu. inaendelea…