“MUME wako anaitwa nani?”
“Anaitwa Omar Kikasha.”
“Hakuna mtu mwingine anayeishi katika nyumba hii anayetumia jina hili?”
Nilianza kutomuamini mwanamke huyo kwa kuhisi alikuwa anatuficha. Tabia ya binaadamu akishaona mtu anaulizwa na polisi hata kama hajui amefanya kosa au la, anamficha. Sijui ni kwanini?
“Mume wako yuko wapi?” nikamuuliza.
“Anafanya kazi wapi?”
“Mume wangu ni mfanyabiashara tu, ana ofisi yake barabara ya Mkwakwani.”
“Una picha yake ili tuweze kumuona?”
“Ninazo, si picha moja ziko nyingi.”
Nilidhani angerudi ndani akatuchukulie hiyo picha lakini alituambia.
Mkono mmoja alikuwa ameshika simu akaingia katika eneo la picha na kutuonyesha picha za mume wake.
Sikuhitaji hata kutoa picha iliyokuwa mfukoni mwangu ili nilinganishe. Mume wake alikuwa mtu tofauti. Wakati mtu tuliyekuwa tukimtafuta alikuwa kijana, aliye kwenye picha alikuwa mtu wa makamo kidogo kisha mnene na mwenye uso mpana tofauti na tuliyekuwa tunamtaka ambaye alikuwa na uso mwembamba.
Baada ya kuzitzama picha hizo nilimuuliza.
“Hii nyumbba ni mali ya nani?”
“Sisi tulipangisha tu.”
“Kama miezi tisa iliyopita.”
Usajili wa Thomas ulikuwa unaonyesha kuwa laini yake ilisajiliwa mwaka mmoja na nusu uliopita. Iliwezekana kwa wakati huo alikuwa akiishi hapo.
“Mwenye nyumba hii ni nani?”
“Mwenye nyumba hii ni mama mmoja, anaishi Iringa.”
“Bila shaka kulikuwa na wapangaji waliohama ndio mkaingia ninyi?”
“Inawezekana kwa sababu mwenyewe anaishi Iringa, hii nyumba inaishi na wapangaji tu.”
Nikajiambia kimoyomoyo huenda Thomas Christopher alikuwa mpangaji na alishahama.
Ili kupata uhakika zaidi nilitoa picha ya Thomas Christopher kutoka mfukonni mwangu na kumuonyesha msichana huyo.
“Hebu itazame hii picha,” nikamwambia huku nikimpa picha hiyo.
Wakati anaitazama nikamuuliza.
“Unaweza kumjua mtu huyo?”
Baada ya kumtazama kwa sekunde kadhaa, msichana huyo alitikisa kichwa.
“Simfahamu. Huyu ndiye unayemuulizia?”
“Hakai humu. Labda umuulizie kwenye nyumba nyingine.”
“Anuani yake inaonyesha alikuwa anakaa katika nyumba namba 313 na ndiyo hii kama sikosei.”
“Nyumba namba 313 ni hii, lakini mtu huyo hakai humu labda ni mpangaji aliyekuwa mwanzo kabla yetu.”
Nikaichukua ile picha na kumuaga msichana huyo kisha tukarudi kwenye gari.
“Umeamini maelezo yake?” Polisi niliyekuwa naye akaniuliza mara tu tulipojipakia kwenye gari.
“Nimemuamini. Sidhani kama alikuwa anatuficha kitu lakini bado tuko katika upelelezi, tunaweza kurudi tena.”
“Sasa tunakwenda wapi?”
“Twende kwa mwenyekiti wa mtaa huu.”
“Tutaijuaje nyumba anayoishi?”
“Hebu rudi kwa yule msichana akuelekeze iliko nyumba ya mwenyekiti.”
Polisi huyo akafungua mlango na kushuka.
Alikwenda kunako geti la nyumba hiyo na kubisha tena. Baada ya sekunde chache hivi mwanamke yule yule akafungua geti. Uso wake ulipokutana na uso wa yule polisi alionekana kuhamaki.
“Mmerudi tena?” akamuuliza kwa sauti ambayo ilionyesha wazi kuwa aliizuia isionyeshe hamaki yake.
“Tuna shida nyingine, ninakuomba utusaidie.”
“Niwasaidie nini?” Mwanamke aliuliza akiwa amekunja uso lakini akilazimisha tabasamu la uongo.
“Tunataka tumuone mwenyekiti wa mtaa huu ila nyumba yake hatuifahamu.”
“Mwenyekiti anakaa mtaa wa pili,” mwanamke akamjibu haraka na kuongeza; “Nyumba yake imepakwa rangi mpya ya bluu. Mbele ya nyumba kuna gari bovu lililowekwa juu ya matofali. Mkienda mtaigundua tu.”
Polisi akaondoka kwenye geti, lakini mwanamama hakulifunga geti haraka. Alibaki kwenye geti hilo akimtazama polisi huyo aliyekuwa akija kwemye gari. Alipomuona anajipakia na tunaondoka ndipo aliporudi ndani na kufunga geti.
“Amesema mwenyekiti anaishi mtaa wa pili,” Polisi huyo akaniambia.
“Nimemsikia. Amesema nyumba yake ni ya bluu…”
“Ndiyo. Na mbele ya nyumba kuna gari bovu lililowekwa juu ya matofali.”
Nililizungusha gari mtaa wa pili kisha nikalisimamisha na kuzitazama nyumba zilizokuwa mbele yetu.
“Nafikiri ni ile pale,” Polisi niliyekaa naye akaniambia huku akinionyesha nyumba ya tano iliyokuwa upande wetu wa kulia. Ilikuwa imepakwa rangi ya bluu na mbele yake kulikuwa na gari lililowekwa juu ya matofali.
“Ndiyo, itakuwa ni ile,” nikamwambia.
Nikaliendesha gari na kulisimamisha mbele ya nyumba hiyo. Wakati tunashuka kwenye gari hilo kulikuwa na mtu aliyetoka kwenye mlango wa nyumba hiyo.
“Habari ya leo?” nikamsalimia.
“Nzuri,” akanijibu huku akitutazama kwa macho ya tashiwishi.
“Mwenyekiti tumemkuta?”
“Mwenyekiti yumo ndani,” akatuambia.
Mtu huyo ambaye alionekana kuwa na hamsini zake, alirudi ndani. Mimi na polisi mwenzangu tukiwa tumesimama kando ya mlango tulimuona yule mtu akitoka na kutuambia.
Akaenda kando yetu na kusimama. Bila shaka alitaka kujua tutazungumza nini na mwenyekiti kwani sura za polisi zinakuwa tishio zinapofika popote.
Baada ya sekunde chache tu akatokea mwanamke. Tena msichana mwenye sura ya kupendeza.
Akatutazama kwa zamu kabla ya kutusalimia.
“Nzuri,” nilimjibu peke yangu.
“Ndio ninyi ambao mmeniita?”Akatuuliza.
“Wewe ndiye mwenyekiti wa mtaa huu?” Nikamuuliza.
“Ndiyo mimi. Mna shida gani?”
Nilitegemea mwenyekiti angekuwa mwanaume. Kumbe mwanamke tena kijana.
Nikajiambia pamoja na sifa nyingine zilizompa kura, uzuri wa sura yake pia ulichangia watu wampigie kura.
“Tuna shida ndogo tu,” nikamwambia huku nikimtolea picha ya Thomas Christopher.
Nilimuonyesha ile picha kisha nikamuuliza.
“Huyu mtu anaishi katika mtaa wako. Unamfahamu?”
Msichana alimtazama kwa makini kisha akatikisa kichwa.
“Huyu simfahamu na sidhani kama anaishi katika mtaa wangu.”
“Alisaini laini yake ya simu kwa kutumia barua ya mwenyekiti mwaka mmoja na nusu uliopita. Barua ilieleza kwamba anaishi nyumba namba 313 na ipo katika mtaa huu.”
“Ungekwenda kumuulizia katika nyumba hiyo.”
“Tumeshakwenda na tumeambiwa kama mtu huyo alikuwa anaishi hapo alishahama.”
“Inawezekana. Kama umesema alisajili laini yake ya simu kwa barua ya mwenyekiti mwaka mmoja na nusu uliopita, atakuwa ni mwenyekiti mwingine aliyepita ambaye nilimshinda katika uchaguzi wa juzi.”
“Sasa yuko wapi huyo mwenyekiti uliyemshinda.”
Msichana akatikisa kichwa.
“Sijui kwa sasa yuko wapi. Baada ya uchaguzi ule kwisha alihama mtaa kabisa. Sijawahi kumuona tena.”
Nikamtazama polisi niliyekwenda naye hapo kama vile nilikuwa ninamwambia, “Tumegonga mwamba!”
“Amefanya nini huyo mtu” Mwenyekiti akayarudisha macho yangu usoni kwake.
“Tunamtafuta kwa kosa la mauaji”
“Amemuua nani na wapi?”
“Bado tunaendelea na uchunguzi, siwezi kukueleza mengi. Asante na kwaheri.”
Nikageuka na kuelekea kwenye gari.
Nilifungua mlango nikajipakia. Polisi niliyekuwa naye alifungua mlango wa upande wa pili naye akajipakia. Nikaliwasha gari na kuondoka.
“Nilidhani tungempata kirahisi…?” nikamwambia polisi huyo wakati gari likiwa katika mwendo.
“Hata mimi nilidhania hivyo.”
“Maelezo tuliyoyapata yamenkatisha tamaa ya kumpata kwa haraka.”
“Kwa vile upelelezi bado unaendelea atafahamika tu.”
Kwa vile nilikuwa nimechukia kidogo sikujibu kitu. Nikaendelea kuendesha hadi kituo cha polisi. Fikiria unakusanya polisi na bunduki kwenda kumkamata mhalifu huku mkiamini kuwa mtamtia mbaroni halafu mnamkosa na kurudi kituoni bila matumaini mtampa wapi, inaudhi kiasi gani?
Mkuu wangu wa kazi wakati naanza sasa kazi ya upolisi, aliwahi kuniambia kadiri unavyohangaika kumtafuta mhalifu ndivyo dakika zake za kukamatwa zinavyokaribia.
Maneno hayo nilikuwa nayakumbuka kila nilinapokwama kumkamata mtu ninayemtafuta.
Niliyakumbuka maneno hayo kwa sababu yalikuwa yakinipa moyo na matumaini.
Nikiwa mbele ya kituo hicho, niliwashusha polisi wote kisha nikaondoka kuelekea Kisosora.
Mawazo ya kumkosa Thomas Christopher na mawazo ya kumkosa Hamisa yalinifanya niendeshe gari huku nimekunja uso.
Nilipofika Kisosora nilisimamisha gari nikashuka na kubisha katika ile nyumba. Kwa bahati njema mtu aliyetoka alikuwa Alphonce Kabendera, yule mkazi ambaye nilikuwa nikishirikiana naye tangu mwanzo nilipofika pale nyumbani.
“Oh Karibu sana,” akaniambia huku akinipa mkono.
“Asante. Habari ya leo?”
“Nzuri. Karibu ndani.”
Nikaingia ndani na yule mtu.
“Nikupe kiti au…?” Akaniuliza.
“Ndiyo lete kiti tukae.”
Hakukuwa na sebule. Kulikuwa na vyumba tu vya wapangaji.
Mtu huyo aliingia katika chumba cha mwisho cha mkono wa kulia. Baada ya sekunde chache alitoka akiwa ameshika kiti na stuli.
Aliniwekea kiti na yeye akaketi kwenye stuli. Inaendelea…