Nikakaa kwenye kiti na kumuuliza.
“Kuna taarifa yoyote ambayo mmeshaipata kuhusiana na mtu aliyefanya yale mauaji?”
“Bado hatujapata taarifa yoyote, tunawasikiliza ninyi polisi.”
“Kwa upande wetu tumemgundua muuaji….”
“Ni mtu anayeitwa Thomas Christopher. Sijui kama unamfahamu mtu huyo”
“Thomas Christopher?”
“Ndiyo Thomas Christopher.”
Alphonce akatikisa kichwa.
“Naamini kwamba ni mmoja wa marafiki wa marehemu na ndiye aliyekuwa naye usiku ule aliouawa.”
“Tulimgundua kutokana na upelelezi wetu na tuliambiwa alikuwa anaishi Chuda lakini tulipofika chuda tukaambiwa alishahama.”
“Umesema ni miongoni mwa marafiki zake?”
“Tunaamini hivyo kwa sababu waliwasiliana kwa simu juzi kabla ya kukutana hapa usiku na kuanza kunywa pombe.”
“Tatizo ni kwamba huyu mwenzetu maisha yake yalikuwa ni ya usiri sana. Akitoka asubuhi kurudi kwake ni usiku. Ilikuwa si rahisi kuwajua marafiki zake.”
“Una maana kwamba hata ndugu zake au jamaa zake pia hamwafahamu?”
“Kusema kwali hatuwafahamu.”
“Nilihitaji kuonana na mwenye nyumba hii. Nadhani yeye anaweza kutusaidia japokuwa kidogo.”
“Mwenye nyumba hakai hapa. Isipokuwa alifika jana na juzi kutokana na hili tukio la kuuawa kwa mpangaji wake.”
“Anaishi hapa hapa Kisosora lakini mtaa mwingine.”
“Unaweza kunipeleka anakoishi?”
“Tafadhali nipeleke nikaonane naye halafu nitakurudisha.”
Dakika chache baadaye Inspekta Fadhil na Alphonce wakawa kwenye gari la polisi wakienda mtaa aliokuwa akiishi mwenye nyumba huyo.
“Namba ya huyo mtuhumiwa nimeipata katika simu ya marehemu,” Fadhil alimwambia Alphonce wakati gari likiwa katika mwendo.
“Kumbe mliipekua simu yake.”
“Katika upelelezi unaweza kupekua kila kitu ili kupata kile unachokitaka. Baada ya kupata namba yake nilikwenda katika kampuni ya simu ambako ndiko nilikopata picha yake na anuani yake. Si unajua unaposajili laini ni lazima utoe maelezo yako.”
“Ungenionyesha. Pengine naweza kumfahamu.”
Fadhil aliitoa kutoka katika mfuko wake wa koti na kumpa Alphonce.
Alphonce aliitazama picha hiyo kisha akatikisa kichwa.
“Kwa kweli huyu sijawahi kumwona.”
Akamrudishia Fadhil picha hiyo.
“Yaani huyo mtu ndiye aliyemuua mpangaji mwenzetu. Sasa kama alikuwa rafiki yake walikosana nini?”
“Ndio kitu ambacho tunakitafuta. Na kuna watu watatu ambao wameandikishwa kuuawa. Tatizo ni kwamba hatuwajui ni kina nani”
Alphonce alishusha pumzi ndefu.
Dakika chache baadaye gari hilo likasimama mbele ya nyumba moja iliyopandwa miti ya vivuli mbele ya baraza.
Kulikuwa na mzee mmoja ambaye alikuwa amekaa barazani kwenye kiti cha uvivu akivuta mtemba.
“Mwenyewe ndiye huyo hapo aliyeketi barazani,” Alphonce alimwambia Inspekta Fadhil huku akifungua mlango wa gari.
“Ndiye huyu mzee anayevuta mtemba?”
Inspekta Fadhil naye alifungua mlango na kushuka.
“Mzee habari ya saa hizi?” Fadhil alimsalimia mzee huyo.
Mzee huyo aliuchomoa mtemba wake midomoni na kuwatazama wageni hao.
“Nzuri. Karibuni,” akawaambia.
“Shikamoo mzee Rajab,” Alphonce akamwamkia.
“Marahaba. Alphonce kulikoni?”
“Tumekuja kwako kutokana na lile tukio la kunyongwa kwa yule mtu kule nyumbani. Huyu mwenzangu ni ofisa wa polisi, alitaka kukuona ndio ikabidi nimlete hapa nyumbani.”
Mzee huyo akageuza uso wake na kumtazama Inspekta Fadhil.
“Karibuni ndani,” akasema huku akiinuka kwenye kiti alichokuwa amekaa.
“Karibuni” akawaambia tena na kutangulia kuingia ndani ya nyumba hiyo. Inspekta Fadhil na Alphonce wakamfuata nyuma.
Ndani ya sebule iliyokuwa imekaa shaghalabaghala ikiwa na fanicha za kizamani, Fadhil na Alphonce walikaribishwa kwenye makochi.
“Mzee wangu mimi naitwa Inspekta Fadhil. Ninafanya uchunguzi wa tukio la kunyongwa kwa mpangaji wako. Nimekuja kwako nikiwa na masuala machache ya kukuuliza,” Inspekta Fadhil alimwambia mzee huyo.
“Niulize tu, hakuna tatizo,” Mzee huyo akaniambia.
“Baada ya kulisikia tukio hili la kunyongwa kwa mpangaji wako ndani ya nyumba yako, unaweza kutueleza unafahamu nini kuhusu kunyongwa kwake au unafahamu nini kuhusu mtu aliyefanya kitendo hicho?”
“Kwanza hili tukio limenishitua na kunisikitisha sana. Nilipopata habari kwamba kuna mpangaji wangu aliyenyongwa usiku nilikwenda nyumbani lakini kwa bahati mbaya mwili wake ulikuwa umeshaondolewa na polisi.” Mzee alinyamaza kuvuta pumzi. Macho yake yalionyesha alikuwa na mengi ya kuniambia. Nikanyamza kumsikiliza.
“Yule mpangaji hana mke wala mtoto. Sasa baada ya kuambiwa kwamba mwili wake umechukuliwa na polisi nikawa ninasubiri. Kwa bahati njema wewe ndio umeletwa hapa kwangu,” Mzee akaendelea kuniambia.
“Ulikuwa unasubiri utueleze nini?”
“Tukio limetokea nyumbani kwangu, mimi ndiye mwenye nyumba. Nilijua ni lazima polisi wangekuja kunihoji.”
“Sasa unaweza kutueleza unafahamu nini kuhusu tukio lile?”
“Kwa kweli sifahamu chochote. Nimewauliza wapangaji wangu wanaoishi pale nyumbanni pia wameniambia hawafahamu chochote. Waliniambia usiku ule ambao marehemu alinyongwa alizungumza sana chumbani mwake akiwa na mwenzake ambaye kwa bahati mbaya hakuwa akifahamika.”
“Unawafahamu ndugu wa marehemu?”
“Kwa kweli siwafahamu.”
“Je, yeye mwenyewe ulikuwa unamfahamu vizuri?”
“Sikuwa nikimfahamu vizuri.”
“Umempangisha chumba mtu ambaye humfahamu vizuri?”
“Yeye aliletwa na mtu ambaye ninamfahamu. Na huyo mtu nilimfahamu kwa sababu alikuwa akijuana na rafiki yangu mmoja aliyekwishafariki. Alimleta kwangu kwa minajili ya kumpangisha katika nyumba yangu ile.”
“Umesema marehemu aliletwa na mtu ambaye unamfahamu, huyo mtu unayemfahamu ambaye ninahisi atakuwa anamjua vizuri marehemu, yuko wapi?”
“Ninataka nionane naye.”
“Anaishi barabara ya nne katika nyumba ya Msajili wa Majumba. Nitakuelekeza nyumba anayoishi…”
Mzee aliniambia ilikuwa nyumba ya ghorofa moja. Huyo mtu anaitwa Frank. Alikuwa anaishi upande wa ghorofani. Ukipanda ngazi, upande wake ni wa kulia.
“Asante. Nitakwenda kumuona.”
Nilipoondoka nyumbani kwa Mzee Rajab, nilimrudisha Alphonce nyumbani kwake kisha nikalielekeza gari barabara ya nne.
Nikiwa njiani nilisikia simu yangu ikiita. Nikaishika na kutazama namba ya mtu aliyekuwa ananipigia.
Nikaona namba ya Sajin Meja Ibrahim, mtaalamu wa polisi wa alama za vidole.
Nikaipokea. “Hello Sajin…!”
“Niko barabarani, naelekea barabara ya nne.”
“Una shughuli muhimu?”
“Niko katika uchunguzi wa lile tukio la kunyongwa kwa yule mtu.”
“Hebu njoo ofisini kwangu mara moja.”
“Kuna kitu kimenitatanisha…hebu njoo.”
Nilivyoisikia sauti ya Sajin Meja Ibrahim ilivyotaharuki niligeuza gari na kwenda kituo cha polisi cha Chumbageni.
Dakika chache baadaye nikalisimamisha gari mbele ya kituo cha polisi cha Chumbageni.
Nilishuka kwenye gari nikaingia kwenye kituo hicho na kwenda moja kwa moja hadi kwenye ofisi ya Saji Meja Ibrahim.
Nilipofungua mlango na kuingia, nilimuona Ibrahim amekaa kwenye kiti akisoma faili lililokuwa juu ya meza yake.
Sajin Meja aliponiona aliinuka kwenye kiti na kuniambia.
Nilifunga mlango nikaenda kunako meza yake, nikavuta kiti na kukaa.
Sajin Meja alipoona nimekaa na yeye akakaa.
“Afande kuna utata ambao umejitokeza hapa,” Sajin Meja Ibrahim aliniambia huku akinisukumia lile faili alilokuwa analisoma.
“Alama za vidole za huyu marehemu zinaonyesha kwamba alishakufa. Alihukumiwa kunyongwa na mahakama kuu mwaka jana. Sasa nashangaa kuona ameuawa tena. Faili lake ndilo hilo hapo.”
Kitu ambacho na mimi kilinishitua katika jalada la faili hilo kulipachikwa picha ambayo niliitambua kuwa ni ya yule mtu aliyenyongwa.
Ilikuwa picha ya ukubwa wa bahasha ambayo ilipigwa na polisi wakati marehemu akiwa hai. Hapo nimemaanisha kuwa marehemu alipigwa picha hiyo alipokuwa mtuhumiwa na ikawekwa katika faili lake.
Nyaraka za polisi zilizokuwemo katika faili hilo ambazo zilimhusu mtu huyo zilionyesha kwamba aliwahi kukamatwa na polisi miaka minne iliyopita kwa tuhuma za mauaji na kushitakiwa ambapo alipatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia na kuhukumiwa kunyongwa.
Kama kulikuwa na tofauti ni ya jina. Jina lililokuwamo katika faili hilo halikuwa la John Lazaro, lilikuwa Ramadhani Unyeke, lakini mtu alikuwa huyo huyo.
“Lakini majina ni tofauti,” nikamwambia Sajin Meja.
“Majina ni tofauti. Sisi tunaangalia kufanana kwa hizo alama. Wahalifu wanabadili majina kila uchao.”