Bidhaa bandia zinavyotafuna uchumi wa Tanzania

Dar es Salaam. Biashara ya bidhaa bandia inaendelea kuathiri uchumi wa Tanzania, huku takwimu zikionesha Serikali inapoteza zaidi ya Sh1.7 trilioni kila mwaka kutokana na ukwepaji wa kodi ya bidhaa kwenye sekta za pombe na sigara.

Tatizo hilo limekithiri zaidi katika maeneo ya mipakani kama Kigoma, Songwe, Katavi, Mbeya, Musoma mkoani Mara na Kagera, pamoja na miji mikubwa kama Dar es Salaam, Pwani, Mtwara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na wazalishaji wakubwa wa bia na sigara, bidhaa bandia zimeendelea kujaa sokoni kupitia mipaka isiyo rasmi, mitandao holela na udhaifu katika mifumo ya utekelezaji wa sheria.

Tatizo hilo lilijadiliwa kwa kina katika warsha ya wadau iliyoandaliwa na kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), ambapo washiriki walieleza kwa kina jinsi biashara haramu inavyozidi kushika kasi.

Wadau walirejea utafiti uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young mwaka 2019, uliobainisha pombe kutoka kwenye masoko haramu husababisha upotevu wa takriban Sh1.7 trilioni kwa Serikali kila mwaka, huku sigara bandia zikichangia upotevu wa karibu Sh20 bilioni kwa mwaka.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, amesema biashara haramu inaleta madhara makubwa, ikiwemo kupunguza mapato ya Serikali, kuhatarisha afya ya umma na kudhoofisha ushindani wa haki, ambao ni msingi wa ukuaji wa sekta ya viwanda.

“Biashara haramu, hasa ya sigara na pombe, inazidi kudhoofisha uchumi kwa sababu ya upotevu wa mapato ya kodi, huku ikiweka maisha ya wananchi hatarini kutokana na bidhaa bandia. Hali hii pia inavuruga bei za sokoni, kukatisha tamaa wawekezaji na kufungua mianya kwa uhalifu uliopangwa,” amesema Khadija.

Amesema Serikali imejipanga kukabiliana na biashara hiyo kwa kuimarisha vyombo vya sheria, kuwekeza katika teknolojia na kuhimiza ushirikiano mkubwa kati ya taasisi za umma na sekta binafsi.

Naye Ofisa Biashara Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Tajiri, akimwakilisha mkuu wa mkoa, amekiri jiji hilo ni kitovu cha uchumi wa Tanzania na ameahidi ushirikiano wa sekta mbalimbali kukomesha biashara ya bidhaa bandia.

“Vyombo vyetu vya usalama ni imara, lakini hili ni tatizo linalohitaji mshikamano. Warsha hii ni fursa ya kuweka mkakati madhubuti wa kulinda biashara halali na mapato ya Serikali,” amesema.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pia imeeleza hatua inazochukua kukabiliana na tatizo hilo, ambapo Meneja wa Mradi wa Stempu za Kielektroniki (ETS), Abyud Tweve, amesema TRA inatumia zana kama programu ya Hakiki Stamp na kifaa kipya cha ukaguzi kilichosambazwa nchi nzima. Pia teknolojia ya Akili Unde (AI) inatumiwa kubaini masoko hatarishi.

“AI inatusaidia kupima hatari, kuelekeza ukaguzi na kutambua wahalifu wa mara kwa mara. Tayari tumebaini walipa kodi wanaokwepa kodi na baadhi yao wana kesi mahakamani kwa kuhusika na biashara bandia,” amesema Tweve.

Kutoka sekta binafsi, viongozi wa viwanda wametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Mwakilishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Neema Mhondo, amesema warsha hiyo imekuja wakati muafaka ili kusaidia mapendekezo ya mabadiliko ya kisera.

“Biashara haramu ikiachwa bila kudhibitiwa, haitasababisha upotevu wa mapato ya Serikali, bali pia itadhoofisha uwekezaji, kuzuia ukuaji wa viwanda na kupunguza fedha kwa huduma muhimu kama elimu na afya,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCC, Roy Manalili, amefichua kiwango cha sigara bandia nchini kimeongezeka kutoka asilimia 2.9 mwaka 2023 hadi asilimia 4.1 mwaka 2025 na kusababisha upotevu wa takribani Sh20 bilioni za kodi.

Amesema wahalifu hutumia mipaka isiyo rasmi na masoko ya mijini yasiyo rasmi kuingiza bidhaa, mara nyingi wakisafirisha bidhaa kwa mafungu madogo au kuzificha ndani ya mizigo halali.

“Lazima tufunge mianya yote inayotumiwa na biashara haramu kuendesha magendo, usafirishaji haramu na uhalifu wa kimataifa. Hili si suala la kibiashara tu, bali pia ni suala la usalama wa Taifa,” amesema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBL, Michelle Kilpin, ameeleza hatari kwa afya ya umma, akibainisha zaidi ya nusu ya pombe inayotumiwa Tanzania hutoka kwenye vyanzo visivyodhibitiwa.

“Pombe haramu si tu inaiibia Serikali mapato ya kodi, bali pia inahatarisha maisha ya wananchi kutokana na ubora duni na njia hatarishi za utengenezaji. Tunahitaji udhibiti mkali na utekelezaji madhubuti wa sheria,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Serengeti Breweries, Obinna Anyalebechi, amesema wazalishaji waliwahi kutoa mapendekezo, ikiwemo kufanya utafiti huru kuhusu pombe haramu na kuongeza elimu kwa umma.

“Kama wazalishaji wenye kuwajibika, tumejitolea kutoa takwimu, kushiriki maarifa na kushirikiana na Serikali kwa njia ya kujenga ili kukabiliana na tatizo hili,” amesema.

Duniani kote, biashara haramu inakadiriwa kuingiza kati ya Dola trilioni 3 hadi 5 kila mwaka, ambapo sigara bandia zinachukua asilimia 15 ya matumizi ya kimataifa, huku pombe haramu ikiwakilisha karibu asilimia 26.

Biashara hizo zina athari kiuchumi na kijamii, hali ambayo sasa inaihusu Tanzania kwa kiwango kikubwa.