KOCHA wa timu ya taifa la Sudan, James Kwesi Appiah ambaye kesho, Jumanne ataongoza kikosi hicho kucheza mechi ya nusu fainali ya mashindano ya CHAN dhidi ya Madagascar, ameweka historia kwenye ramani ya soka la Afrika.
Wakati nchi hiyo ikiendelea kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha mamilioni kukimbia makazi yao, Appiah ameibadilisha Sudan kuwa moja ya timu tishio kwa sasa.
Vita vilivyopamba moto nchini Sudan tangu Aprili 2023 vimesababisha zaidi ya watu milioni 12 kuwa wakimbizi na ligi ya ndani kusitishwa, licha ya hali hiyo, Sudan imetinga nusu fainali ya CHAN na kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 nchini Morocco, wakizishinda timu kubwa ikiwemo Ghana nchi alikotoka Appiah.
Zaidi ya hapo, Sudan inafanya vizuri kwenye kundi lao la kufuzu Kombe la Dunia 2026, kundi linalowajumuisha vigogo wa soka Afrika kama Senegal na DR Congo. Kwa nchi inayocheza michezo yake ya nyumbani Libya au Sudan Kusini na wachezaji wake kuishi kama wakimbizi,haya ni mafanikio makubwa.
Licha ya historia hiyo, Appiah anaamini makubwa bado yanakuja.
“Ukishiriki kwenye mashindano, lengo lazima liwe ubingwa,” alisema kocha huyo.
Kuhusu hali inavyoendelea huko Sudan, Appiah alisema: “Mara nyingi tunapokea taarifa kuwa mchezaji amepoteza ndugu, huwaambia, ninyi ndio mnaoweza kuipa nchi matumaini. Wakati mwingine watu wanasema mapigano yanapungua kwa muda kutokana na furaha ya michezo.”
Akiwa mchezaji, Appiah alikuwa sehemu ya kikosi cha Ghana kilichotwaa Afcon 1982 nchini Libya. Akiwa kocha, aliweka historia mwaka 2014 kwa kuwa Mwafrika wa kwanza kuiongoza Ghana kwenye Kombe la Dunia nchini Brazil. Pia alikuwa msaidizi mwaka 2010 Ghana ilipofika robo fainali ya Kombe la Dunia, mafanikio makubwa zaidi kwa timu ya Afrika.