Hofu ongezeko gharama za kupanda ndege Tanzania

Dar es Salaam. Nauli za usafiri wa anga wa kimataifa huenda zikapanda kwa dola 45 (Sh111,250) kwa tiketi ya safari moja na dola 90 (Sh222,500) kwa safari ya kwenda na kurudi, endapo ada mpya itaanza kutumika kama ilivyopangwa.

Serikali imepanga kuanza kutoza ada ya uwezeshaji abiria (Passenger Facilitation Fee) kwa wasafiri wote wa kimataifa kuanzia Novemba 1, hatua ambayo inadaiwa kuimarisha usalama wa mipaka na kuboresha mifumo ya uchakataji abiria.

Hata hivyo, mashirika ya ndege na wataalamu wa sekta hiyo wanatahadharisha kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza gharama za tiketi na kuathiri ushindani wa Tanzania, kama kitovu cha safari za kimataifa katika ukanda wa Afrika.

Kwa mujibu wa mpango huo, wasafiri wa kimataifa watalipa dola 45 kwa safari ya moja kwa moja kuingia Tanzania na dola 90 kwa safari ya kwenda na kurudi. Watoto chini ya miaka miwili hawatalipa ada hiyo.

Ada hiyo itakusanywa wakati wa ununuzi wa tiketi na itaoneshwa tofauti kwenye tiketi husika. Hata hivyo ada hiyo itarejeshwa kwa tiketi ambazo hazitatumika.

Ingawa ada hiyo inalenga kufadhili mifumo mipya ya usalama na uhamiaji, mashirika ya ndege yanasema gharama hiyo itabebwa na abiria kupitia ongezeko la nauli.

Mashirika mawili yanayohudumu Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar yakizungumza na gazeti la The Citizen yamebainisha kuwa ada hiyo itajumuishwa kwenye mifumo ya tiketi.

Msemaji mmoja wa shirika la ndege alisema kuwa: “Kwa upande mmoja, hii inaongeza shinikizo la kuongeza nauli kwa mashirika ya ndege yanayojaribu kuuza safari za Tanzania. Wakati huohuo, inalifanya shirika lionekane ndilo linalopandisha nauli ilhali sisi tunalazimika tu kukusanya kodi kwa niaba ya Serikali.”

Msemaji wa Precision Air, Hillary Mremi, alisema tayari wamejulishwa kuhusu mabadiliko hayo na wanasubiri utekelezaji kuanzia Novemba mosi.

“Ndiyo, tunafahamu mabadiliko haya na tunajiandaa kuyatekeleza kulingana na maelekezo ya mamlaka,” alisema.

Shirikisho la mashirika ya ndege duniani (IATA) nalo limeonyesha wasiwasi wake kuhusu mzigo wa gharama hizo.

Makamu wa Rais wa IATA Kanda ya Afrika Mashariki na ya Kati, Kamil Al Awadhi, alisema ada hiyo inaweza kuongeza changamoto kwenye mazingira ambayo tayari ni magumu kwa mashirika ya ndege barani Afrika.

“Afrika tayari ina viwango vya juu vya kodi na ada kwa asilimia 12 hadi 15 zaidi ya wastani wa dunia. Kuongeza gharama zisizo na msingi kunawaongezea mzigo abiria na kudhoofisha nafasi ya usafiri wa anga kama chombo cha kuunganisha watu na uchumi, sambamba na kupunguza ushindani wa kivutio,” alisema.

Al Awadhi aliisihi Tanzania kushirikiana na wadau wa sekta ya anga na kulinganisha ada hiyo na kanuni za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) ili kuhakikisha usafiri wa anga unabaki nafuu na wenye manufaa kiuchumi.

Kwa nini ada hii imeletwa?

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), mapato yatakayotokana na ada hiyo yatatumika kufadhili mifumo mipya ya Advanced Passenger Information (API) na Electronic Border Control (eBMC).

Mifumo hii itawawezesha mamlaka kupata taarifa za abiria kabla ya kuondoka, kuwachunguza mapema na kuharakisha ukaguzi wa uhamiaji wanapowasili.

Tanzania, katika ukaguzi wa usalama wa ICAO mwaka 2023, ilipata alama ya asilimia 86.94 na kushika nafasi ya nne Afrika, lakini ikaonyeshwa mapungufu kwenye utekelezaji wa API na Passenger Name Record (PNR).

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi, Juni 16 mwaka huu  alisema mifumo hiyo mipya itaweka Tanzania sambamba na wajibu wa kimataifa na kuboresha huduma kwa abiria.

“Ada hii inalinda uendelevu wa muda mrefu wa mradi, ikihusisha gharama za uchakataji data, uboreshaji mifumo, ulinganifu wa kanuni, usalama wa mtandao na mafunzo,” alisema.

Mifumo hiyo itakamilishwa na huduma zingine kama e-visa, mifumo ya udhibiti wa uhamiaji iliyounganishwa na hifadhidata za kitaifa, na mifumo ya uchambuzi wa taarifa kwa madhumuni ya usalama.

Serikali inasema mageuzi haya si kwa ajili ya kufuata tu matakwa ya kimataifa bali pia kuimarisha usalama wa Taifa.

Kupitia ukusanyaji wa taarifa za abiria kabla ya safari, Tanzania itaweza kutathmini hatari na kuzuia ugaidi, uhalifu wa kimataifa na uhamiaji haramu.

Aidha, mifumo hiyo inatarajiwa kupunguza msongamano, kuongeza kasi ya huduma viwanjani na kuboresha uzoefu wa abiria.

Hata hivyo, gharama za utekelezaji na uendeshaji zitahitaji uwekezaji endelevu kwenye teknolojia na rasilimali watu, hali iliyoifanya Serikali kupitisha sehemu kubwa ya mzigo huu kwa abiria wa kimataifa badala ya kutegemea bajeti ya Taifa pekee.

Hatari kwa ukuaji wa sekta ya anga

Wataalamu wa sekta ya anga  wanasema ada hiyo inaweza kuathiri uchumi mpana zaidi, ikizingatiwa Tanzania inalenga kukuza sekta ya utalii na kuviimarisha viwanja vyake kama kitovu cha safari za kimataifa.

Mtaalamu wa usafiri wa anga, John Njawa, alionya kuwa sekta ya ndege ni nyeti kwa bei na ongezeko lolote la gharama huenda likawazuia abiria kutumia usafiri huo. “Kila ada ya ziada kwenye sekta ya ndege huwa inawaogopesha abiria, isipokuwa iwapo kituo cha safari kina vivutio vya kipekee vya kuvutia wageni,” alisema.

Watoa huduma za utalii pia wameonyesha wasiwasi kwamba ada hiyo inaweza kuongeza mzigo kwa watalii wa safari ndefu, ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za kupanda kwa gharama za mafuta na mabadiliko ya thamani ya sarafu duniani.

Changamoto kubwa kwa watunga sera itakuwa ni kutafuta uwiano kati ya kutimiza wajibu wa usalama wa kimataifa na kuhakikisha usafiri unabaki nafuu na wenye ushindani.