ILO yataka mkazo ajira zenye staha Tanzania

Dar es Salaam. Shirika la Kazi Duniani (ILO), limesema katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ni muhimu Tanzania iweke kipaumbele katika ajira zenye staha kwa kuwa ndiyo msingi wa amani na utulivu wa jamii.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo, Agosti 25, 2025 na Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla, katika mkutano wa tisa wa kamati ya utatu.

“Ajira yenye staha ni msingi wa amani, utulivu wa kijamii na maendeleo jumuishi. Bila kuhakikisha heshima, ulinzi na fursa, kwa kila mfanyakazi awe wa sekta rasmi au isiyo rasmi, hatuwezi kufanikisha maendeleo ya kweli,” amesema.

Amesema dira ya 2050 ya Tanzania si tu mpango wa kiuchumi bali ni mkataba wa kijamii unaolenga kuhakikisha ukuaji jumuishi, haki na fursa zinapanuliwa kwa wananchi wote.

Kwa mujibu wa Mugalla, vyama vya wafanyakazi vina jukumu la kuhakikisha sauti za makundi yote ya wafanyakazi zinasikilizwa na kutimiziwa mahitaji.

“Vyama lazima viendelee kutetea haki, pia viwe na ubunifu katika kusaidia wafanyakazi kukabiliana na changamoto za kidijitali, mabadiliko ya tabianchi na utandawazi,” amesema.

Kwa upande wa waajiri, amewataka waongoze kwa kuunganisha ushindani wa kibiashara na uwajibikaji wa kijamii,  kuwekeza katika mafunzo ya stadi kwa vijana, kuboresha mazingira salama kazini na kuunga mkono ajira zinazolinda mazingira huku zikiongeza tija.

Amesema taasisi za Serikali zina wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayoruhusu kuwepo kwa ajira zenye staha, huku mahakama na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) zitoe haki kwa wakati ili wananchi waamini mfumo wa haki za kazi.

Ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), kuimarisha usalama kazini, kwani hakuna anayepaswa kuhatarisha maisha yake ili apate kipato, huku taasisi za hifadhi ya jamii zikitakiwa kupanua wigo ili kuwafikia wa sekta isiyo rasmi.

“Sekta isiyo rasmi ndiyo chanzo kikuu cha kipato kwa Watanzania wengi, lakini wafanyakazi wake wanabaki bila ulinzi. Kurasimisha si suala la kufuata sheria pekee, ni suala la heshima, usawa na maendeleo ya Taifa,” amesema.

Amesisitiza vijana kupewa kipaumbele kwa kuwa ndilo kundi kubwa la Watanzania na msingi wa Taifa la kesho.

“Wakipewa stadi, fursa na msaada katika ubunifu, vijana hawawezi tu kubeba Taifa, bali kulisukuma mbele,” amesema.

Kuhusu watu wenye ulemavu, amesema wanapaswa kuonekana kama rasilimali na si mzigo wa kijamii, akiitaka Serikali, waajiri na jamii kuondoa vikwazo, kuandaa mazingira rafiki na kubadili mitazamo ili kufanikisha ushirikishwaji wa kweli.

Mugalla amesema tangu kuanzishwa kwake, ILO imejengwa katika msingi wa ushirikiano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi na kwamba falsafa hiyo ndiyo chachu ya kufanikisha maendeleo ya muda mrefu.

“Dira ya 2050 ni wito wa kuchukua hatua. Ni lazima tusimame kwa ujasiri na ubunifu kuhakikisha kila Mtanzania anaweza kuangalia kesho yake kwa heshima, usalama na matumaini,” amesema.

Ametoa rai kwa wadau kushirikiana, kusikilizana na kutafuta suluhu za pamoja kwa changamoto zinazokabili sekta ya ajira, akiahidi kuwa ILO itaendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha taasisi, kupanua hifadhi ya jamii na kuendeleza masoko ya ajira jumuishi.

Amesisitiza Tanzania ikitaka kufanikisha malengo yake ya 2050, itapaswa kuweka kipaumbele cha ajira zenye staha, ujumuishaji wa kijinsia, usalama kazini na kupunguza ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana.