Jela miaka 30 kwa kusafirisha gramu moja ya heroini na bangi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu Muharami Ahmed, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya heroini na bangi.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kusafirisha Heroini zenye uzito wa gramu 1.58 pamoja na bangi yenye uzito wa kilo 1.04, katika bandari ya Dar es Salaam, tukio alilolitenda Mei 6, 2024.

Mbali na kifungo hicho, Mahakama hiyo imetoa amri ya fedha taslimu Sh173,550 zilizokutwa kwa mshtakiwa, zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali, huku kiasi hicho cha dawa kipelekwe Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa ajili ya kuteketezwa.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Jumatatu Agosti 25, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini, wakati kesi ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Hakimu Mhini amesema Mahakama imemtia hatiani Ahmed kama alivyoshtakiwa.

“Upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka la mshtakiwa pasi na kuacha shaka kwa kuleta mashahidi tisa na vielelezo viwili” alisema Hakimu Mhini na kuongeza.

“Hivyo, kutokana na ushahidi huu, Mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa na kumuhukumu kwenda jela miaka 30 kwa kuzingatia uzito wa kosa lenyewe, na kwa lengo la  kutoa fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya Ahmed,” alisema Hakimu Mhini.

Hata hivyo, Mhini amesema haki ya kukata rufaa ipo wazi kwa mshtakiwa iwapo hajaridhika na uamuzi uliotolewa.


Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na wengine kwani dawa za kulevya zinasababisha athari kubwa kwa jamii, hususan vijana ambao ni tegemeo la Taifa la kesho.

Vile vile aliomba, begi lililobeba dawa za kulevya pamoja na fedha taslimu Sh173,550 zilizokutwa kwa mshtakiwa, zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Kwa upande wa dawa za kulevya alizokamatwa nazo mshtakiwa, Mwakamele aliomba Mahakama itoa amri ya kuzipeleka DCEA kwa ajili ya kuteketezwa.

Mahakama hiyo ilikubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kutoa amri kutaifisha mali hizo pamoja na kutekeleza dawa hizo.

Mahakama hiyo, ilipompa nafasi ya kujitetea mshtakiwa huyo,  aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ana mzazi ambaye ni mzee na watoto wadogo wanaomtegemea.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa mnao Mei 6, 2024 eneo la Bandari ya Dar es Salaam, sehemu ya mizigo, alikutwa alisafirisha dawa za kulevya kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar.

Mshtakiwa anadaiwa wakati anapita mashine ya ukaguzi (scana) katika eneo hilo, ofisa wa bandari alitilia shaka begi la mshtakiwa huyo na kuamuru likaguliwe.

Baada ya ukaguzi mshtakiwa alikutwa na pakiti ya unga mweupe na majani yaliyodhaniwa kuwa ni bangi pamoja na fedha taslimu kiasi cha Sh173,550 ndani ya begi alilokuwa anasafiria.

Hata hivyo, dawa hizi zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi ambapo ilithibitika kuwa begi hilo lilikuwa limebeba dawa za kulevya aina ya Heroini na bangi.