Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametoa maagizo sita kwa Wizara ya Elimu na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) yanayolenga kuongeza ufikiaji wa watu wazima wanaohitaji kusoma na kujiendeleza zaidi.
Majaliwa ametoa maagizo haya wakati ambao zaidi ya wasichana 13,000 waliokuwa wamekatisha masomo kwa sababu mbalimbali wamefanikiwa kurudi shuleni kupitia mpango unaoratibiwa na TEWW tangu ulipoanza rasmi.
Miongoni mwa maagizo aliyotoa Majaliwa ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya watu wazima, kukuza mafunzo ya amali na stadi za kazi, kutumia teknolojia katika utoaji elimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ushirikiano na wadau.
Ametoa maagizo hayo alipoongoza mamia ya washiriki katika ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW yaliyoanza leo, Agosti 25, 2025, jijini Dar es Salaam na yanayotarajiwa kukamilika Agosti 27.

Majaliwa amesema ni wakati sasa wa kuangalia namna ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya watu wazima, ikiwemo kuyafikia makundi yote nchini, hususan yaliyopo pembezoni yenye changamoto za kijamii na kijiografia.
“Tukifanikiwa kuwafikia huko walipo, tutakuwa tumepata mafanikio makubwa. Hilo liende sambamba na kukuza mafunzo ya amali na stadi za kazi kwa kufanya ufuatiliaji katika vyuo vinavyotoa taaluma hiyo vya umma na binafsi,” amesema Majaliwa.
Amesema anasisitiza ufuatiliaji wa elimu ya amali na stadi za kazi kwa sababu Serikali inataka elimu hiyo itolewe na kila mwenye nia ya kushiriki katika utoaji wa elimu, kwani wanataka Watanzania waweze kujiajiri, kujipatia kipato, kuajirika na kujenga uchumi unaotegemea maarifa anayopata kutoka katika mpango mkakati wa TEWW.
Pia ametaka kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia kwa kujenga na kukarabati vituo vyao, kwa kushirikisha taasisi zisizokuwa za Serikali kutafuta vifaa vya kisasa vya kujifunzia ili utoaji wa elimu na upatikanaji uwe rahisi zaidi.
Ameagiza pia TEWW kuendelea kubuni mifumo ya kisasa ya kidijitali, ikiwemo masomo kwa njia ya mtandao na mafunzo ili elimu ya watu wazima ibaki kuwa ya kisasa, jumuishi na yenye kutolewa kwa njia ya teknolojia kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa.
“TEWW, hakikisheni mnaendelea kufanya tafiti za mara kwa mara za uhitaji wa Watanzania kujua wanahitaji nini kuhusu elimu ya watu wazima ili waweze kubaini changamoto..
“Mpate mapendekezo ambayo yatawafikisha katika kutoa suluhisho. Pia nendeni kwa vijana wabunifu muone kuwa kazi zao ni mtaji kwao na mratibu bunifu hizo ili zilete manufaa kwao na wanaotumia ubunifu huo,” amesema.

Hayo ameagiza yaende sambamba na kuongeza ushirikiano kati ya wadau wa ndani na nje ya nchi, pamoja na taasisi zinazoendesha programu zinazoshabihiana na zile za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
“Ushirikiano huu ulenge katika kupata rasilimali watu, rasilimali mbalimbali na uzoefu wa teknolojia mpya ambayo itakwenda kuwezesha na kurahisisha utoaji wa elimu ya watu wazima, ili iendelee kuwa nguzo muhimu, tegemeo linaloijenga jamii ya Watanzania inayoweza kusoma, kuandika na kuhesabu na kutumia maarifa yake katika kukuza maendeleo binafsi au ya kitaifa,” amesema.
Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati ambao Mkuu wa TEWW, Profesa Philipo Sanga, amesema mbali na mafanikio waliyoyashuhudia kwa miaka 50, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo baadhi wanaangalia namna ya kuzitatua.
Amesema moja ya changamoto wanazokumbana nazo ni kutopata kwa wakati eneo la kujenga ofisi za taasisi hiyo jijini Dodoma baada ya eneo la awali kutwaliwa na Bunge.
“Hivyo, mpaka sasa bado tunatafuta eneo lingine jijini Dodoma ili tufungue ofisi hiyo. Pia tumekuwa na juhudi ya kufungua madarasa kila wakati, maeneo mbalimbali nchini yanakufa kutokana na kukosa usimamizi unaohitajika,” amesema.
Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema katika miaka 50 ya taasisi hiyo wanajivunia mambo mbalimbali yaliyofanyika sambamba na mchango wake katika kuboresha elimu.
“Tumekuwa tukiendesha tafiti mbalimbali ambazo zinasaidia kuboresha ubora wa elimu kwa makundi mbalimbali na hata kutoa mchango wetu katika maboresho yanapohitajika,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema katika siku tatu za maadhimisho hayo wamelenga kutathmini mafanikio na changamoto waliyoyashuhudia.
“Pia tutaweka mikakati ya utoaji wa elimu nje ya mfumo rasmi wa elimu,” amesema.