Majogoro aibuka mazoezi ya KMC, uongozi wafunguka

MUDA mfupi baada ya Mwanaspoti kuripoti kuwa aliyekuwa kiungo mkabaji wa Chippa United ya Afrika ya Kusini, Baraka Majogoro kuhitajiwa na KMC nyota huyo ameibukia mazoezi ya timu hiyo.

Majogoro kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na Chippa na tayari baadhi ya timu zimeonyesha nia ya kumhitaji ikiwemo KMC.

Timu hiyo ikiwa inaendelea kujifua kwenye Uwanja wao wa nyumbani chini ya kocha mpya Marcio Maximo, Majogoro alikaa jukwaani akishuhudia mazoezi na baadae kushuka kusalimiana na wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo.


Kiungo huyo, licha ya kuvaa nguo za kawaida na sio za mazoezi mkononi ameonekana akiwa ameshika jezi za timu hiyo ni wazianaweza akawa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu ujao.

Mwanaspoti lilifanya jitihada ya kuzungumza na Katibu Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula kufahamu kama wamekamilisha usajili wa nyota huyo aliyeonekana  akishuhudia mazoezi,  naye amesema Majogoro amekuja kufanya mazoezi kwa muda na timu hiyo baada ya kuomba.

“Hapana hatujamalizana naye, kaja kuomba kuanza kujifua pamoja na timu kwa muda baadae atajua anaitumikia timu gani,” amesema Mwakasungula na kuongeza;

“Hatuwezi kumzuia mchezaji yeyote akiomba kufanya mazoezi na timu yetu na tunatambua ni wengi wanatamani kufanya ivyo tunawakaribisha.” 


Kuhusu kupewa jezi, amesema ni sehemu ya kumuandaa atakapoanza mazoezi atatakiwa kuvaa jezi sawa na wachezaji wa timu hiyo, hawezi kuruhusiwa kuja na jezi tofauti na KMC.

Kabla ya kwenda Afrika Kusini, Majogoro aliwahi kuitumikia timu hiyo pamoja na kupita Mtibwa Sugar mbali na kuitumikia Taifa Stars.