Maofisa wa Takukuru wafundwa | Mwananchi

Kibaha. Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru ) imeanza mafunzo ya siku mbili kwa maofisa wake waajiriwa (307) kutoka mikoa yote nchini ili kuwaongezea weledi na utaalamu kuhusu manunuzi ya umma.

Mafunzo hayo yanafanyika wilayani Kibaha mkoani Pwani ambapo maofisa hao wanapitishwa na kuelezewa kuhusu manunuzi ya umma kupitia mfumo wa mtandao (NeST), mabadiliko ya sheria mbalimbali na maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.


Mada zingine ni uelewa wa kukusanya ushaihidi kwa njia ya kielektroniki na kuwasilisha mahakamani.

Akifungua mafunzo hayo leo Jumatatu Agosti 25, 2025 Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,  Crispian Chalamila, amewataka maofisa wanasheria wa taasisi hiyo kuhakikisha wanazingatia mada   zitakazotolewa na wawezeshaji ili kuongeza tija katika utendaji kazi.

“Ni lazima tuwe makini na kuhakikisha kazi zinafanyika kwa weledi ili kuleta tija kwa Taifa. Kesi zetu tuhakikishe zina ushahidi wa kutosha kabla ya kuzipeleka mahakamani ili Serikali isibebeshwe gharama kutokana na mapungufu ya kisheria,” amesema.

Awali, Mkurugenzi wa huduma za Sheria wa Takukuru makao makuu, George Balasa alisema mafunzo hayo ni hatua ya kujivunia, kwani ni miaka 14 imepita tangu yalipofanyika mara ya mwisho mwaka 2021.


“Sheria hubadilika mara kwa mara, hivyo ni muhimu wanasheria wetu kuendelea kujengewa uwezo. Uchaguzi mkuu unaleta changamoto nyingi za kisheria, na mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi yetu,” amesema Balasa.

Furahini Kibanga kutoka Mkoa wa Kilimanjaro amesema, “Mafunzo haya yamekuja kwa muda muafaka uchaguzi ni kipindi nyeti, na sisi kama wanasheria tunapaswa kuwa na uelewa mpana wa sheria mpya na namna ya kuzisimamia.”

Naye ofisa uchunguzi mkuu wa Takukuru  makao makuu, Biswaro Biswaro, amesema mafunzo hayo si ya kawaida mwani yatawapa ujuzi wa kushughulikia kesi zinazohusiana na rushwa na ukiukaji wa sheria wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.