Mastaa Pamba Jiji wamkosha Baraza, kujipima na Fountain Gate kesho

BAADA ya mazoezi ya wiki zaidi ya tatu, kikosi cha Pamba Jiji kesho Jumanne Agosti 26, 2025  kinatarajia kujipima nguvu dhidi ya Fountain Gate huku kocha Francis Baraza akiweka wazi kuwa anazingatia utimamu sio mabao ya kufunga au kufungwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza amesema maandalizi yanaenda vizuri na timu hiyo imefikia asilimia 80 ya ubora kwenye maeneo mengi hasa utimamu wa mwili.

Amesema amefurahishwa na uwezo wa wachezaji wake kujituma na kuonyesha kuwa na uhitaji wa kufunga na kuzuia kitu ambacho kinampa picha ya kujenga timu ya ushindani.

“Mechi hii ni kwa ajili ya kuangalia utimamu wa wachezaji baada ya mazoezi ya muda mrefu, ili kuwa na timu imara ni kufanya vitu kwa vitendo.

“Nafurahishwa na maendeleo ya wachezaji wangu tangu wiki ya kwanza ya maandalizi hadi hapa tulipo, naamini tutakuwa na kikosi kizuri chenye ushindani na wachezaji wangu wamefikia asilimia 80 ya utimamu wa mwili,” amesema.

Akizungumzia mchezo huo dhidi ya Fountain Gate, amesema anatarajia kuona nidhamu ya hali ya juu kwenye maeneo yote kuanzia ushambuliaji hadi wazuiaji lengo ni kufanyia kazi kile walichokifanya kwa kujiandaa na mashindano ya ligi.

Baraza amesema matarajio yake ni makubwa kuelekea msimu ujao ambao ameutaja utakuwa mgumu kutokana na sajili zinazofanywa na timu shiriki za Ligi Kuu Bara.