Dodoma. Serikali imesema, bila kuwekeza katika utafiti hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana kwenye sekta ya madini na Taifa halitafaidika nayo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Agosti 25, 2025 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini nchini ambalo linajengwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Jengo la Maabara hiyo litajengwa kwa siku 690 na litafungwa vifaa vyote muhimu vinavyopaswa kuwekwa kwenye uchunguzi huo, baada ya jengo lililokuwepo ambapo lilijengwa 1926 kutokuwa na mahitaji muhimu ya kisasa yanayotakiwa.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini nchini.
Mavunde amesema kutokana na hali hiyo, Serikali imeweka nguvu kubwa kwenye utafiti ili kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayechimba madini kwa kubahatisha badala yake kila mtu atafanya kazi hiyo kwenye eneo ambalo ana uhakika wa kupata madini.
Ameeleza maabara inayojengwa eneo la Kizota katika Jiji la Dodoma itakuwa suluhisho la kudumu la kumaliza changamoto hizo ambazo zimedumu kwa muda mrefu.
“Jengo tunalolitumia sasa lilijengwa karibu miaka 100 iliyopita, limechoka, halitufai kwa mahitaji ya sasa lakini haliwezi kufungwa zile nyenzo muhimu zinazohitajika ndiyo maana tunataka kuelekeza nguvu huku upande wa pili,” amesema Mavunde.
Pia amesema vifaa vitakavyofungwa ndani ya jengo hilo vitakuwa ni vya kisasa zaidi hivyo wakati ujenzi unaendelea, Serikali imeamua kuwa itawasomesha wataalamu ili wawe na ujuzi wa matumizi ya mashine kwa kuwa inataka kusiwe na ucheleweshaji wa mambo.
Katika hatua nyingine Mavunde ameagiza taarifa zinazopaswa kwenda kwa watu zitolewe mapema na kwa usahihi kwani haiwezekani kuwa na jengo kubwa na zuri la kwanza kwa utafiti wa madini Afrika Mashariki na Kati, halafu wachimbaji waendelee kupata taarifa zisizokuwa sahihi ama kupewa kwa kuchelewe.
Naye Mkurugenzi wa huduma za Maabara (GST), Notka Banteze amesema jengo hilo linalojengwa kwenye kiwanja cha ukubwa wa hekta mbili na nusu litatumika siyo kwa Watanzania pekee bali na wahitaji wa kutoka nje ya nchi.

Benteze amesema jengo la GST kwa sasa limechoka kutokana na kujengwa miaka mingi hivyo wamekuwa wakipata wakati mgumu katika kukamilisha mipango ya kuwahudumia Watanzania hasa katika sekta ya madini ambayo ndiyo msingi mkuu.
“Jengo tunalotumia kwa sasa lilijengwa karibu miaka 99 iliyopita, hakuna jipya tena mahali hapo ingawa wahudumu wameendelea kupambana kwa kutumia taaluma zao kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri, hapa tunazo hekta mbili na nusu na tutajenga jengo linalokwenda kutosheleza mahitaji yote muhimu ikiwemo ofisi za watumishi na kumbi za mikutano,” amesema Banteze.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Yahya Samamba amesema juhudi zinaendelea kufanyika ili kuifanya sekta ya madini iwe miongoni kwa taasisi zinazofanya vizuri zaidi kuliko sasa, huku akisisitiza kuwa kinachosubiriwa ni ukamilishaji wa jengo hilo lakini kwa upande wa vifaa na wataalamu wamejiandaa.