HATUA ya 12 bora ya mashindano ya Yamle Yamle Cup imeanza kuchezwa jana Jumapili Agosti 24, 2025 katika Uwanja wa Mao A uliopo Unguja kwa kuzikutanisha Al Qaida FC na Melinne City.
Katika mchezo huo ulioanza saa 10:00 jioni, Melinne City imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali kwa kuitandika Al Qaida mabao 3-2.
Fred Kiligo aliitangulizia bao Melinne City dakika ya 39 huku Said Pamba akiongeza mawili dakika ya 69 na 77. Al Qaida ikapata mawili ya kufutia machozi kupitia Ramadhan Kiramoto dakika ya 84 na Aboubakar Makame dakika ya 90.
Katika mchezo mwingine uliochezwa saa 12:30 jioni, Real Nine FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Melitano City wafungaji wakiwa ni Seif Salum na Ismaili Idrissa.
Mashindano hayo yataendelea leo jioni ambapo Mwembe Makumbi itavaana na Kajengwa majira ya saa 10 jioni huku Welezo City ikipambana na Miembeni FC saa 12:30 jioni.