Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa 2025, utakuwa na uwakilishi wa wanawake 34 wanaogombea ubunge majimboni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) huku katika mikoa 13 chama hicho kikiteuka wanaume pekee.
Ingawa idadi hiyo ya wanawake walioteuliwa na chama hicho kugombea ubunge majimboni imeongezeka ukilinganisha na ile ya mwaka 2020, wadau wanasema bado hatua iliyopigwa hairidhishi katika msingi wa uwiano wa wanawake na wanaume katika fursa.
Wadau hao wameeleza kuwa, kinachokwamisha mwamko wa wanawake, si uchumi na elimu kama ilivyowahi kuelezwa kabla, bali wamekosa uthubutu na kujawa woga wa mapambano katika uwanja wa kisiasa.
CCM ilitangaza uteuzi wa wagombea hao Agosti 23, 2025 katika majimbo 272 Tanzania Bara na Zanzibar, baada ya vikao vyake vya Kamati Kuu kisha Halmashauri Kuu vilivyoketi kwa siku mbili tofauti.
Katika majimbo 272, CCM imewateua wanawake 34 kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho, sawa na asilimia 12.5.
Hiyo ni sawa na uwiano wa kila wagombea wanane wa chama hicho, mwanamke ni mmoja pekee.
Idadi hiyo ni ongezeko la karibu asilimia tatu ya wanawake walioteuliwa na chama hicho kugombea ubunge wa majimbo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwa, waliteuliwa 25 kwenye majimbo 264 sawa na asilimia 9.4.
Wanawake hao walioteuliwa na CCM kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025, ni Mariam Kisangi katika Jimbo la Temeke, Bonnah Kamoli (Segerea), Kunti Majala (Chemba), Dk Ashatu Kijaji (Kondoa Vijijini), Mariam Ditopile (Kondoa Mjini) na Dk Ritta Kabati (Kilolo).
Pia, yumo Anna Lupembe (Nsimbo), Florence Samizi (Muhambwe), Profesa Joyce Ndalichako (Kasulu Mjini), Anne Malecela (Same Mashariki), Salma Kikwete (Mchinga), Asia Halamga (Hanang’), Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Esther Matiko (Tarime Mjini).
Wengine ni Mgore Kigera (Musoma Mjini), Mary Joseph (Serengeti), Dk Tulia Ackson (Uyole), Bahati Ndingo (Mbarali), Sarah Msafiri (Mvomero), Kellen Rwakatare (Mlimba), Amina Mussa (Kibiti), Subira Mgalu (Bagamoyo) na Judith Kapinga (Mbinga Vijijini).
Pia, yumo Sikudhani Chikambo (Tunduru Kaskazini), Jenista Mhagama (Peramiho), Lucy Mayenga (Kishapu), Jesca Kishoa (Iramba Mashariki), Condester Sichalwe (Momba), Hawa Mwaifunga (Tabora Mjini), Margaret Sitta (Urambo), Wanu Ameir (Makunduchi), Asha Kombo (Mfenesini) na Asma Mwinyi Jimbo la Welezo.
Aidha, Angellah Kairuki amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu na katika Bunge la 12 lililopita alikuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais na sasa amejitosa Jimbo la Kimbamba.
Kairuki aliongoza kura za maoni dhidi ya Issa Mtemvu aliyekuwa anataka kutetea nafasi hiyo.
CCM imempitisha Kairuki kupeperusha bendera ya chama hicho.
Hata hivyo, mwaka huu, wanawake wawili waliotia nia ya ubunge wa majimbo, waliongoza katika kura za maoni, lakini wakateuliwa wanaume badala yao ni Ummy Mwalimu (Tanga Mjini), badala yake ameteuliwa, Kassimu Mbaraka.
Katika Jimbo la Sikonge nako, aliongoza Munde Tambwe katika kura za maoni, lakini aliyeteuliwa kugombea ubunge wa jimbo hilo, ni Amosy Maganga.
Lakini, wapo wanawake wanne waliotia nia ya ubunge wa majimbo, hawakuongoza katika kura za maoni na vikao vya kitaifa vya chama hicho, vikawateua kugombea, vikiwaacha wanaume.
Wanawake hao ni Hawa Mwaifunga, aliyeshika nafasi ya tatu katika kura za maoni za CCM Tabora Mjini na akateuliwa. Aliyeongoza ni Shaaban Mrutu.
Vivyo hivyo, kwa Michael Kembaki aliyeongoza katika kura za maoni Tarime Mjini, lakini akateuliwa Esther Matiko huku Bunda Mjini akiteuliwa Ester Bulaya aliyeshika nafasi ya tatu lakini aliongoza Robert Maboto.
Mwingine ni Sikudhani Chikambo, ameteuliwa na CCM kugombea ubunge wa Tunduru Kaskazini, chama hicho kikimuacha Abdulkadir Issa aliyeongoza katika kura za maoni.
Ukiacha idadi hiyo ya walioteuliwa na CCM kugombea ubunge wa majimbo kwenye uchaguzi wa mwaka huu, mikoa 13 nchini wameteuliwa wagombea wanaume pekee.
Mikoa hiyo ni Arusha wanaume saba, Geita (tisa), Kagera (tisa), Mtwara (10), Mwanza (tisa), Njombe (sita), Rukwa (watano), Simiyu (wanane), Tanga (12), Kaskazini Pemba (tisa), Kaskazini Unguja (wanane), Kusini Pemba (tisa) na Mjini Magharibi (wanane).
Lakini, mikoa minne imeongoza kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagombea wa ubunge wanawake walioteuliwa na chama hicho tawala. Mikoa hiyo ni Mara wanawake wanne huku Dar es Salaam, Dodoma na Ruvuma watatu kila mmoja.
Katika orodha hiyo ya waliopewa ridhaa ya kuipeperusha bendera ya CCM kwa nafasi za ubunge, wapo waliokuwa wabunge wa viti maalumu waliovuka viunzi na kupenya kuwa wagombea wa majimbo, akiwamo Subira Mgalu (Bagamoyo) na Judith Kapinga (Mbinga Vijijini).
Wengine ni Mariam Kisangi (Temeke), Jesca Kishoa (Iramba Mashariki), Kunti Majala (Chemba), Hawa Mwaifunga (Tabora Mjini), Mariam Ditopile (Kondoa Mjini), Dk Ritta Kabati (Kilolo) na Wanu Hafidh Ameir (Makunduchi).
Aidha, Esther Matiko (Tarime Mjini) na Ester Bulaya wa Bunda Mjini.
Hata hivyo, Matiko na Bulaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wakiwa Chadema walishinda kwenye majimbo hayo. Mwaka 2020 walishindwa na walikwenda bungeni wakiwa viti maalumu.
Akizungumzia hilo leo Agosti 25, 2025, Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Tike Mwambipile amesema idadi ndogo ya walioteuliwa, imechochewa na uchache wa waliojitokeza.
Ameeleza imeshuhudiwa katika michakato ya ndani ya uchukuaji fomu ndani ya chama hicho, idadi ya wanawake walioonesha nia ya kuutaka ubunge wa majimbo ni ndogo ukilinganisha na wanaume.
“Kama wamejitokeza wachache na chama kinateua kwa kuangalia sifa na vigezo mbalimbali, ukiwachuja lazima watakaoteulia ni wachache kwa sababu walikuwa wachache tangu kwenye kujitokeza,” ameeleza.
Lawama ya wanawake wachache, Tike amesema imeshaondoka kwa vyama vya siasa na sasa wanaopaswa kulaumiwa ni wanawake wenyewe.
Amesema wanawake wameacha kuchangamkia fursa ya uchukuaji fomu za kugombea ubunge wa majimbo, wengi wamejikita katika nafasi za viti maalumu.
“Inaonekana bado wanawake tuna uoga wa kwenda kuchukua fomu,” amesema Tike.
Kwa sababu ya uhalisia huo, amesema inaonekana dhahiri kuna ombwe la uhamasishaji na uelimishaji wanawake kutoka kwa wadau wa jinsia.
“Sisi asasi za kiraia hii inatuonesha bado hatujafanikiwa kuifanya kazi yetu vizuri ya kuwahamasisha wanawake wajitokeze kwenye kugombea. Bado hatujafanya vizuri na kuna umuhimu wa kuendelea kuwapa motisha wanawake ili waone umuhimu wa kushika nafasi za majimbo,” amesema.
Amesema kwa sababu hakuna visingizio vya kiuchumi wala fursa kwa sababu zinatolewa, kilichobaki ni wanawake wenyewe kujitokeza kuchukua fomu na hatimaye kugombea.
Mhariri Mwandamizi wa Habari za Siasa na Jinsia wa Mwananchi, Lilian Timbuka amesema mwamko duni wa wanawake katika kuwania nafasi za kisiasa, unachochewa na hofu ya mbinu za kisiasa wakati wa michakato.
Amesema bado wanawake hawakuzoea kile alichokiita nginjanginja na ushindani katika uwanja wa siasa, hivyo wanapomwona mpinzani mwanamume wanajidharau.
“Wanawake siku hizi wana fedha zinazowawezesha kufika kila eneo kuomba kura, kinachowasumbua ni uwezo duni wa kukabiliana na nginjanginja za ushindani,” amesema Lilian ambaye pia ni mwanaharakati wa masuala ya jinsia.
Lilian ameongea suala la elimu na uchumi, sio visingizio tena kwa wanawake, bali umebaki uthubutu na kuamua kuingia ulingoni kupambania nafasi.
Ameeleza hilo ndilo jukumu lililobaki kwa wadau wa jinsia kuhakikisha wanawajengea wanawake ujasiri wa kuthubutu na hatimaye wawe sehemu ya uongozi unaofanya uamuzi kuhusu masilahi ya wengi.
Mwanasiasa mkongwe, Anna Abdallah amesema licha ya idadi ndogo ya waliojitokeza, angalau wameonesha uthubutu na wanastahili pongezi.
“Wanastahili pongezi, bado nchini kuna maeneo jamii haziamini katika mwanamke kuwa kiongozi, hivyo wanakumbana na vikwazo.
“Viongozi wa chama sio kwa CCM pekee bali vyama vyote viwahimize wanawake wagombee. Lazima wagombee,” amesema Anna ambaye pia ni mwenza wa Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa.
Amesema zamani kulikuwa na hali mbaya zaidi, kwa kuwa wanawake wengi waliogopa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, lakini sasa angalau.