MABOSI wa Tanzania Prisons wanaendelea kukisuka kimyakimya kikosi hicho kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao na kwa sasa inafanya mazungumzo na aliyekuwa kiungo mkabaji wa KCB ya Kenya, Mkenya Michael Mutinda.
Mutinda aliyezaliwa Desemba 27, 1995, ni miongoni mwa mapendekezo ya kocha mpya wa timu hiyo Mkenya mwenzake, Zedekiah ‘Zico’ Otieno, aliyetambulishwa kukiongoza kikosi hicho, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Amani Josiah aliyeondoka.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa uongozi wa timu hiyo, zinaeleza pia kiungo huyo amependekezwa na Zedekiah ambaye anamhitaji ili kuboresha eneo la katikati mwa kikosi hicho na kwa sasa mazungumzo hayo yanaendelea vizuri.
“Mazungumzo yanayoendelea kwa sasa ni kati ya mchezaji na uongozi wa Prisons kwa sababu ameshamaliza mkataba wake na KCB ya Kenya, jambo zuri ni ana uhusiano mzuri na kocha wetu hivyo, haitokuwa shida kupata saini yake,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya presha ya timu hiyo, mabosi wa kikosi hicho wameanza mapema kukisuka upya na licha tu ya mazungumzo hayo na Mutinda, ila tayari imeshakamilisha pia usajili wa aliyekuwa beki wa kati wa Dodoma Jiji, Mkongomani Heritier Lulihoshi.
Nyota wengine waliotua kikosini humo ni kiungo wa ukabaji, Masoud Abdallah ‘Cabaye’ aliyetokea KenGold ambayo imeshuka daraja, winga, Neva Kaboma (JKU) na washambuliaji, Emmanuel Mtumbuka (Mashujaa) na Lucas Sendama (Stand United).
Prisons ilimaliza nafasi ya 13 na pointi 31 msimu wa 2024-2025 katika Ligi Kuu Bara na kuepuka janga la kushuka daraja, baada ya kucheza ‘Play-Off’ dhidi ya Fountain Gate iliyokuwa ya 14 na pointi 29, kisha kuiondosha kwa jumla ya mabao 4-2.