Mmemsikia aliyeivuruga Stars kwa Mkapa

KIUNGO wa Morocco, Mohamed Rabie Hrimat ameweka wazi dhamira ya timu hiyo katika mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2024 ni kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu.

Mara baada ya kuizamisha Tanzania kwa bao 1-0 katika mechi ya robo fainali kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Hrimat alisema mechi hiyo haikuwa rahisi kutokana na nguvu ya wapinzani na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa nyumbani, lakini Morocco ilionyesha dhamira ya kufanikisha ndoto yao.

“Morocco ni nchi ya mpira wa miguu na tumepiga hatua kubwa. Tulijua tunapaswa kupambana kwa nguvu zote ili kulinda heshima ya taifa letu,” alisema nyota huyo wa FAR Rabat.

Hrimat, ambaye alicheza nafasi ya kiungo lakini mara kwa mara akisaidia katika kushambulia, alieleza mafanikio ya Morocco si ya mchezaji mmoja bali matokeo ya mshikamano wa kikosi kizima na mchango wa benchi la ufundi.

“Nawashukuru sana wachezaji wenzangu na benchi la ufundi. Tumefanya kazi kubwa na hii ni hatua moja tu. Lengo letu ni kushinda taji la CHAN 2024,” alisema.

Akizungumzia mchango wa kocha Tariq Sektioui, kiungo huyo alimsifu kwa maarifa na mbinu zake.

“Ukiwa na kocha bora kama Sektioui na wachezaji wenye vipaji, huwezi kutoka mikono mitupu. Amejenga timu yenye mshikamano na kiu ya mafanikio.”

Kwa mara ya pili, Hrimat alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa mechi dhidi ya Taifa Stars na kwa mara ya kwanza vijana wa Hemed Suleiman ‘Morocco’ walipoteza tuzo hiyo kwani walizibeba katika mechi zote za hatua ya makundi.