Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku sita kuanza kwa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka ‘mwendokasi’ barabara ya Mbagala, huenda nauli ya safari moja ikawa Sh1,000.
Taarifa ya kuanza kwa huduma ya usafiri huo Mbagala ilitolewa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia alipozungumza na The Citizen.
Tayari mabasi 99 kati ya 255 yatakayoanza kutoa huduma hiyo katika awamu ya kwanza, yameshawasili nchini na Dk Kihamia alisema kinachosubiriwa ni kukamilishwa kwa taratibu za kodi ili kuruhusu yaanze kufanya kazi.
Mwananchi leo, Jumatatu Agosti 25, 2025 imeelezwa na Dk Kihamia kuwa, masuala yote kuhusu taratibu za kuanza huduma za usafiri huo, iulizwe Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kwa kuwa imeshakabidhiwa mapendekezo siku nyingi.
Wakati Dk Kihamia akisema hivyo, chanzo cha kuaminika, kimesema imependekeza nauli iwe Sh1,000 kwa watu wazima na Sh200 kwa wanafunzi, ikiwa ni tofauti ya Sh250 inayotozwa katika mabasi hayo kwa barabara ya Kimara ambayo ni Sh750.
“Tumetoa mapendekezo nauli iwe Sh1,000 ili kuweza kutoa huduma bora na kukidhi gharama za kuyaendesha mabasi hayo ukizingatia kuna masuala ya ulipaji mishahara ya wafanyakazi, kuyatengeneza pale yatakapopata hitilafu na gharama nyingine zilizopo kwenye mradi huo,” kimesema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa Mofati, kampuni iliyopewa zabuni ya kuleta mabasi hayo, abiria watapanda wakiwa ndani ya kiyoyozi na hakuna atakayeruhusiwa kufungua kioo kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari.
Chanzo hicho kimesema matarajio ni kila baada ya dakika mbili hadi tatu kuwe na basi kituoni kwa ajili ya kubeba abiria na kuepuka changamoto za msongamano wa abiria vituoni.
Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Latra, Johansen Kahatano, amekiri kupokea mapendekezo hayo ya nauli ingawa hakuwa tayari kueleza kiwango pendekezwa.
Alipoulizwa ni lini hasa wataziweka wazi, Kahatano amesema bado wapo katika mchakato wa kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na kubainisha inaweza kuwa chini ya Sh1,000 au zaidi.
Ili kupitisha nauli ni lazima kuitishwe mkutano wa wadau kuzichambua. Alipoulizwa ni lini mkutano huo utaitishwa, Kahatano amesema watajitahidi kufanikisha hilo kabla mabasi hayo hayajaanza kazi.
Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema amesema bado hawajapewa taarifa hadi sasa kuhusu mkutano wa mapendekezo ya nauli hizo.
Lema amesema nauli hupangwa kutokana na umbali wa kilomita, anaamini nauli hiyo haitatofautiana zaidi na ile ya Kimara huku akionyesha wasiwasi, kwa muda uliobaki hadhani nauli mpya ambayo itatoa nafasi kwa watu pia kukata rufaa kuikataa kama hawataridhika nayo.
“Kiutaratibu nauli ikishatangazwa, kuna muda hutolewa kwa ambaye hajaridhika kukata rufaa, sasa tayari tumesikia mabasi hayo yataanza kutoa huduma Septemba mosi, sidhani kama muda utatosha kwa yote hayo, ninachokiona hapa huenda nauli ikatumika ileile ya Sh750 ili kuondoa hizo sintofahamu,” amesema Lema.
Mmoja wa wananchi wanaotumia barabara hiyo ya Mbagala, Maajabu Amri amesema ni vema suala la nauli wakazi wa maeneo hayo wakashirikishwa katika kutoa maoni kwa kuwa wao ndio watakuwa watumiaji.
Omar Kanje amesema kuna haja ya nauli hiyo ikaangaliwa kuwa ndogo zaidi ya inayotozwa sasa kwa njia ya Kimara, kutokana na hali za maisha za wakazi wa maeneo hayo.
Ujenzi wa barabara ya Mbagala yenye urefu wa kilomita 20.3 kutoka katikati ya jiji ulikamilika mwaka 2023, lakini utoaji wa huduma uliahirishwa mara kadhaa kutokana na kuchelewa kufikishwa kwa mabasi na kutokamilika miundombinu itakapopita mabasi hayo.
Hata hivyo, tangu mabasi hayo kuingizwa nchini, maandalizi yameonekana kupamba moto katika barabara hiyo ambapo wiki mbili zilizopita Mwananchi ilishuhudia vituo vya kupanda abiria vikiwa vinafanyiwa usafi, huku wakaguzi wakipita kukagua barabara zitakapopita mabasi hayo.
Agosti 13, 2025, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kukagua mabasi hayo yaliyopo bandarini na kutembelea ujenzi wa kituo maalumu cha kujazia gesi kwa ajili ya mabasi hayo, kinachojengwa Mbagala Rangi Tatu, aliagiza kukamilisha maeneo yaliyobaki kujengwa usiku na mchana ili mabasi hayo yaanze kutoa huduma ndani ya mwezi huu.
Agosti 20, wakati wa ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Kivukoni, Depo ya Mbagala na bandari akiwa na bodi ya wakurugenzi ya Dart, Dk Kihamia alisema mabasi 99 yanatarajiwa kukamilisha taratibu katika Bandari ya Dar es Salaam, huku waendeshaji wakikamilisha taratibu za kodi ili kuruhusu usambazaji wa haraka.
Pia, ameeleza kuwa matarajio yao Kampuni ya Lake Energies itakabidhi kituo cha kujazia gesi asilia (CNG) kwa Dart wiki ijayo kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho.
Aidha amebainisha hadi sasa kadi milioni moja za kielektroniki zimeagizwa kwa ajili ya abiria huku mageti ya kielektroniki ya tiketi yaliyoagizwa kutoka Uingereza na China yakitarajiwa kuwasili ndani ya mwezi huu na kusisitiza hata kama kutakuwa na ucheleweshaji wa vifaa vingine, huduma zitaanza kama ilivyopangwa:
“Changamoto pekee inayoweza kuchelewesha uzinduzi ni iwapo waendeshaji watashindwa kukamilisha taratibu za kupokea mabasi bandarini. Vinginevyo, tuko tayari,” amesema Mkurugenzi huyo
Awamu ya Pili ya BRT imepangwa kuendeshwa kwa kutumia jumla ya mabasi 755, ambayo yatawasili kwa awamu. Mbali na mabasi 99 yaliyopo bandarini sasa, mengine 51 yanatarajiwa kuwasili kati ya Agosti 25 na 27.