Pamba Jiji yamkomalia beki Azam FC

BAADA ya beki wa kati wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, Abdallah Kheri ‘Sebo’, kukitumikia kikosi cha Pamba Jiji kwa mkopo wa miezi sita msimu wa 2024-25, mabosi wa timu hiyo wanafanya mazungumzo ya kumsajili moja kwa moja.

Awali, uongozi wa Azam ulimtoa nyota huyo kwa mkopo kwenda Fountain Gate katika dirisha dogo la Januari 2025, ingawa aligoma na kutua Pamba Jiji, huku akiwa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na kikosi hicho cha matajiri wa Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Pamba zinaeleza mabosi wa kikosi hicho wanafanya mazungumzo na Azam ili kuipata saini yake moja kwa moja, kwa lengo la kumalizia mkataba wa mwaka mmoja uliobakia, kutokana na kiwango bora alichokionyesha.

“Tumeongeza mabeki wengine eneo la katikati lakini, Sebo tunahitaji kuendelea naye kwa sababu ni pendekezo pia la benchi letu la ufundi, mazungumzo yanaendelea na naamini yatafikia sehemu nzuri kwa pande zote,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha, alisema hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa juu ya suala hilo, ingawa uamuzi wa mwisho umebakia kwa benchi la ufundi endapo itamuhitaji pia asajiliwe.

Nyota huyo awali alihusishwa na kujiunga na Polokwane City ya Afrika ya Kusini, ingawa dili hilo lilikwama na sasa Pamba Jiji imeonyesha dhamira ya kumsajili moja kwa moja, kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara akiwa na Azam.

Sebo aliyechezea JKU, Zimamoto na Ndanda, anahitajika Pamba ili kuongeza nguvu, licha ya usajili wa mabeki, Abdulmajid Mangalo aliyetamba na Biashara United na Singida Fountain Gate na Mkenya Brian Eshihanda aliyetokea Kakamega Homeboyz.