Dar es Salaam. Askari wanne wa Kitengo cha Intelijensia cha Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakikabiliwa na shtaka la wizi wa pikipiki ya abiria maarufu bodaboda kwa kutumia silaha.
Maofisa hao wa Polisi, wanatuhumiwa kuiba pikipiki hiyo mali ya Ramadhani Singe katika kambi ya Polisi.
Kabla ya kupandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la wizi wa bodaboda hiyo, mali ya Ramadhani, askari Polisi sita mkoani Kilimanjaro walitiwa mbaroni kuhusiana na tukio la kutoweka kwa dereva bodaboda, Deogratius Shirima (35).
Askari waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa bodaboda ni Ramadhan Jumanne mwenye namba G.2478, Goodluck Richard F.7340, Zakayo Sanga G.654 na Victor Shelukindo, wote wakiwa na cheo cha Sajini.
Washtakiwa hao walisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Mkama.
Katika mfumo wa mahakama wa ufunguaji na usajili wa mashauri, kesi hiyo, iliyopewa usajili wa namba 20614/2025, ilifunguliwa Agosti 22, 2025.
Kwa mujibu wa sheria, shtaka hilo halina dhamana, hivyo washtakiwa wataendelea kuhifadhiwa mahabusu.
Kwa mujibu wa upande wa Jamhuri, kulingana na hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 22, 2025.
Wadaiwa, siku hiyo katika eneo la Police Line ndani ya Wilaya ya Moshi, wakiwa na silaha aina ya pingu, waliiba pikipiki yenye namba za usajili MC 406 ERU, aina ya Sinoray, mali ya Ramadhan Singe.
Kabla na baada ya kuiba pikipiki hiyo, watuhumiwa wanadaiwa walimtisha na kutumia pingu hizo kwa kumfunga Singe ili kujipatia pikipiki hiyo.
Kulingana na hati hiyo ya mashtaka ya VB iliyopo kwenye mfumo, wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, kinachohusu wizi wa kutumia silaha.
Kifungu hicho kinasema: mtu anayeiba kitu chochote, na kabla au baada ya kuiba anakuwa na silaha au chombo chochote cha hatari au cha kukera, na akakitumia kupata au kuhifadhi kitu hicho, anakuwa ametenda kosa la wizi wa kutumia silaha.
Endapo mtuhimiwa atatiwa hatiani, atawajibika kwa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 jela kwa kosa hilo la wizi, au pamoja na adhabu ya viboko. Kesi imeahirishwa hadi Septemba 3, 2025, itakapotajwa.
Bodaboda huyo, Shirima alitoweka Julai 21, 2025, lakini pikipiki aliyokuwa akiendesha ilidaiwa kubainika kuwa ilikuwa ndani ya nyumba ya mmoja wa washtakiwa hao askari, ndani ya kambi hiyo. Hata hivyo, mpaka sasa bodaboda huyo hajapatikana na hajulikani alipo.
Jumanne ya Agosti 5, 2025, Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, kwa simu, na alipoulizwa juu ya tukio hilo na ni askari wangapi wa Jeshi la Polisi wa mkoani kwake wanashikiliwa, alijibu: “Kama tulivyosema, uchunguzi unaendelea, viongozi wakubwa tupo nao hapa.”
Ingawa Kamanda Maigwa hakufafanua zaidi viongozi hao ni akina nani, taarifa za uhakika ambazo Mwananchi ilizipata zilibainisha kulikuwa na timu ya maofisa wa Polisi kutoka makao makuu Dodoma ikiongozwa na ofisa mwenye cheo cha Kamishna.
Baada ya kutoweka kwa bodaboda huyo, mmiliki wa pikipiki hiyo aliitafuta kupitia mfumo wa Global Positioning System (GPS) uliokuwa umefungwa katika pikipiki hiyo, ambao uliwaelekeza hadi nyumbani kwa polisi ndani ya kambi ya Polisi.
Singe, ambaye ni mmoja wa waendesha bodaboda mwenza na mwendesha bodaboda aliyetoweka, Shirima, aliachwa eneo hilo kuangalia kama lingekuwa na hatua yoyote ingechukuliwa na watuhumiwa kuhusiana na bodaboda hiyo.
Hata hivyo, bodaboda huyo, Singe alijikuta matatani baada ya polisi wawili kufika alipokuwa, ambao walimkamata, wakamfunga pingu na kumuondoa. Baadaye, pikipiki ya bodaboda aliyetoweka ikahamishwa kutoka ndani ya nyumba ya askari kambini hapo ilipokuwa.
Pikipiki hiyo, aliyokuwa akiendesha Shirima kabla ya kutoweka, ilikutwa imetelekezwa mtoni umbali wa kati ya kilometa tatu hadi saba.
Ndugu wa dereva bodaboda huyo wameendelea kupaza sauti wakitaka polisi aliyekutwa na pikipiki hiyo aeleze ukweli alipo ndugu yao, ambaye leo amefikisha siku 35 bila kupatikana wala kujulikana aliko.
Kwa mujibu wa mkewe, Mariam Abdi, siku mumewe alipotoweka, waliachana saa 11 jioni ambapo alimtaka ampigie baadaye ili ampe fedha kwa ajili ya chakula cha jioni. Hata hivyo, muda huo ulipofika, alipiga simu yake lakini haikupatikana.