Sababu simu kutumia sana bando bila kujua, fanya hivi kuzuia

Dar es Salaam. Inawezekana simu yako kwa upande wa intaneti ikawa inatumia data (bando) nyingi zaidi bila wewe kufahamu au kutarajia.

Baadhi ya watu wanaweza kulalamika wakijiunga vifurushi vinawahi kuisha pengine wasiweze kufahamu, zipo sababu zinazoweza kusababisha simu zao kutumia data nyingi kuliko.

Mwananchi kupitia vyanzo mbalimbali vya kurasa za kiteknolojia imekuletea sababu kuu za matumizi makubwa ya data kwenye simu yako.

Kwanza, Programu zinazojiendesha chinichini (Background App Activity) Programu nyingi huendelea kutumia data hata wakati huzitumii.

Hii hutokea kwa ajili ya kusawazisha (syncing) taarifa, kusasisha maudhui, na kuangalia arifa mpya (notifications).

Hii inaweza kujumuisha programu za mitandao ya kijamii, barua pepe, na za kuhifadhi data mtandaoni (cloud storage).

Usasishaji wa kiotomatiki (Automatic Updates), mfumo wa uendeshaji wa simu yako, pamoja na programu zake, unaweza kuwekwa ili kupakua na kusasisha kiotomatiki.

Ikiwa hii imewekwa kupitia data ya simu badala ya Wi-Fi, inaweza kumaliza haraka kifurushi chako cha data, hasa kwa sasisho kubwa.

Kuangalia video na kusikiliza muziki mtandaoni (Streaming Media), Kutazama video na kusikiliza muziki kwa ubora wa juu kunatumia sana data.  Pia Huduma kama vile Netflix, YouTube, Spotify, na Apple Music.

Kuangalia video kwa ubora wa hali ya juu. (High-Resolution Media). Ikumbukwe ubora wa picha na video kwenye mitandao ya kijamii na programu zingine umeongezeka kadri teknolojia mpya zinavyokuja.

Kutokana na maboresho hayo ya usasa unatumia data nyingi kuliko zamani. Vilevile, video zinazojicheza zenyewe kwenye mitandao ya kijamii huchangia matumizi hayo makubwa ya data.

Pia, huduma za eneo (Location Services), programu zinazotumia mara kwa mara GPS na huduma za eneo, kama vile programu za ramani (navigation) au za usafiri wa teksi mtandao zinaweza kutumia data nyingi.

Kucheza michezo mtandaoni (Online Gaming), michezo mingi ya simu, hasa ile inayohitaji intaneti moja kwa moja, inaweza kutumia kiasi kikubwa cha data.

Pia, kutumia VPN (Virtual Private Network) kunaweza kuongeza matumizi yako ya data kwa asilimia 15-20 kwa sababu ya usimbaji (encrypion) na usalama wa ziada inayoitoa.

Wi-Fi Assist/Ubadilishaji wa mtandao: Baadhi ya simu, kama vile iPhones zilizo na “Wi-Fi Assist,” hubadilika kiotomatiki kwenda kwenye data ya simu ikiwa muunganisho wako wa Wi-Fi ni dhaifu. Hii inaweza kukufanya utumie data bila kujua wakati ulidhani uliunganishwa na Wi-Fi.

Vilevile kupakua video na picha kiutomatiki (Auto-Download), pia sasisho la system (System Update), kuingia blogu zenye matangazo mengi.

Kwanza unapaswa utambue Programu zinazotumia data nyingi zaidi. Simu za Android na iOS zina kipengele cha kupima matumizi ya data kwenye settings yake.

Nenda kwenye mipangilio ya simu yako (settings) kisha utafute ‘Data Usage’ au ‘Cellular Data’ ili kuona orodha ya programu na kiasi cha data iliyotumika kwa kila moja.

Aidha, unaweza kuzuia matumizi ya data (Background Data) kupitia settings, chagua programu moja baada ya nyingine na uzime kipengele cha ‘Background Data’ au ‘Background App Refresh’. Hii itazuia programu hizo kupakua taarifa mpya bila wewe kuzitumia.

Unaweza kuzima sasisho za kiotomatiki za data ya simu kwa kwenda kwenye settings ya duka la programu (Google Play Store au Apple App Store) na hakikisha programu zinasasishwa tu wakati umeunganishwa kwenye Wi-Fi. Fanya vivyo hivyo kwa sasisho za mfumo wa uendeshaji wa simu yako.

Punguza ubora wa video na muziki kwa sababu huduma nyingi za kutazama video na kusikiliza muziki mtandaoni (kama YouTube, Netflix, na Spotify) hukupa chaguo la kupunguza ubora wa video au sauti. Badili ubora kuwa wa kawaida (standard) au wa chini (low) unapotumia data ya simu.

Zima video zinazojicheza zenyewe kwenye programu za mitandao ya kijamii kama Facebook au Instagram, video hucheza zenyewe nenda kwenye mipangilio ya programu hizo na uzime kipengele hiki ili video zicheze tu unapoziwasha wewe mwenyewe.

Pakua maudhui unapokuwa na Wi-Fi, Badala ya kutazama au kusikiliza mtandaoni, pakua muziki, filamu, au podikasti unazopenda wakati umeunganishwa na Wi-Fi salama. Hii itakuruhusu kufurahia maudhui hayo popote bila kutumia data.

Simu zenye Wi-Fi (Wi-Fi Assist) unapaswa kuzima kipengele hicho kwenye mipangilio ya simu yako ili kuzuia matumizi yasiyotegemewa.

Funga Programu usizozitumia, Ingawa simu za kisasa zina uwezo mzuri wa kusimamia programu zinazoendesha chinichini, ni vizuri kufunga programu ambazo huzitumii ili kuhakikisha hazitumii data bila wewe kujua.

Mwisho tumia kipengele cha kuokoa data (data saver) simu nyingi za kisasa zina kipengele hicho  au ‘low data mode’. Kuwasha kipengele hiki kunaweza kusaidia kupunguza matumizi ya data kwa ujumla kwenye programu mbalimbali.