SIMBA imefichua kuwa nahodha wake wa zamani, John Bocco ‘Adebayor’ amestaafu rasmi kucheza soka la ushindani na itamuaga katika siku ya kilele cha Tamasha la Simba Day, Septemba 10, 2025.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa wanamuaga Bocco kwa heshima kwa vile ni mchezaji aliyeifanyia makubwa klabu yao.
Amesema kuwa mbali na Bocco, mchezaji mwingine ambaye watatumia siku hiyo kumuaga ni Jonas Mkude ambaye bado anaendelea na soka la ushindani.
“Mwaka huu tutatumia siku ya Tamasha la Simba Day kuwaaga rasmi wachezaji wetu wawili wa zamani ambao wamefanya mambo makubwa katika klabu yetu.
“Mchezaji wa kwanza ambaye tutamualika na amethibitisha kushiriki na amefurahi sana. Ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu akiwa na Simba. Simba imepata nafasi ya kumuaga. Hapa namzungumzia nahodha John Bocco ‘Adebayor’.
“Mwingine ni mchezaji aliyeitumikia Simba kwa miaka 15. Aliyetuvumilia, tukamvumilia hadi mwaka juzi. Si mwingine ni nahodha wetu kutoka timu ya vijana hadi ya wakubwa. Si mwingine bali ni kipenzi chetu, Jonas Gerrard Mkude,” amesema Ahmed Ally.
Akizungumzia maendeleo ya kikosi chao, Ahmed Ally amesema kuwa kitarejea nchini, Agosti 28 na kabla ya hapo itacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa.
“Kikosi chetu kinatarajia kurejea tarehe 28. Tarehe 26 tunacheza na timu ya Wadi Degla inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri. Tarehe 27 tutacheza mechi na timu ya Fassell ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu ya Liberia.
“Baada ya hapo, tarehe 28 tutaanza safari ya kurejea nyumbani,” amesema Ahmed Ałły. Wiki ya Simba kuzinduliwa Mafinga
Ahmed Ally amesema kuwa wiki ya Tamasha la Simba Day itazinduliwa Mafinga Mjini, Agosti 31 mwaka huu.
“Awali tulipanga iwe Iringa Mjini lakini baada ya maoni na majadiliano tukaona tuhamishie Iringa. Nichukue fursa hii kuwaomba radhi Wanasimba wa Iringa Mjini. Niwaombe sasa Wanasimba wote wa Iringa na Wanasimba wote wa Nyanda za Juu tukutane Mafingakwa uzinduzi wa Wiki ya Simba.
“Uzinduzi ambao tutaufanya Mafinga haijawahi kutokea. Kwanza ni kwa wingi wa watu na pili kwa ukubwa wa tukio na tatu ni kwa shamrashamra ambazo zitafanyika,” amesema Ahmed Ałły.
Mtiririko wa matukio ya Wiki ya Simba
-Msafara kuelekea Hospital ya Mafinga kwa ajili ya huduma za kijami.
-Safari Kurejea Dar es Salaam
-Droo ya Bonanza la Matawi ya Simba
-Siku ya uzinduzi wa Matawi
-Siku ya Chakula cha Pamoja kwa Wanasimba
-Simba Kurudisha kwa Jamii
-Timu kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya Tamasha na Mazungumzo na Waandishi wa Habari
-Siku ya Tamasha la Simba