Shambulio hilo limefanywa na Jeshi la Israel (IDF) katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, kwa kutumia makombora na ndege zisizokuwa na rubani likilenga kituo cha mafuta na Ikulu.
Dodoma. Watu sita wameuwawa na wengine 86 kujeruhiwa kufuatia shambulizi la bomu lililofanywa na vikosi vya Israel mjini Sanaa nchini Yemen Jumapili ya Agosti 24, 2025.
Al Jazeera imeripoti kuwa Jeshi la Israel limeshambulia kwa mabomu na ndege zisizo na rubani mji mkuu wa Yemen Sanaa, ikilenga kituo cha mafuta, kituo cha kuzalisha umeme na Ikulu iliyopo katika kambi ya jeshi mjini humo.
Mashambulizi ya Israel yamekuja siku mbili baada ya Wahouthi kudai kurusha kombora dhidi ya Israel ikiwa ni sehemu ya mpango wa kundi hilo la nchini Yemen, wa kuishinikiza Israel kukomesha ukatili wake kwa Wapalestina walioko Gaza.
Ikumbukwe kuwa siku ya Ijumaa, Wahouthi walirusha kombora la hypersonic na ndege mbili zisizo na rubani huko Israeli, wakiapa kusimama na Wapalestina hadi uchokozi dhidi ya Gaza utakapokoma.
Ofisa kutoka Wizara ya ulinzi ya Houthi Abed al-Thawr, amedai kwamba vikosi vya Israel havijashambulia kambi za kijeshi peke yake kwani vililenga miundombinu na makazi ya raia wa taifa hilo.
“Huu ni uhalifu wa kivita unaolenga kuwaumiza Wayemen , na kukiuka haki za mamlaka ya Waarabu na sheria za kimataifa,” amesema Thawr.
Ofisa huyo ameongeza kuwa kikundi cha Houthi hakitasitisha mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya IDF ambavyo vimeendelea kuikalia Gaza kimabavu na kusababisha hali mbaya kwa maelfu ya Wapalestina.
Amesema mashambulizi hayo yalifanywa kujibu mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa Houthi dhidi ya taifa la Israel na raia wake, yakihusisha kurusha makombora ya uso kwa uso na ndege zisizo na rubani kuelekea Yemen, hivyo huo ni mwanzo wa uugwaji mkono wa Hamas kutoka kwao.
“Uchokozi wa Israel dhidi ya Yemen hautatukatisha tamaa kuendelea kuunga mkono Gaza, bila kujali kujitolea,” amesema.
Vikosi vya Hamas pia vililaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Yemen, na kueleza kuwa uchokozi wa kifashisti wa Israel unalenga kuizuia Yemen katika jitihada zake za kuwaunga mkono Wapalestina.
Hamas pia ilisifu msimamo wa Wahouthi, ikiuelezea kuwa ni ujasiri unaotakiwa kuungwa mkono na mataifa yote ya Kiarabu na vikosi vyote vilivyo huru, ili kuweka juhudi za pamoja kukomesha uvamizi huo.
Israel imekuwa ikishambulia kwa mabomu mitambo na bandari za Yemen kwa mwezi mmoja sasa. Lakini shambulio la Jumapili lilikuja muda mfupi baada ya jeshi la wanamaji la Israel kukishambulia kituo cha umeme.
Imeandikwa na Elidaima Mangela (UDOM) kwa msaada wa mashirika