SMZ yapokea gawio la Sh10 bilioni kutoka PBZ

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepokea gawio la Sh10 bilioni kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ikiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana kwa mwaka 2024.

Kutokana na kazi zilifanywa na benki hiyo kwa mwaka huo, imefanikiwa kutengeneza faida ya Sh107 bilioni ambapo gawio lililotolewa litaingizwa moja kwa moja katika mfuko wa Serikali.

Akizungumza katika hafla ya upokeaji gawio hilo leo Jumatatu Agosti 25, 2025 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema kutokana na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na benki hiyo ndio sababu iliyofanya kuongezeka kwa gawio.

Amesema, katika mwaka 2023 benki hiyo ilitoa gawio kwa Serikali la Sh7 bilioni pekee hivyo ongezeko hilo linathibitisha kuwa wanaendelea kuboresha utendaji kazi kwa lengo la kuongeza pato la Serikali.

“Gawio la Benki ya Watu wa Zanzibar limeongezeka kutoka Sh7 bilioni hadi kufikia Sh10 bilioni, nachukua fursa hii kuwapongeza kwa juhudi wanazoendelea kuzichukua na kuwa miongoni mwa benki 10 zinazofanya vizuri Tanzania,” amesema Dk Saada.

Katika kuhakikisha benki hiyo inabaki katika ubora wake, Dk Saada amesema inachukua hatua kutoa huduma bora kwa wananchi na kufungua matawi katika maeneo ya Tanzania Bara na kuimarisha huduma mtandao ili kuwarahisishia wateja wao.

Ameeleza, bado benki hiyo inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuboresha huduma kwa wateja, kuongeza mikopo kwa Serikali kuwekeza katika miundombinu ya kiuchumi na kuboresha mifumo ya utoaji wa fedha kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa faida.

Amefafanua kuwa, benki hiyo imekuwa kinara katika kutoa huduma kwa kufuata misingi ya sheria jambo ambalo limesababisha gawio hilo kuongezeka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Fahad Soud Hamid amesema benki hiyo imejipanga kujitanua zaidi katika maeneo mengine ikiwemo ndani na nje ya Tanzania.

Hivyo, amesema wanajiimarisha zaidi sehemu ya usalama wa mifumo kwa kuifanya isomane kwani eneo hilo linahitaji ulinzi wa kutosha.