TFS YAONGOZA TUZO YA USIMAMIZI BORA WA FEDHA 2025

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kung’ara kitaifa baada ya kutwaa Tuzo ya Usimamizi Bora wa Fedha kwa Taasisi zisizo za Kibiashara 2025, katika Mkutano wa Majadiliano wa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Serikali (CEOs Forum 2025) uliofanyika jijini Arusha.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa leo Agosti 24, 2025 na Makamu wa Rais, Dk. Philip Isdor Mpango, kwa niaba ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).

Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, tuzo hiyo ilipokelewa na Mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa TFS, Adv. Piensia Christopher Kiure, akiwa ameambatana na Naibu Kamishna Mwandamizi wa Fedha na Mhasibu Mkuu wa TFS, SACC Peter Mwakosya.

Katika hotuba yake, Mchechu alisema ushindani ulikuwa mkali kwani ulihusisha taasisi kadhaa zisizo za kibiashara ambazo zimefanya vizuri katika usimamizi wa fedha na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali.

“Kundi hili lilikuwa na mashirika matano bora: TIRA, BRELA, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), na TFS. NBS ilishika nafasi ya tatu, TTB nafasi ya pili, na TFS kuibuka mshindi wa kwanza,” alisema.

Alibainisha kuwa pamoja na taasisi kama BRELA kuingiza mapato makubwa, vigezo vya ushindi vilijikita zaidi kwenye uwajibikaji, utawala bora na ufanisi wa matumizi ya fedha.

Kwa upande wake, Adv. Piensia Kiure alisema ushindi huo ni matokeo ya nidhamu ya kifedha iliyojengwa tangu kuanzishwa kwa wakala huo mwaka 2011.

“Kwa miaka 14 sasa, TFS imekuwa ikipata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku mapato yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 10 kila mwaka. Tumeboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha, tukizingatia maelekezo ya bodi, wizara na uongozi wa taifa,” alisema.

Aliongeza kuwa TFS imejijengea heshima kimataifa kupitia ushirikiano na nchi kama Brazili na Urusi kubadilishana uzoefu wa sekta ya misitu, hatua inayoiweka taasisi hiyo kwenye viwango vya ubora wa kimataifa.

“Tuzo hii ni chachu kwetu kuendelea kuwaelimisha wananchi kufuata taratibu za serikali katika shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu. Ushirikiano wetu na wananchi umeendelea kuimarika, na tunatarajia mafanikio makubwa zaidi,” alisisitiza.

Mbali na ushindi huo, TFS pia imepokea tuzo nyingine ya utendaji mzuri iliyokabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kutokana na mchango wa TFS. Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Pindi Hazara Chana, huku ikikabidhiwa na Makamu wa Rais, Dk. Mpango.

Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali, ukiwa na ajenda kuu ya kuimarisha uwajibikaji na utawala bora katika sekta ya umma.