Arusha. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua mfumo mpya wa kielektroniki wa usimamizi wa maarifa (Knowledge Management System) unaolenga kuongeza uwazi na weledi katika ukusanyaji wa mapato.
Mfumo huo unatajwa kuongeza ufanisi, uwazi, kupunguza mianya ya rushwa kwa watendaji wasio waadilifu, kuongeza usawa ambapo hakutakuwa na mlipakodi atakayetolewa makadirio makubwa sana au atakayependelewa kwa kutoa makadirio ya chini.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 25, 2025 na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda wakati akizungumza jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa mfumo huo.
Uzinduzi huo umeshuhudiwa na watendaji mbalimbali wa mamlaka hiyo wakiwemo makamishna wa idara za kodi, wakurugenzi wa idara saidizi, manaibu kamishna na wakurugenzi wa idara na mameneja wa mikoa.
Mwenda amesema kuwa mfumo huo umezinduliwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa Mamlaka hiyo ihakikishe inatenda haki kwa walipakodi kwa kutowawekea makadirio makubwa au madogo.
“Moja ya maagizo ya Rais ni kuhakikisha tunatenda haki kwa walipakodi, kwa kutowatolea makadirio makubwa au madogo kuliko wanayostahili, moja ya vitu vinavyoweza kusababisha kutotenda haki ni pamoja na kutokuwa na maarifa yaliyo sawa,” amesema.
Amesema mfumo huo utaongeza maarifa kwa watendaji wa TRA, kuimarisha usawa na kuondoa mianya ya rushwa.
“Mtumishi wa TRA akiwa Mbeya atafanya hicho anachotakiwa kufanya au sehemu yoyote, hakutakuwa na mianya kwa wachache itakayosababisha mazungumzo na rushwa.
“Hakutakuwa na mianya ya wale wanaoweza kuomba wapendelewe, huu mfumo ni muhimu na wote tuhakikishe tunaenda kuusimamia, huu ni ukombozi kwa walipakodi, haki ya walipakodi inaenda kuimarishwa na mfumo utajenga uwazi,” ameongeza.
Awali Mkurugenzi wa Idara ya Tehama wa TRA, Emmanuel Nnko amesema mfumo huo ni msingi imara wa kuifanya Mamlaka hiyo kuwa yenye maarifa, inayojifunza na kubadilika kulingana na mazingira ya dunia ya sasa ya ukuaji wa kasi wa teknolojia.
“Idara ya Tehama itaendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha mfumo huu unapatikana wakati wote na kusaidia pale changamoto inapojitokeza wakati wa utekelezaji, wataalamu wetu wa Tehama wataendelea kuboresha mfumo huu ili kurahisisha matumizi yake na kuhakikisha inaunganishwa na mifumo mingine,” amesema.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa TRA, Moshi Kabengwe amesema mfumo utasaidia kuhakikisha maarifa yanazalishwa, yanahifadhiwa na kuwepo pindi yanapohitajika.
Amesema kumekuwa na changamoto ya muda mrefu, wakati mwingine maarifa kuwepo kwenye vitabu au majarida ambayo hayafikiki kirahisi huku mengine yakiwa kwa watu.
“Maarifa mengine yako kwenye vichwa vya watu ambayo hatuwezi kwenda kuyachukua, mfumo huu utarahisisha kuhakikisha maarifa yanapatikana, yanatumika na yanahifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye,” amesema.
Mkurugenzi huyo ametaja maeneo matatu yaliyopo kwenye mfumo huo kuwa ni moduli ya kwanza ambayo itawezesha watumishi wenye ujuzi, unaofanana kuwa na fursa ya kujadili maarifa au changamoto zinazowahusu kwenye eneo lao kwa pamoja.
Amesema hiyo itarahisisha badala ya kila mmoja kukaa akaumiza kichwa kwamba ninapata suluhu hii wapi, watajadili kwa pamoja na kufikia suluhisho na itahifadhiwa siku nyingine kukitokea suala hilo itatumika.
Ametaja moduli ya pili kazi yake ni kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu zote kwa ajili ya rejea huku ya tatu ikiwezesha watumishi kujisomea na kupata maarifa kwa urahisi kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni.
Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha amesema kuwa kuanzishwa kwa mfumo huo ni hatua ya kuwezesha Mamlaka kufanya kazi kwa ufanisi, weledi mkubwa na kuimarisha huduma wanazotoa kwa wananchi.