Vodacom inavyojivunia mafanikio ya ESG

Dar es Salaam. Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imeeleza mafanikio yake kupitia mfumo wa jumuishi wa Mazingira, Kijamii na Utawala (ESG) unaozinduliwa kesho Jumanne, Agosti 26, 2025, huku ikisisitiza kukuza ujumuishi wa kidijitali na kufanya biashara kwa uwajibikaji.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, inayohudumia wateja milioni 22.6 nchini na zaidi ya milioni 211 barani Afrika, ESG si mkakati wa pembeni bali ni sehemu ya malengo yake makuu ya kuunganisha watu kwa mustakabali bora.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ulioishia Machi 31, 2025, mfumo wa ESG wa Vodacom umejikita katika vipaumbele vya kuwawezesha watu, kulinda dunia na kudumisha uaminifu.

Vodacom imeendelea kupunguza pengo la kidijitali, hasa kwa wanawake na vijana, kupitia programu ya Code Like a Girl, wasichana 699 waliongezewa ujuzi kidigitali na kufanya jumla ya walionufaika kufikia 3,039 kati ya 2024 na 2025.


Katika ujumuishi wa kifedha, kampuni ilitoa mikopo ya Wakala Songesha ya Sh1.5 trilioni hadi Machi 2025, ikilinganishwa na Sh1.1 trilioni mwaka 2024. Hatua hii imesaidia wafanyabiashara wadogo na kaya kupata huduma za kifedha kupitia simu.

Bidhaa za kifedha za simu za Vodacom pia zimepata tuzo kwenye Tanzania Digital Awards.

M-Pesa super-app ilichaguliwa kuwa programu bora zaidi nchini kwa mwaka wa nne mfululizo, huku M-Koba ikitambuliwa kwa kuchochea utamaduni wa kuweka akiba kwenye jamii.

Katika kulinda mazingira, Vodacom iliwekeza Sh1.5 bilioni kwenye miradi ya ufanisi wa nishati mwaka 2024 na Sh1.4 bilioni kufikia Machi 2025. Uwekezaji huu umeokoa megawati saa 1,000 (MWh) na 2,861 MWh mtawalia.

Kampuni imeendelea kutambulika kimataifa cha ISO 50001 kwa usimamizi wa nishati, ufanisi na uendelevu.

Ili kupunguza taka, Vodacom imeokoa tani 242 za karatasi kupitia matumizi ya smart recharge.

 Aidha, kupitia kampeni ya upandaji miti chini ya Twende Butiama Cycling Tour, miti 18,000 ilipandwa katika shule na jamii na kufanya jumla ya miti iliyopandwa kufikia 37,000.

Kwa kushirikiana na Kampuni ya Gas Fasta, Vodacom imehamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni.

ESG inataja kuendeleza biashara endelevu na kuhakikisha uwajibikaji. 

 Ilitoa mfano kuwa wafanyakazi wote walikamilisha Programu ya Doing What’s Right inayohusu faragha ya data, usalama mtandaoni, kupinga rushwa, pamoja na afya na usalama kazini.

Vodacom pia imetambuliwa kitaifa kwa uongozi wake wa kiutawala ikitajwatajwa kama mwajiri bora nchini na Top Employer Institute, ilishinda tuzo kutoka kwa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa kuwa kioo kwenye kufuata mfumo wa ESG na ikapewa heshima na CEO Roundtable Awards kwa kuimarisha ushirikiano na maendeleo.

Vilevile, Vodacom ikawa miongoni mwa mashirika matatu ya kwanza nchini kupata cheti cha usajili wa Data Processor and Controller, hatua muhimu katika kulinda faragha ya taarifa.

Katika usalama kazini, wafanyakazi 379 walipimwa afya kazini na kaguzi 17 za Osha zilifanyika katika maeneo ya kampuni.

Dhamira thabiti, ushirikiano na MCL

Akizungumzia uzinduzi wa ripoti ya ESG, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire amesema:“Katika kipindi cha mwaka uliopita, tumedumisha juhudi zetu za kusukuma mbele ujumuishaji wa kifedha, upatikanaji wa huduma za kidijitali na uwajibikaji kwenye kimazingira. Maendeleo yetu yanapimwa si tu kwa teknolojia tunayoitumia, bali pia kwa athari chanya inayoleta katika maisha ya watu.”

“Kuanzia upanuzi wa huduma za kifedha za kidijitali na mtandao wa 4G katika maeneo ambayo hayajafikiwa, hadi kukuza ufanisi wa nishati na upandaji miti, tumeendelea kujitolea kufanikisha Dira ya Tanzania 2050 kuendeleza ukuaji shirikishi na mustakabali endelevu kwa wote.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalyn Mndolwa-Mworia, amesema:“Uzinduzi wa ESG wa Vodacom ni mwito wa kuchukua hatua kwa sisi sote. Hapa Mwananchi Communications tunajivunia kuwa jukwaa ambalo Serikali, biashara na wananchi wanakutana ili kuunda ajenda za kitaifa na kikanda kwa mustakabali endelevu na wenye ustawi.”

Kwa kuwafikia watu zaidi ya milioni 574 kupitia mitandao yake ya simu barani Afrika, Vodacom inasisitiza kuwa safari yake ya ESG inazidi kufuata masharti pekee; ni safari ya kusukuma ukuaji shirikishi sambamba na kukabiliana na changamoto za uendelevu duniani.