Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uvunjaji na kupora mali za wananchi.
Hayo yamesemwa leo Agosti 25, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Makambako.
New Content Item (1)
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Emmanuel Gakia maarufu Rasi mkazi wa Changarawe mkoani Iringa na Neema Joshua mkazi wa Lumumba, Makambako mkoani Njombe.
Amesema kulingana na taarifa za raia wema, watuhumiwa hao wanajihusisha na matukio ya uvunjaji na tayari mali mbalimbali zimekamatwa baada ya msako wa Jeshi la Polisi.
“Mali zilizopatikana ni pamoja na TV 10, magodoro matano, sabufa 10, spika 17, deki tatu, mitungi ya gesi miwili, mashine za kushonea masweta na guta moja,” amesema Banga.
Aidha jeshi hilo linamtafuta mtuhumiwa Gudluck Matandala na kutakiwa kujisalimisha kituo chochote cha polisi kutokana na kudaiwa kupokea mali hizo za wizi.

New Content Item (1)
Amesema jeshi hilo linafanya kazi ili kuhakikisha mji wa Makambako unaendelea kuwa salama na upelelezi utakapokamilika, watuhumiwa hao watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Ametoa wito kwa watu wote wanaojihusisha na uhalifu kuacha mara moja, kwani jeshi hilo lipo macho na kila atakayejiingiza kwenye uhalifu atachukuliwa hatua za kisheria.
Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Renata Mgalilwa amelipongeza jeshi hilo kwa kuendelea kuwakamata wahalifu, kwani hatua hiyo itapunguza matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza watu kuibiwa mali zao.