……………………….
Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua mradi wa kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani (Children in Street Situation (CiSS) utaotekelezwa katika mikoa ya Dar Es Salaam, Dodoma na Mwanza wenye lengo la kupunguza kuwapatia elimu, ujuzi na stadi mbalimbali kwa watoto waliokuwa wanaishi mtaani.
Waziri Dkt. Gwajima amezindua Mradi huo leo Agosti 25, 2025 jijini Dar Es Salaam huku akisema kuwa Serikali imechukua msimamo thabiti kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeachwa nyuma na kwamba kila mtoto, bila kujali asili au mazingira yake, anafurahia haki ya kulindwa, kutunzwa na kupata fursa ya kufikia uwezo wake kamili.
Ameongeza kuwa watoto wanaoishi katika mazingira ya mitaani wanawakilisha mojawapo ya makundi yaliyo hatarini zaidi katika jamii zetu. Kila siku wanakabiliwa na hatari zinazoweza kuathiri usalama, afya, elimu, na ustawi wao kwa ujumla hivyo mradi huo utasaidia juhudi za Serikali katika kuwanusuru watoto wanaoishi katika hayo mazingira.
“Ninapongeza Shirika la SOS Children’s Villages International na washirika wake kwa maono na kujitolea walikoonesha kupitia mradi wa CiSS. Tangu kuanzishwa kwake nchini Ethiopia mwaka 2022 na kupanuliwa hadi Tanzania na Rwanda mwaka 2023, mradi huu umeonesha jinsi uokoaji, ukarabati, urejeshaji kwa familia na ujumuishaji unaofanywa kwa uratibu unavyoweza kuleta matumaini mapya kwa watoto waliopoteza utoto wao kutokana na maisha ya mitaani.” amesema Waziri Dkt. Gwajima
Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara, imefanya ulinzi wa watoto wa mitaani kuwa kipaumbele cha kitaifa na ipo katika mchakato wa kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kumaliza Changamoto ya Watoto wa Mitaani, ambao utatumika kama mfumo kamili kwa wadau wote, hivyo mchango wa dhati wa SOS Children’s Villages Tanzania na washirika wengine katika mchakato huu kwani mchango wao wa kitaalam na uzoefu wao wa vitendo umekuwa muhimu katika kuhakikisha mpango huu unazingatia uhalisia na suluhisho za kiubunifu.
Ameeleza kuwa Serikali inabaki thabiti katika dhamira yake ya kuweka mazingira thabiti ya ulinzi kwa watoto kupitia utekelezaji wa sera, sheria, na mipango mbalimbali. Hata hivyo, juhudi za Serikali pekee hazitoshi kuleta mabadiliko ya kudumu. Ni muhimu tushirikiane kwa karibu na asasi za kiraia, taasisi za kidini, jamii, familia, na, muhimu zaidi, watoto wenyewe. Ni kupitia ushirikiano huu jumuishi na endelevu ndipo tunaweza kufikia maendeleo yenye maana na ya kudumu katika kulinda haki na ustawi wa kila mtoto.
Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando amesema Idara ya Ustawi wa Jamii inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha inawatoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa kuwa na mifumo thabiti na mipango mbalimbali ya kuwasaidia watoto hawa kuishi kama watoto walio katika familia.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Shirika la SOS Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Bedilu Shegen amesema mradi wa kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani (Children in Street Situation (CiSS)) umelenga kuwasadia watoto katika nchi za Afrika kwa kuwapatia huduma na stadi mbalimbali ambao wamepatwa na changamoto ya kuishi na kufanya kazi mitaani.