Yusuph Mhilu aongeza mmoja Geita Gold

GEITA Gold ya Championship imemwongezea mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji Yusuph Mhilu kuitumikia timu hiyo msimu ujao wa 2025/2026.

Msimu uliopita Mhilu aliifungia timu hiyo mabao 10 na asisti moja, jambo ambalo uongozi wa timu hiyo umeona umuhimu wa kuendelea naye, kutokana na mikakati yao ya kupanda Ligi Kuu.

Alipotafutwa Mhilu kuthibitisha hilo alisema baada ya kushindwana kimasilahi na baadhi ya timu za Ligi Kuu, hivyo akaona bora aendelee kucheza Championship msimu ujao

“Ni kweli nimesaini mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuona tumeelewana katika masilahi kama unavyofahamu soka ni kitega uchumi kwa wachezaji, ndiyo maana nimeshindwana na baadhi ya timu za Ligi Kuu,” alisema Mhilu na kuongeza;

“Kuna changamoto nimeiona kwa miaka ya hivi karibuni, mchezaji akicheza Championship inakuwa ngumu kupata timu za Ligi Kuu kwa masilahi mapana ila lazima kupambana hiyo ni kazi yetu.”

Mhilu ambaye aliwahi kuichezea Simba, Yanga, Kagera Sugar na Ndanda FC alisema soka la Tanzania kwa sasa lina thamani kubwa, hivyo wachezaji kutoka mataifa mbalimbali wanatamani kuja kucheza, ndio maana kunakuwa na ugumu wa kupata timu kwa wachezaji wazawa, kitu ambacho kitatubeba ni upambanaji tu.”