KOCHA wa Azam, Florent Ibenge, ameanza kufungua makali yake na sasa anatarajia kuwaacha wachezaji kadhaa waandamizi kwenye kikosi hicho.
Ibenge mmoja kati ya makocha wakubwa Afrika, alijiunga na Azam baada ya msimu uliopita wa ligi kumalizika na tayari timu hiyo imeshaweka kambi ya maandalizi mkoani Arusha kwa wiki mbili na sasa ipo nchini Rwanda ikiwa imeshacheza mechi nne za kujipima nguvu, huku kocha huyo akitumia sababu kuu tatu kuwatema mastaa hao.
Azam ambayo itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, inapambana kuona inafanya vizuri mashindano yote itakayoshiriki baada ya msimu ujao uliopita kumaliza nafasi ya tatu Ligi Kuu Bara nyuma ya mabingwa Yanga na Simba.
Ibenge ameanza kuonyesha moto wake baada ya kukaa na timu hiyo kambini kwa wiki tatu ambapo ameshaonyesha kutowakubali wachezaji kadhaa wa timu hiyo kwa sababu mbalimbali zikiwemo kimo cha mchezaji, kutokujituma pamoja na uwezo binafsi wa kupambana uwanjani ambao kocha huyo anautaka.
Jina ambalo linawashtua wengi ni chanzo kusema kuwa kocha huyo hamtaki kikosini ni nahodha wa timu hiyo Sospeter Bajana kutoka na aina ya wachezaji ambao amekuwa akiwatumia kwenye timu zote ambazo amekuwa akiwafundisha.
Kocha huyo wa zamani anamkataa Bajana kwenye timu yake siyo kwa sababu ya uwezo bali kimo chake kwani inaelezwa kuwa alishaueleza uongozi wa timu hiyo kwamba anataka kiungo mkabaji mwenye urefu wa futi 6 na kuendelea huku Bajana akiwa na futi 5.4.
“Awali kocha alishaueleza uongozi kuwa anataka kiungo wa namna gani kwenye timu yake, amekuwa muumini wa viungo warefu kuanzia futi sita na kuendelea ndiyo maana akamsajili Sadio Kanoute ambaye ana urefu wa futi 6.1 na sasa ndiye anaamini kuwa anaweza kuvaa jezi ya Azam,” kilisema chanzo kutoka Azam.
Hata hivyo, kuonyesha kuwa ni jambo la kweli, sehemu zote ambazo kocha huyo ametoka wachezaji wake wote ambao amekuwa akiwatumia ni wale ambao wana urefu huo na kuendelea.
Alipokuwa AS Vita alikuwa na Fabrice Ngoma (futi 6.2), Eddy Emomo (futi 6.1)na Nelson Munganga (futi 6).
Ngoma na Munganga pia ndio waliomsaidia Ibenge kushinda Kombe la CHAN mwaka 2016 akiwa na timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akiwa Berkane alikuwa Larbi Naji (futi 6.2), Bakr El Helali (fut 6.1), na Sofian El Moudane (futi 5.8).
Alipokuwa Al Hilal pia alikuwa na watu kama Aprocius Peter (futi 6), Guessouma Fofana (futi 6.1), Walieldin Khidir maarufu kama Pogba (futi 6.3) na huyu alimtaka sana aje naye Azam lakini ikashindikana, ndio akamchukua Sadio Kanoute mwenye futi 6.1.
Moja kati ya wachezaji waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuwika kwenye timu hiyo kwenye usajili huu ni Ever William Meza Mercado raia wa Colombia pamoja na Jhonier Blanco, lakini wiki tatu za kocha huyo mazoezini ameshasema kuwa haoni nafasi yao kwenye kikosi hicho kutokana kuwa hawajitumi vya kutosha mazoezini.
“Kocha amewaona kuwa hawawezi kumsaidia, akizungumza na wasaidizi wake anasema kuwa uwezo wanao tena wa juu kabisa, lakini hawajatumi hivyo kuna uwezekano mkubwa akaachana nao kabla dirisha la usajili halijafungwa, hata mazoezini wanaonekana kuwa chini sana,” kilisema chanzo.
Wengine ambao wanaonekana kutokuwa kwenye mipango yake ni Frank Tiesse na Mamadou Samake.
Pia kuna wachezaji wengine kadhaa ambao kocha Ibenge anatilia shaka uwezo.
“Maeneo wanayocheza Samake na Tiesse, mwalimu anasema ni sehemu ngumu kwao kupata nafasi, lakini pia kwa kuwa ni wachezaji wa kigeni anataka waondolewe ili waingie wengine kuchukua nafasi zao kwa kuwa hataki mgeni anayekaa benchi muda wote,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, kocha huyo ameonyesha pia mshangao mkubwa baada ya kuwakata wachezaji ambao walikuwa wanapewa nafasi kubwa ya kuwika wakiwa na Azam, James Akaminko na Yeison Fuentes ni wachezaji anaowatazama hadi Desemba huku akisema anaamini uwezo wao, lakini bado anafikiri anatakiwa kuwatazama zaidi hadi Desemba atatoa taarifa, anawaona ni wachezaji wakubwa lakini bado hawajamuonyesha makali.
Pia jambo la ajabu ni kwamba ameshaonyesha hali ya kuwakataa hata wachezaji waliosajiliwa kwenye dirisha hili na wengine akipendekeza mwenyewe, mfano anataka kuwatazama upya Mukhsini Malima, Himid Mao na Pape Doudou Diallo.
“Huyu Diallo uongozi unasema alimchagua mwenyewe lakini inaonekana hajakubali uwezo wake uwanjani hadi sasa.”
Hata hivyo, chanzo hicho kinasema kuwa pamoja na kocha huyo kuwaondoa wachezaji hao na tayari kuna wapya ukiachana na Issa Fofana, Muhsini Malima, Himid Mao na Pape Doudou Diallo, pia timu hiyo imemsajili, Aishi Manula, Edward Manyama, Sadio Kanoute, Tayeb Ben Zitoun, Baraket Hmidi, Japhet Kitambala na Lameck Lawi. Pia kuna wachezaji wengine kumi wapya kambini ambapo wanasubiri nafasi za wale ambao wanaweza kutemwa na wengine kocha huyo ataachana nao.