Jaji Mkuu awatangazia kiama waajiri, akililia haki za wafanyakazi

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, ametaka taasisi binafsi na Serikali kuheshimu haki za wafanyakazi, akisema waajiri wanaoshindwa kupeleka michango ya wafanyakazi watashughulikiwa.

Jaji Mkuu huyo amesema yupo hatua za mwisho kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali (GN) kanuni za kurekebisha sheria ya mwenendo wa madai, ili waajiri wanaoshindwa kupeleka michango ya wafanyakazi wachukuliwe hatua haraka.

Masaju, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), amesema hayo jana Jumatatu, Agosti 25, 2025, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tisa wa kamati ya utatu uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema ndani ya mwezi mmoja atafanyia mabadiliko hayo ili wadaiwa wa michango ya wafanyakazi mashauri yao yasipoteze muda wanapofika mahakamani.

“Umekata michango hukuiepeleka, ulikuwa unaipeleka wapi, huyu sio mtu wa kumsamehe kwenye fidia,” amesema.

Jaji Mkuu huyo amesema hata serikalini wapo waajiri wanakata michango ya wafanyakazi na hawapeleki, akitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushughulika nao.

“Shida zinapatikana pale watu wanapostaafu. Watu wakishastaafu wanaanza kufuatilia mafao na mifuko, nayo inaanza kumpiga chenga mara leta karatasi hii, mara ile. Ninyi mlikuwa na karatasi hizo tangu zamani, mnanidai mimi tena nini?

“Sijui hii akili ya zamani wametoa wapi. Yaani mimi nastaafu, sasa unaanza kuniambia ‘sijui leta hiki, leta kile’. Taarifa hizi mmekuwa nazo tangu mwanzo, na mimi kabla ya kustaafu tunawaambia, kabla ya miezi sita,” amesema.

Msimamo huo wa Jaji Mkuu Masaju umepokewa kwa mtazamo chanya na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Henry Mkunda, ambaye amesema wafanyakazi wanamshukuru Jaji Mkuu Masaju kwa kuzungumzia changamoto hiyo, akitambua ipo kwa wafanyakazi wengi.

“Ni kweli waajiri wengi wanachelewesha mafao ya wafanyakazi na sio kiinua mgongo tu. Hata NSSF ya matibabu, mfanyakazi anapofuatilia anaambiwa hana sifa kwa sababu michango haikuwasilishwa. Kwa hiyo, alichozungumza Jaji Mkuu, akitumia njia zake kukomesha hilo, ni faida kwa wafanyakazi,” amesema Mkunda, alipozungumza na Mwananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzane Ndomba, amesema wanawasisitiza waajiri kupeleka michango kwani ni takwa la kisheria.

“Pia tunawapa elimu kuhusu sheria za hifadhi ya jamii na tunafanya kazi kwa kushirikiana na mifuko, hasa kwenye mafunzo na ufuatiliaji. Suala la kanuni ni sawa, lakini nafikiri kwanza uelewa wa dhana nzima ya hifadhi ya jamii ni muhimu,” amesema.

Ametolea mfano sekta isiyo rasmi inayokabiliwa na changamoto katika suala zima la hifadhi ya jamii.

“Nafikiri tushirikiane kutoa elimu,  Serikali, waajiri na wafanyakazi. Kucheleweshwa kwa mafao kuna sababu nyingi, nafikiri mifuko inaweza kueleza vizuri. Lakini rai yangu kwa waajiri ni kuhakikisha wanawasilisha michango ya wanachama kwa wakati kuepuka kupelekwa mahakamani,” ameeleza.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jaji Mkuu huyo aligusia kikokotoo cha zamani akipendeza kirudi kwa watumishi wa Serikali Kuu kama ilivyokuwa zamani, kwani hakiwezi kufikia hatua hiyo kama wengine hawalipi michango yao.

Kwa kuwa majaji wanajua wastaafu watarajiwa hawatakuwa na la msalia, kesi za madai zinapopelekwa mahakamani, kwani wapo na majaji ambao mafao yao hayalipwi.

Amesema yeyote atakayepelekwa mahakamani na ushahidi ukawepo wa kutosha, wote watawajibishwa kutokana na matendo yao.

Pamoja na hayo, amewasisitiza wafanyakazi kuhakikisha wanafuatilia michango yao inakwenda mahala sahihi.

“Hifadhi ya jamii ni muhimu sana na imewekwa kwenye Katiba yetu, ibara ya 10. Sasa ibara ya 142 ya Katiba, pamoja na mambo mengine yanayozungumzia mfuko mkuu wa Serikali, inatambua mambo ya kiiunua mgongo na malipo ya uzeeni,” amesema Masaju.

Amesema moja ya vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ni haki, hivyo katika Taifa la wananchi wenye usawa lazima haki iheshimiwe, na kipengele cha uwekezaji hakiwezi kutumika kuficha ukiukaji wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kucheleweshwa kwa mafao, Jaji Mkuu huyo amehoji namna sheria inavyotafsiriwa, akisema majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani mishahara yao ni duni na hawana fursa kama wengine.

Masaju amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na kudumisha nidhamu ya kazi, akiwasisitiza pia kutambua haki zao na kuangalia usalama wao mahala pa kazi.

“Kuna sehemu fulani waajiri hawapeleki hii michango, sijui kwanini. Na waajiri, mnapowaajiri wafanyakazi, waelimisheni haki zao na ninyi wafanyakazi msibweteke kuhusu kutambua haki zenu,” amesema.

Amewataka waajiri kuthamini maisha ya wafanyakazi badala ya kuangalia faida pekee. Ametolea mfano muajiri kukata fedha za wafanyakazi na kutozipeleka michango panapostahili, akihoji: ni wapi fedha hizo muajiri anazipeleka?

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Dk Yose Joseph, amesema kupitia mkutano huo wamezindua juzuu mbili za uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu migogoro ya kazi nchini.

Amesema sababu ya kuwepo kwa juzuu hizo ni kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu bado una uzito mkubwa wa kisheria wa kuripotiwa na yanatoa muongozo kwa vyombo vya chini.

Kwa upande wake, Shirika la Kazi Duniani (ILO), limesema katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ni muhimu Tanzania iweke kipaumbele katika ajira zenye staha kwa kuwa ndiyo msingi wa amani na utulivu wa jamii.

Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla, amesema: “Ajira yenye staha ni msingi wa amani, utulivu wa kijamii na maendeleo jumuishi. Bila kuhakikisha heshima, ulinzi na fursa, kwa kila mfanyakazi awe wa sekta rasmi au isiyo rasmi, hatuwezi kufanikisha maendeleo ya kweli.”

Amesema Dira ya 2050 ya Tanzania si tu mpango wa kiuchumi, bali ni mkataba wa kijamii unaolenga kuhakikisha ukuaji jumuishi, haki na fursa zinapanuliwa kwa wananchi wote.

Kwa mujibu wa Mugalla, vyama vya wafanyakazi vina jukumu la kuhakikisha sauti za makundi yote ya wafanyakazi zinasikilizwa na mahitaji yake kutimizwa.

“Vyama lazima viendelee kutetea haki, pia viwe na ubunifu kusaidia wafanyakazi kukabiliana na changamoto za kidijitali, mabadiliko ya tabianchi na utandawazi,” amesema.

Kwa upande wa waajiri, amewataka waongoze kwa kuunganisha ushindani wa kibiashara na uwajibikaji wa kijamii, kuwekeza katika mafunzo ya stadi kwa vijana, kuboresha mazingira salama kazini na kuunga mkono ajira zinazolinda mazingira huku zikiongeza tija.

Amesema taasisi za Serikali zina wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayoruhusu kuwepo kwa ajira zenye staha, huku Mahakama na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) zikitoa haki kwa wakati ili wananchi waamini mfumo wa haki za kazi.

Ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha) kuimarisha usalama kazini, kwani hakuna anayepaswa kuhatarisha maisha yake ili apate kipato, huku taasisi za hifadhi ya jamii zikitakiwa kupanua wigo ili kuwafikia wa sekta isiyo rasmi.

“Sekta isiyo rasmi ndiyo chanzo kikuu cha kipato kwa Watanzania wengi, lakini wafanyakazi wake wanabaki bila ulinzi. Kurasimisha si suala la kufuata sheria pekee, ni suala la heshima, usawa na maendeleo ya Taifa,” amesema.