Mbeya. Jeshi la Magereza mkoani Mbeya limeiomba jamii kuwapokea vizuri wafungwa wanaomaliza muda wao wa adhabu gerezani kurejea uraiani, ili kuwafundisha kutii sheria na kuondokana na uhalifu.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Agosti 26, 2025 kwenye maadhimisho ya miaka 64 ya Jeshi la Magereza baada ya uhuru, na Mkuu wa Gereza la Ruanda jijini Mbeya, Christopher Fungo, kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Raymond Mwampashe.
Fungo amesema wafungwa hao ni sehemu ya familia na jamii kwa ujumla, hivyo wanapomaliza adhabu zao gerezani wapokelewe vizuri, akiomba jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza kuwafundisha kutii sheria.
Amesema jeshi hilo limeendelea kuimarika na kuendana na mahitaji ya kijamii, kuzingatia haki za binadamu na maendeleo ya teknolojia na kuwa kiungo katika kuandaa watu waliorekebishwa wakiwa gerezani.
“Katika kipindi cha ukoloni wa Kijerumani, Magereza ilikuwa chombo cha ukandamizaji na kutesa wananchi ili wakubaliane na utawala wao na sheria zao za kikoloni, baada ya uhuru ilibadilishwa kuwa sehemu ya urekebishaji wafungwa.
“Katika kutekeleza azma ya urekebu, jeshi hili lilianzisha mafunzo kwa wananchi na programu kwa wafungwa katika kusimamia haki, urekebishaji, usalama na uzalishaji,” amesema na kuongeza:
“Kwa miaka ya 2,000 hadi sasa, jeshi limetekeleza mabadiliko ya kimfumo kama kuboresha afya kwa wafungwa, elimu ya msingi, sekondari na ufundi katika magereza yaliyotengwa kama Wami Kuu vijana (Morogoro) na Ruanda (Mbeya),” amesema Fungo.
Kamanda huyo ameongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likishirikiana na taasisi za kimataifa ikiwamo UNHCR (Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi), UN (Umoja wa mataifa), Unicef (Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto) na ICRC (Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu) katika kusimamia haki, ulinzi wa amani na kuwa sehemu ya maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema Serikali imekuwa sehemu ya mabadiliko ya Jeshi la Magereza kwa kuboresha maeneo mengi ya jeshi hilo.
Amesema baadhi ya sehemu hizo ni kuongeza mishahara kwa askari, ujenzi wa magereza mpya, maboresho, ukarabati wa miundombinu ya magereza na uundwaji tume ya haki jinai inayopunguza msongamano wa wafungwa magerezani.
“Tunaenda kwenye uchaguzi, wafungwa waliojiandikisha wapewe haki yao kupiga kura, wapewe mafunzo ya stadi za kazi, ongezeni nguvu katika uzalishaji na mbuni miradi mingine ya uchumi ili kujitegemea,” amesema.