Lusaka. Zikiwa zimetimia siku 82 tangu Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu (68), afariki dunia, mvutano wa mazishi yake umewaibua viongozi wa dini ambao wametoa wito kwa Serikali kuanzisha majadiliano ya haraka na dhati kwa familia yake.
Tangu kufariki dunia kwa Lungu, Juni 5, 2025 Serikali ya Zambia imeingia kwenye mvutano na familia kuhusu wapi mazishi yake yafanyike. Familia inataka azikwe Afrika Kusini huku Serikali inataka azikwe Zambia.
Wito wa viongozi hao wa Kikristo umetolewa ikiwa ni siku 61 tangu Serikali ya Zambia ipate amri ya Mahakama Kuu ya Afrika Kusini kusitisha mipango ya kumzika Lungu huko Johannesburg Juni 25, 2025, saa chache kabla ya kuanza kwa ibada ya mazishi ya faragha.
Taarifa iliyotolewa Agosti 23, 2025 na viongozi wa makanisa wakiwamo Baraza la Maaskofu Wakatoliki wa Zambia (ZCCB), Ushirika wa Kinjili wa Zambia (EFZ), na Baraza la Makanisa Zambia (CCZ), inaeleza kuwa, majadiliano hayo yanapaswa kufanyika kwa njia inayoheshimu ofisi kuu aliyowahi kuishikilia (Rais Lungu) pamoja na matakwa ya familia yake.
Viongozi hao wameitaka Serikali kuanzisha majadiliano ya haraka na ya dhati ili kutatua mvutano uliopo kuhusu mazishi ya kiongozi huyo wa zamani aliyekuwa madarakani kati ya mwaka 2015 hadi 2021, aliposhindwa kwenye uchaguzi na Hakainde Hichilema.
Viongozi hao wa kanisa wameeleza matumaini yao kuwa, mazishi ya Rais wa zamani yatafanyika katika mazingira ya amani, umoja na heshima, inayoendana na huduma aliyotoa kwa Taifa na maadili.
“Kwa msingi huo, tunawaomba Wazambia wote, bila kujali itikadi za kisiasa au kijamii, kujiepusha na matamshi ya uchochezi au ya kudhalilisha kuhusu suala hili nyeti,” inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisainiwa na Katibu Mkuu wa ZCCB, Padre Francis Mukosa, Katibu Mkuu wa CCZ, Mchungaji Emmanuel Chikoya na Katibu Mtendaji wa EFZ, Askofu Andrew Mwenda, ambao wamesisitiza matamshi ya kudhalilisha yanakiuka maadili ya kitamaduni na misingi ya Kikristo.
Wawakilishi wa CCZ, EFZ na ZCCB pia walipongeza hatua ya Serikali kuzuia kauli za umma kuhusu mazishi ya Rais wa zamani, wakisema: “Ingawa uamuzi huo wa Serikali umetolewa kwa kuchelewa, ni hatua ya kupongezwa na muhimu katika mchakato wa uponyaji wa kitaifa na kujenga ushirikiano wa kweli na familia ya marehemu Rais.”
Hata hivyo, wawakilishi hao wametoa wito kwa waumini na wananchi wa Zambia kubaki wamoja kama watoto wa Mungu.
Juni 19, mwaka huu viongozi wa Kanisa walielezea masikitiko yao juu ya hali ya sintofahamu kuhusu mazishi ya Rais huyo wa zamani, wakionya kuwa hali hiyo inaathiri uendeshaji wa Taifa kwa jumla, ambalo bado liko katika maombolezo.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba, mazishi ya kiongozi mkuu wa zamani bado yako njia panda,” inaeleza taarifa ya Juni 19 ikirejelea hali ya kutokuwepo kwa uhakika kuhusu urejeshaji wa mwili wa Rais ambao awali ulikuwa umepangwa kurejeshwa Juni 18 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ripoti ya BBC ya Juni 19, familia ya marehemu Rais Lungu ilizuia urejeshaji wa mwili wake kutoka Afrika Kusini, ikidai kuwa Serikali ya Zambia ilikiuka makubaliano muhimu ya mazishi, ikiwamo kutangaza ratiba ya mazishi bila kushauriana na familia.
Mahakama Kuu ya Afrika Kusini iliamua kuwa Serikali ya Zambia ina mamlaka ya kuurejesha mwili wa marehemu kwa mazishi ya kitaifa, licha ya familia kutaka azikwe kwa faragha Afrika Kusini.
Marehemu Lungu, ambaye kitaaluma alikuwa wakili, alipanda madarakani baada ya kushika nyadhifa za Waziri wa Sheria na Waziri wa Ulinzi chini ya uongozi wa Rais Michael Sata (kwa sasa ni marehemu).
Mahakama Kuu Afrika Kusini ilitoa uamuzi kuwa Serikali ya Zambia inaweza kuurejesha mwili wa Lungu na kumfanyia mazishi ya kitaifa, licha ya pingamizi kutoka kwa familia yake.
Familia ya Lungu ilitaka azikwe kwa faragha Afrika Kusini alikofia wakati wakipatiwa matibabu.
Akitangaza uamuzi huo, Jaji Aubrey Ledwaba alisema Serikali ya Zambia ina haki ya kuurejesha mwili wa Rais huyo wa zamani na akaamuru familia yake ikabidhi mwili huo mara moja kwa mamlaka husika.
Baada ya Lungu kufariki kutokana na ugonjwa ambao haukutajwa akiwa na umri wa miaka 68, familia ilitaka iwe na udhibiti wa mipango yote ya mazishi, ikiwamo urejeshaji wa mwili wake, lakini mamlaka za Zambia zilikuwa zikitaka kudhibiti mchakato huo.
Awali, Serikali na familia yake walikubaliana kuwa angefanyiwa mazishi ya kitaifa, lakini uhusiano wao ukavunjika kutokana na kutokubaliana juu ya baadhi ya mipango, hali iliyoifanya familia kuchagua kumzika Afrika Kusini.
Dada wa marehemu, Bertha Lungu alilia mahakamani baada ya uamuzi huo kutangazwa.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha, alisema uamuzi huo haukuwa ushindi kwa Serikali bali ni jambo la busara.
“Unapokuwa baba wa Taifa, huwezi kujiwekea mipaka kwa familia yako ya karibu tu,” alisema.
Kabesha aliisifu Mahakama kwa kutoa uamuzi wa busara, akisema ingawa familia ina haki ya kukata rufaa, tukio hilo linatoa funzo kwa wale wanaotamani kushika nafasi ya juu ya uongozi.
Mgogoro huu unatokana na uhasama wa muda mrefu kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema, familia ya Lungu imedai kuwa alieleza wazi kuwa Hichilema asihudhurie mazishi yake.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.