Kihogonsi awajibu wanaoandamana CCM kupinga ‘kukatwa’ watiania

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi amewasititizia WanaCCM kuheshimu uamuzi wa vikao kuhusu watiania walioteuliwa na chama hicho kuwania ubunge na udiwani.

Amesema kila MwanaCCM anapaswa kutambua, kuheshimu chama hicho, badala ya watu ndani ya chama, akitumia msemo wa ‘chama kwanza, mtu baadaye.’

Kihongosi ameeleza hayo leo Jumanne Agosti 26, 2025 katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa halmashauri kuu, viongozi wa CCM wa wilaya, kata na Jumuiya za mkoa wa Dar es Salaam.

Hii ni ziara yake ya kwanza kwa Kihongosi ambaye aliteuliwa na Halmashauri Kuu  Agosti 23, 2025 jijini Dodoma. Kihongosi amechukua nafasi ya Amos Makalla aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

“Hapa juzi kamati kuu na halmashauri ilipitisha majina ya watiania, kuna baadhi ya wanachama wetu wametoka hadharani na kurudisha kadi wanasema maneno, maana yake hawakuwa wafuasi wa chama bali wafuasi wa mtu ndani ya chama,”amesema Kihongosi.

Kauli ya Kihongosi inawajibu baadhi ya baadhi ya makada waliojitokeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo, Tarime, Tanga na Nachingwea waliotoa madai ya kutaka watiania wanaowaunga mkono na kuwekwa kando, warejeshwe kwenye kinya’ng’iro.

Agosti 24, 2025 katika mitandao ya kijamii walionekana wanachama wa CCM Jimbo la Tanga Mjini wakiandamana nje ya ofisi za chama hicho, wilayani humo kwa lengo la kuwasilisha malalamiko yao, baada ya Ummy Mwalimu kuwekwa kando, licha ya kuongoza kura za maoni.

Wanachama hao walidai hatua ya CCM kumpitisha Kassim Mbaraka, aliyepata kura 80 pekee kwenye kura za maoni, badala ya Ummy aliyepata kura 5,750, ni kitendo cha dharau na kupuuza sauti za wanachama wa ngazi za chini.

Siyo Tanga pekee, bali hata Tarime baadhi ya makada walionekana wakilalamika wakikitaka CCM kumrejesha Michael Kembaki aliyekuwa ameongoza katika kura za maoni, lakini aliwekwa kando na nafasi yake ikachukuliwa na Ester Matiko.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti Ummy na Kembaki walizungumza na wanahabari wakiwahisi wanachama hao kuheshimu uamuzi wa vikao, huku wakisema wapo tayari kutoa ushirikiano kwa watiania waliopendekezwa na chama hicho.

Katika hatua nyingine,Kihongosi amesema CCM kimekuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo na kuwafundisha siasa makada wa chama hicho, ili kuwapika kuwa wanachama bora kupitia vyuo viliyopo mikoa ya Pwani,Unguja, Dar es Salaam na Iringa.

Hata hivyo, Kihongosi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM), amesema imefika wakati kuna watu wanadhani wanaweza kukichezea CCM wanavyotaka, jambo ambalo si rahisi kwa sababu ya misingi iliyowekwa.

Katika maelezo yake, Kihongosi amesema kuna watu walioaminiwa na chama hicho, na kupewa heshima kubwa za uongozi wa juu ndani ya ccm, lakini wamengeuka na kuwa mwiba wa upotoshaji kwa Watanzania.

“Wakulinda CCM ni mimi na nyinyi (wanachama na viongozi.Wakulinda chama hiki ni makada wa kweli wasiokuwa na unafiki,” ameeleza, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kabla ya uteuzi huo.

Mbali na hilo, Kihongosi amesema miongoni mwa majukumu kwa sasa ni kuhakilisha chama hicho kinaibuka na ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu 2025 utakaofanyika Oktoba.

Awali, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu amesema uchaguzi wa serikali za mitaa CCM ilishinda mitaa yote ya mkoa huo, akisema hiyo ni dalili kwamba katika uchaguzi wa Oktoba wataibuka kidedea.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), Zainab Shomary amesema jumuiya hiyo ipo imara na wapo mguu sawa kumchagua Samia.

“Jumuiya tumejipanga tupo vizuri, tunajua kura zetu ni wapi tutazipata. Tumejipanga juzi tulifanya mafunzo kuhusu mkakati huu na viongozi wa mikoa wanajua,” amesema Zainab.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Richard Kasesela amesema yeye na Mwenyekiti wa UWT wameteuliwa na kamati kuu ya CCM kuhakikisha Dar es Salaam chama hicho kinashinda kwa kishindo.

“Tutaingia kila sehemu kuhakikisha kura za Samia zinapatikana kwa wingi,naomba msiniungushe mimi mwenyewe ni mtoto wa Dar es Salaam.Uchaguzi ni namba nataka kila MwanaCCM wa mkoa wa Dar es Salaam alete wapiga kura,” “Dar es Salaam nataka iongoze kwa kura Tanzania, lakini lazima tujitume,” amesema Kasesela.

Chalamila aonya watakavuruga amani

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema amehudhuria mkutano wa Kihongosi ikiwa ni mwendelezo wa kuhudhuria mikutano yote ya vyama vya siasa pasipo kujali vyama.

“Nikitoa hapa nakwenda mkutano wa CUF, kisha nitakwenda wa Chaumma ili kueleze masuala ya Serikali kwa wanachama wa vyama hivyo. Wajibu wangu ni kuhakikisha CCM kinakuwa balozi sahihi wa kulinda amani na mshikamano,”

“Mtu yeyote awe MwanaCCM au chama chochote atakayeharibu mustakabali wa amani uliojengwa, Serikali haitaogopa rangi ya kijani au njano itamdhibiti mtu yeyote bila itikadi ya chama ilimradi uimara ya kisiasa uwepo,” amesema Chalamila.