Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo katika kuhakikisha ulimwengu wa kidijitali unamfikia kila Mtanzania amesema lazima watu wawezeshwe bila kusahau ushirikiano wa sekta binafsi, miundombinu na sera madhubuti.
Ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 26, 2025 jijini Dar es Salaam, kwenye uzinduzi wa ripoti ya ujumuishi wa Mazingira, Kijamii na Utawala (ESG) ya Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania ikishirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
Amesema suala lililopo sasa watu wanafuata huduma za Serikali kwa kwenda ofisini bali dunia ya sasa ilipo na lengo la Serikali hata katika dira ya 2050 ni watu kufuatwa walipo, na hilo linawezekana kupitia uboreshwaji wa kidijitali.
“Ulimwengu wa leo, na kile tunachotazamia katika miaka ijayo si Serikali tu kuwa karibu na watu, lakini kwa hakika Serikali inayowafuata watu mahali walipo na hilo linawezekana,” amesema.

Hapa ndipo ushirikiano unapohitajika huku akitolea mfano kampuni ya Vodacom ilivyo muhimu na wanafanya kazi nayo kwa karibu, ili kuona jinsi inavyoweza kufanya uwekezaji kidijitali kwa gharama nafuu.
“Katika kufanikisha hilo, jambo la kwanza linatoka kwenye sera ambayo ni jukumu la Serikali katika uwezeshaji. “Ushirikiano kama tulivyofanya katika dira iliyopita ambapo tulifanya kazi na kila mtu ikiwa ni pamoja na sekta binafsi,” amesema.
Profesa Mkumbo amesema Serikali lazima ihakikishe miundombinu ya msingi ya kifizikali na kidijitali ipo ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi.
“Kwa hivyo, hii ndiyo sababu unaweza kuona kwamba tunasukuma miundombinu mingi ya kiuchumi, huwezi kuwa unazungumza kuhusu uboreshaji wa kidijitali bila kuwa na mtandao wa kuaminika na wa haraka.”
“Kwa hivyo, sera na miundombinu ni nyenzo mbili muhimu za kuhakikisha kuwa sekta binafsi inastawi hapa nchini.”