Lindi yataja mikakati kufanikisha upatikanaji nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu

Lindi. Kupata nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu ni moja ya malengo makuu ya Serikali kupitia mpango wa ruzuku unaolenga kuwasaidia wananchi kuachana na kuni na mkaa.

Katika matokeo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) namba mbili, lengo ni kuongezeka kwa upatikanaji na usambazaji wa nishati safi, nafuu, endelevu na ya uhakika ya kupikia kwa kuimarisha miundombinu, upatikanaji wa malighafi na kurahisisha njia za ununuzi wa nishati hizo.

Katika mkoa wa Lindi, jitihada za kufanikisha hili zimeanza kwa taratibu kwa kushirikisha taasisi za umma na wadau binafsi, ili kuhakikisha mitungi ya gesi na majiko banifu yanapatikana kwa gharama nafuu.

Hata hivyo, pamoja na mpango huo, changamoto za kipato cha wananchi, gharama za awali na upungufu wa vituo vya usambazaji vijijini bado zinakwamisha kasi ya mabadiliko.

Katibu Tawala Wilaya ya Lindi, Hudhaifa Rashidi, anasema juhudi za kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa zimekuwa zikiendelea kwa muda mrefu kwa kushirikiana na viongozi na taasisi mbalimbali.

 “Tunatoa elimu mara kwa mara kwa wananchi na kuendesha vikao na viongozi wa wilaya ili kuhakikisha kila mtu anaelewa faida za kutumia nishati safi,” anasema.

Kwa mujibu wa Rashidi, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeshaanza mchakato wa kuleta majiko banifu kwa bei ya Sh9,000 na mitungi ya gesi kwa Sh19,000 kabla ya mwaka huu kuisha.

Rashidi anasema hayo kutokana na uhalisia kuwa gharama ya jiko banifu mkoani hapa ni zaidi ya Sh25,000 na mtungi wa gesi unauzwa hadi Sh40,000.

Anasisitiza kuwa hata baada ya mpango wa ruzuku kukamilika, wilaya imejipanga kutumia mapato yanayotokana na mazao ya korosho na ufuta ili kusaidia wananchi kupata nishati safi kwa gharama nafuu.

“Tumeanza kuona mafanikio kwani taasisi kama magereza ya mkoa na baadhi ya shule za sekondari zinatumia nishati safi. Tumekubaliana na Rea kuhakikisha majiko banifu yanapatikana kwa bei nafuu zaidi, na mitungi ya gesi inauzwa kwa Sh9,000. Tunashirikiana na taasisi kama Tatedo (shirika lisilo la kiserikali linalohamasisha nishati mbadala, maendeleo endelevu na mazingira) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi,” anasema Rashidi.

Anaongeza kuwa barabara zilizojengwa na Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) na Wakala wa Barabara (Tanroads) zimesaidia kufikisha elimu na mitungi hadi vijijini.

“Tumeanza kusambaza mitungi kwa wananchi walioko pembezoni kabisa. Tukishikamana kama viongozi na wananchi, tunaamini Lindi inaweza kufikia asilimia 100 ya matumizi ya nishati safi,” anasema.


Pamoja na jitihada hizo, hali ya wananchi wengi wa Lindi bado ni ngumu, kwani wanategemea kuni na mkaa kwa sababu gharama za awali za vifaa vya nishati safi ni kubwa na vituo vya usambazaji havipatikani kwa urahisi vijijini.

Mariamu Juma, mkazi wa Mtuleni, Lindi Mjini na mfanyabiashara wa kuuza mihogo, anasema gesi inamshinda kutokana na kipato kidogo.

“Nanunua kuni kwa Sh2,000 kila siku, lakini mtungi mdogo wa gesi unahitaji zaidi ya Sh25,000 kubadilisha, nikitaka kununua na mtungi ni zaidi ya Sh40,000. Sina uwezo wa kumudu, ingawa najua kuni zina madhara kwa afya,” anasema.

Mariamu anaiomba Serikali ipunguze bei na iweke vituo vya kujazia karibu na vijiji ili waweze kupata huduma hizo.

“…ninajua madhara ya kuni na mkaa kwenye afya, lakini kutokana na kipato changu simudu gharama hizo. Serikali ingeharakisha upatikanaji wake au utoaji wa ruzuku ili na sisi tutumie nishati safi,” anasema.

Mkazi wa Manispaa ya Lindi, Abdalla Saidi, anasema wanaume  wanapaswa kuelimishwa zaidi kuhusu umuhimu wa nishati safi.

“Mwanaume akiwa kiongozi wa familia akielewa, familia nzima itaelimika. Serikali itazame zaidi maeneo ya pembezoni kwa sababu bado kuna uelewa mdogo kuhusu faida za nishati safi,” anasema.

Saidi ambaye ana familia ya watu saba, anasema jukumu la kutafuta kuni ni la mkewe na wanawe wakubwa. “Japo nashiriki kwenye kutafuta kuni mara kadhaa, lakini hilo ni jambo la mama,” anasema.

Athari za moshi wa kuni na mkaa

Kaimu Ofisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira, Manispaa ya Lindi, Maajabu Mkungu, anasema moshi wa kuni unaharibu mazingira na afya.

“Hewa yenye sumu inayotokana na moshi huleta madhara makubwa, ikiwemo kuathiri macho na kupunguza ubora wa hewa. Wananchi wajitahidi kutumia gesi au majiko banifu,” anasema Mkungu.

Mwenyekiti wa mtaa wa Sabasaba katika Manispaa ya Lindi, Elizabeth Michenje, anasema elimu imetolewa lakini uwezo wa kifedha unakuwa kikwazo.

“Wachache sana mtaani kwangu wanatumia gesi. Wengi bado wanategemea kuni na mkaa. Tunaiomba Serikali iendelee kutoa mitungi ya ruzuku ili kila mtu aweze kuipata kwa bei nafuu,” anasema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine, Dk. Alexander Makalla, anasema madhara ya kiafya ni makubwa.

“Moshi wa kuni na mkaa unasababisha pumu na kansa ya mapafu. Wananchi waache kutumia nishati chafu kwa manufaa ya afya zao,” anasema.

Wataalamu wa sekta ya nishati safi wanasema Lindi itabaki nyuma kwenye utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) bila hatua madhubuti.

Wanashauri Serikali kushirikiana na sekta binafsi kupunguza gharama za awali kwa kutoa ruzuku na mikopo nafuu.

“Mfumo wa kulipia kidogo kidogo unaweza kusaidia familia nyingi kumudu gesi au majiko ya umeme,” anasema Maajabu Mkungu.

Aidha, kampeni za kitaifa za elimu kwa umma zinahitajika ili kuondoa hofu kuhusu usalama wa gesi na kuongeza uelewa wa faida zake kiafya na kimazingira.

Pamoja na changamoto hizo, Lindi ina rasilimali kubwa ya gesi asilia. Wachambuzi wa maendeleo wanasema wananchi hawaoni faida ya moja kwa moja, licha ya kuwa gesi hiyo ipo.

Serikali kupitia TPDC tayari imeunganisha zaidi ya kaya 200 katika eneo la Mnazi Mmoja na inalenga kuunganisha kaya nyingine 473. Hata hivyo, mpango huo unapaswa kupanuliwa ili kufikia vijiji vya pembezoni.

Elizabeth Michenje, anasema ili Lindi ifikie lengo la kitaifa la asilimia 80 ya wananchi kutumia nishati safi kufikia mwaka 2034, kuna haja ya mchanganyiko wa sera thabiti, uwekezaji wa miundombinu, ruzuku, mikopo nafuu na kampeni za elimu ya umma.

“Bila hatua hizo, utegemezi wa kuni na mkaa utaendelea kudumaza afya, mazingira na maendeleo ya uchumi wa mkoa huu,” anasema.