Mazishi ya mfanyabiashara yasimamisha shughuli Songea

Songea. Mazishi ya mfanyabiashara  mashuhuri wilayani Songea  Mkoa wa Ruvuma, Titus Mbilinyi maarufu Mwilamba ambayo yamefanyika leo Agosti 26,2025 kwenye kiwanda chake cha mifuko kilichopo  Ruhuwiko yamesimamisha shughuli ikiwamo maduka kufungwa.

Tangu   saa 12 asubuhi  maduka mengi yamefungwa ikiwa ni ishara ya heshima kwa ajili ya kumsindikiza mfanyabiashara huyo, aliyekuwa kipenzi cha wanyonge.


Mamia ya watu wamejitokeza na kusimama pembezoni mwa barabara kutoa heshima zao za mwisho, wakati msafara wa magari uliosindikiza mwili wa marehemu ukipita kuelekea katika kiwanda chake, ambako ndiko amepumzishwa milele.

Akihubiri wakati wa ibada ya mazishi, Askofu wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, Dk Martine Mlata amesema marehemu alikuwa tajiri si tu kwa mali, bali pia kwa matendo mema.

Dk Mlata amesema marehemu enzi za uhai wake alijitolea kwa dhati kuwekeza kwa watu wanyonge na kuwasaidia bila ya kujisifu wala kuwadhalilisha.

Ameongeza kuwa marehemu Tito Mbilinyi, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma, ameacha alama isiyofutika kupitia kazi kubwa aliyoifanya mkoani humo.

“Maisha ni dhamana, ripoti ya marehemu inatia moyo na amefanya kazi kubwa hivyo ana wajibu wa kurudi nyumbani, hivyo kila mtu ajiandae vizuri ili muda wake ukifika wa kupumzika aache alama kwenye jamii,” amesema.


Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Marry Mwakondo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa  huo, ametoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki  na jumuiya ya wafanyabiashara nchini kwa niaba ya Serikali.

Amesema msiba huo umeacha pengo kubwa kwa jamii na familia.

Mwakondo amesema, marehemu atakumbukwa katika kuwaunganisha wafanyabiashara alikuwa mstari wa mbele kusikiliza na kuziwakilisha changamoto zao kwa uwazi, alikuwa kiongozi shupavu, jasiri na mwenye upendo wa kweli.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho amesema chama kinatambua kazi kubwa iliyofanywa na marehemu enzi za uhai wake.

Amesema marehemu enzi za uhai wake amesaidia kutekeleza ilani CCM kupitia wakulima wadogowadogo na wa kati.

“Alikuwa sehemu ya ukombozi kwa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma, alikua akileta changamoto za wakulima ofisini na kuwaelekeza, kuwaelimisha wafanyabiashara na walimsikiliza.

“Alikuwa ni kiongozi wa aina yake, aliwahudumia wakulima huduma za pembejeo na viatilifu na alikua akitukopesha mbolea na mimi nina deni alikuwa muungwana na kiukweli tumempoteza mtu muhimu sana,” amesema.


Mwisho amesema Mbilinyi kwa miaka mitano mfululizo alikua akimkopesha mbolea zaidi ya mifuko 40 na wakulima walinufaika kukopeshwa na kusaidiwa ushauri, hivyo ameitaka familia idumishe biashara hiyo na wale waliosaidiwa wawe na moyo wa kurudisha, siyo mpaka wafuatwe na dalali ili kampuni hiyo iendelee kusaidia watu wengine.

” Huu ni moyo wa upendo bila kujali mtapata hasara na mmefunga maduka yote kuja kumsindikiza mwenzenu,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma, Hilary Gerard amesema kuwa wamepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa kiunganishi thabiti kati ya wafanyabiashara na TRA.

Ameeleza kuwa marehemu aliwasaidia kujenga uhusiano wa maridhiano, uliowezesha ulipaji wa kodi kwa hiari.

“Kwa hakika, ametuachia dhamana ya kuendeleza ushirikiano huo kwa kuboresha mawasiliano baina yetu na wafanyabiashara, kama njia ya kumuenzi,” amesema Gerard.

Marehemu alizaliwa Desemba 9, 1966. Ameacha mjane mmoja, watoto watano wakiwamo wasichana watatu na wajukuu watatu.