Mgunda aongeza nguvu kambi ya Namungo

KOCHA wa Namungo, Juma Mgunda anajiandaa kutua kambini jijini Dodoma ikiwa ni siku chache tangu atoke katika majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ili kuendelea na programu za kujiandaa na msimu mpya.

Katibu wa timu hiyo, Ally Seleman alisema  Mgunda atajiunga na kambi iliyopigwa Dodoma na wachezaji walishaanza kufanya mazoezi chini ya kocha msaidizi Ngawina Ngawina.

“Kocha Mgunda alikuwa katika majukumu ya kitaifa na programu aliziacha chini ya msaidizi wake Ngawina, hivyo ujio wake unakwenda kuongeza nguvu katika maandalizi hayo ya msimu, kuhakikisha anakiandaa kikosi cha ushindani,” alisema katibu na kuongeza;

“Namungo tumealikwa katika michuano iliyoandaa Fountain Gate itakayoanza Agosti 31 Babati, hivyo Dodoma tutaondoka tarehe 29, tunaamini  mechi hizo zitatusaidia kuwapa ushindani wachezaji.”

Alisema baada ya kushiriki michuano hiyo, watamsikiliza kocha Mgunda anachokitaka ili kuhakikisha kambi inafanyika kwa umakini mkubwa utakaoendana na ushindani wa Ligi Kuu.

“Ligi ni ngumu inahitaji maandalizi ya nguvu ili kuweza kuukabili ushindani, ndiyo maana tumesajili wachezaji wapya na wengine tumewaacha kulingana na ripoti ya kocha ilivyokuwa inataka,” alisema.