MHANDISI MUTASINGWA ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UBUNGE BUKOBA MJINI, AAHIDI KUTEKELEZA MURADI YA WATANGULIZI WAKE

Na Diana Byera, Bukoba.

MGOMBEA ubunge Jimbo la Bukoba mjini Mhandisi Johnston Mutasingwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo huku akiahidi kutekeleza miradi mikubwa yote iliyoachwa na watangulizi wake

Akizungumza baada wa kuchukua fomu hiyo Mhandisi Mutasingwa amewataka Wanaccm kuwa wamoja na kuvunja makundi yote ili washirikiane kunadi sera za chama hicho, na kuwezesha kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

“Niwaombe wana- CCM wote tuvunje makundi, tuwe wamoja maana wote lengo letu ni moja kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi katika kura za madiwani, wabunge na Rais” amesema Mhandisi Mutasingwa.

Amesema yupo tayari kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Bukoba mjini na kuhakikisha miradi yote itakayoletwa katika Jimbo hilo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bukoba Mjini Melkion Komba amesema mgombea ametimiza vigezo vyote na kusisitiza kwamba tarehe ya mwisho ya wagombea kurejesha fomu ni Agosti 27, mwaka 2025.